Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Ali Mohamed Sein, akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa Jamuhuri ya China Ikulu Zanzibar, alipofika kuonana na Rais Dk. Shein kwa mazungumzo leo.18/11/2018.Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya
maendeleo sambamba na kukuza uhusiano uliopo.
Dk. Shein amesema hayo
leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa
Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Cai Defeng, aliopo nchini Tanzania kwa ziara ya
siku sita kufuatia mwaliko wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Job Yustino Ndugai.
Katika mazungumzo hayo,
Rais Dk. Shein alitoa shukurani kwa Serikali ya Watu wa China kwa kuendelea
kuiunga mkono Zanzbar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo
imekuwa chachu katika kukuza uchumi wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo
kati yake na Jamhuri ya Watu wa China ambapo ujio wa kiongozi huyo
unathibitisha ukweli huo.
Alieleza kuwa China na
Zanzibar zina historia kubwa, tangu wakati wa kupigania uhuru hadi hivi leo,
ambapo nchi hiyo ilikuwa ya mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya
Januari 12, 1964.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar
alipongeza uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya (CCM) na chama cha
Kikomunisti cha China (CPC) chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping wan chi hiyo.
Dk. Shein alizipongeza
hatua za Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuunga mkono jitihada za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo
afya, elimu, kilimo, maji safi na salama, miundombinu, viwanda na mengineyo
Dk. Shein alipongeza
juhudi kubwa zinazochukuliwa na nchi hiyo katika kutoa nafasi za masomo kwa
wanafunzi kutoka Zanzibar sambamba na mashirikiano yaliopo kutoka Jimbo la
Jangsu katika kuimarisha sekta ya afya.
Alipongeza azma ya
Jamhuri ya Watu wa China kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika
sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo uchumi wa bahari, uvuvi, uwekezaji
pamoja na gesi asilia na mafuta.
Dk. Shein aliwakaribisha
wawekezaji kutoka China kuja kuekeza Zanzibar sambamba na watalii wa nchi hiyo
kuitembelea Zanzibar kutokana na vivutio kadhaa vilivyopo hapa nchini.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa uchumi wa Bahari ni miongoni mwa mambo muhimu yaliopewa kipaumbelea na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uchumi wake hasa ikizingatiwa
kuwa ni mwa wanachama wa nchi zinazopakana na
bahari ya Hindi (IORA).
Pia, Rais Dk. Shein
alipongeza mashirikiano yaliopo kati ya Bunge la Jamhuri ya Watu wa China na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Job Yustino Ndugai kwa kumualika kiongozi huyo kuja kuitembelea
Tanzania.
Aidha, Rais Dk. Shein
alimuhamikikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kuthamini juhudi za Jamhuri ya watu wa China chini ya kiongozi wake
Rais Xi Jinping kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli
ataendeleza uhusiano uliopo kati ya nchini mbili hizo kwa kutambua ushirikiano
wa kihistoria ambao umeanzishwa na waasisi wa Mataifa hayo.
Nae, Makamu Mwenyekiti
wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Cai Defeng alimuhakikishia Rais Dk. Shein
kuwa Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na
kuimarisha ustawi wa jamii.
Alimuhakikishia Dk.
Shein kuwa China iko tayari kuisaidia Zanzibar katika kuendeleza uchumi wa
bahari, uvuvi, utalii pamoja na sekta nyengine huku akiahidi kuimarisha sekta
ya uwekezaji hapa Zanzibar kwa kuwaalika wawekezaji wa China kuja kuwekeza
Zanzibar.
Aidha, kiongozi huyo
alipongeza mazungumzo aliyoyafanya na viongozi wa Mabunge hapa nchini pamoja na
kueleza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Bunge la nchi yake na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Sambamba na hayo, alipongeza
mapokezi makubwa aliyoyapata pamoja na ukarimu wa wananachi na viongozi wa
Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment