Habari za Punde

UJUMBE WA MADAKTARI KUTOKA CHUO KIKUU CHA JOHNS HOPKINS CHA MAREKANI WAKUTANA NA WAZIRI WA AFYA ZANZIBAR

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Hamad Rashid Mohamed akizungumza na ujumbe wa  Madaktari kutoka Chuo Kikuu cha JOHNS  HOPKINS cha Marekani  ulipofika ofisi ya Wizara ya Afya  Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Ujumbe wa Madaktari kutoka Chuo Kikuu cha JOHNS  HOPKINS uliofika Zanzibar kuja kuangalia miradi ya Malaria inayofadhiliwa na Marekani kwa upande wa Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akisalimiana na kiongozi wa msafara wa Madaktari kutoka Chuo Kikuu cha JOHNS HOPKINS Nchini Marekani Bi Ellen J MacKenzie alipofika ofisini kwake  Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar  kwaajili ya kujitambulisha  .
Mkurugenzi wa Chuo cha JOHNS  HOPKINS cha Marekani kwa Tanzania  Waziri Nyoni akizungumzi na Waandishi wa habari, hawapo pichani kuhusiana na ujumbe wa madaktari uliofika nchini kukagua miradi ya malaria kwa upande wa Zanzibar. Picha na Abdalla Omar-Maelezo Zanzibar.  

Na Ali Issa –Maelezo Zanzibar  23/10/2018
Wizara ya Afya Zanzibar imesema kiwango cha ugonjwa wa Malaria kilichopo nchini kwa sasa kinaridhisha kutokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa kuutokomeza ugonjwa huo nchini.
Ugonjwa huo kwa sasa upo chini ya asilimia moja na hivyo juhudi mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Wadau tofauti ili kuutokomeza nchini.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed ameyasema hayo alipokutana na ujumbe wa Madaktari 20 kutoka Chuo cha Udaktari cha Johns Hopkin Bloomberg cha Marekani huko Ofisini kwake Mnazi mmoja mjini Zanzibar.
Waziri Hamad amesema amefurahishwa na ujio huo kutoka Marekani uliokuja kukagua Miradi ya kupambana na ugonjwa wa Malaria inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani.
Amesema kupitia ziara hiyo Wageni hao wataweza kufanya tathmini ya kiwango cha Malaria nchini na kuweza kujua mafanikio  na changamoto zilizopo katika uendeshaji wa Mradi huo wa kupambana na Malaria.
Hata hivyo Waziri wa Afya aliwaelezea Wageni hao mafanikio yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuubakisha ugonjwa huo chini ya asilimia moja nchini.
Waziri wa Afya ameendelea kutoa wito kwa wananchi 
kuendelea kutumia Vyandarua vilivyotiwa Dawa na 
kuyaweka mazingira safi ili kujikinga na Mbu wanaoweza 
kueneza ugonjwa huo.
Amewashukuru Madaktari hao kwa juhudi wanazozichukuwa na kuwaomba kuzidisha mashirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili wananchi wa chini waweze kufaidika.
Hata hivyo aliwaomba kufanya Tafiti nyengine za Maradhi mengine yasio ambukiza ili kuweza kuyatokomeza nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa cha JOHN HOPKINS nchini Tanzania Waziri Nyoni aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya namna inavyopambana kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini.
Amesema mafanikio hayo pia yanatokana na juhudi zinazofanywa na Chuo cha JOHN HOPKINS kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kuhakikisha afya za Wananchi wa Zanzibar zinazidi kuimarika.
Aidha Mkurugenzi Nyoni amelipokea ombi la kufanya tafiti za maradhi mengine yasiyoambukiza ili wayafanyie kazi kulingana na hali zinavyoruhusu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.