Habari za Punde

UWEKAJI WA JIWE LA MSINGI JENGO LA UGONJWA YA AKILI WAFANYIKA ZANZIBAR

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Asha Abdulla Juma kulia  akiwa pamoja na Mshirika wa Maendeleo Trond Mohn kutoka Heuckland Hospital Norway wakikata utepe katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi jengo la magonjwa ya Akili Kidongo chekundu mjini Unguja.
Na Maryam Kidiko –Maelezo Zanzibar.                                 16/11/2018.
Kukamilika kwa ujenzi wa Jengo jipya la maradhi ya Akili katika Hospitali ya maradhi hayo Kidogo chekundu, kutaimarisha mfumo mzuri wa upatikanaji wa huduma za matibabu ya maradhi hayo.
Hayo aliyasema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Abdulla wakati akiweka Jiwe la Msingi la Jengo hilo huko Kidongochekundu mjini Unguja.
Amesema kwa muda mrefu matibabu ya maradhi hayo yalikosa mfumo imara uliotokana na changamoto za kiutendaji ikiwemo uhaba wa rasilimali.
Hata hivyo amesema Serikali itaendelea na juhudi zake za kuimarisha matibabu katika kila eneo ikiwemo Afya ya akili.
Katibu huyo ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ni kuhakikisha inaimarisha huduma za matibabu ya afya ili kila mwananchi wa Zanzibar aendelee kuyafurahia maisha yake.
Amefahamisha kuwa Wagonjwa watakuwa katika mazingira mazuri zaidi katika Wodi ikiwa ni pamoja na kuwepo Wodi za Watoto.
Aidha amesema kutakuwa na Vitanda 100 katika Jengo hilo ili kurahisisha matibabu ya Wagonjwa hao
Katika kuimarisha vyema matibabu hayo tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya imeshapeleka Madaktari kusomea masomo ya afya ya akili na Saikolojia katika nchi mbalimbali.
Akielezea kuhusu mashirikiano na Hospitali ya Houckland nchini Norway amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikishirikiana vyema na Hosptial hiyo hasa katika
kujenga jengo la Watoto la Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.  
Aidha alisema kumalizika kwa Jengo hilo kutapelekea kuimarika zaidi kutolewa huduma za Maradhi ya akili ambayo ilikosa mfumo muhimu kwa muda mrefu katika huduma ya ugojwa huo.
 Hata hivyo alisema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha wanaimarisha huduma za Maradhi ya akili katika hospitali hiyo jambo ambalo litaleta faraja kwa wagojwa watakaopelekwa katika Hospitali hiyo.
“Hatua mbali mbali zinachukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wagonjwa wa maradhi ya akili, ”alisema Katibu Mkuu Asha.
Pia alisema jengo hilo litakapomalizika Serikali tayari imeandaa madaktari  wa kutosha wa magojwa hayo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali kuu ya Mnazimmoja Dkt. Ali Salim alisema kuwa kumalizika kwa Jengo hilo kutapelekea kuboreshwa huduma za afya ya akili.
Sambamba na hayo Dkt. Ali alisema kutokana na kuboreshwa kwa huduma hiyo Wananchi nao watahamasika kupeleka wagojwa wao  kupata huduma zinazostahiki na kuacha imani potofu walizokua nazo.
Alisema Jengo hilo jipya la wagojwa wa akili linatarajiwa kumalizika Novemba 2019 chini ya ufadhili wa Hospitali ya Heuckland ya nchini Norway ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Heuckland Elvind Hanseen alisema lengo la kusaidia ujenzi huo ni kutaka kuona huduma za wagonjwa wa akili kuboreshwa na kuongeza ufanisi kwa wafanyakazi katika utendaji wa kazi zao.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.