Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Akutana na Balozi wa UAE Nchini Tanzania.

Balozi Mpya Bwana Khalifa Abdulrahman Mohamed Al – Marzooqi wa Muungano wa Falme za Kiarabu {UAE} kati kati akisabahiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza umuhimu wa Wawekezaji wa Muungano wa Falme za Kiarabu kutumia fursa za Uwekezaji zilizopo Tanzania kuanzisha Miradi yao.
Balozi Khalifa Abdulrahman Mohamed Al – Marzooqi wa Muungano wa Falme za Kiarabu {UAE}akimueleza Balozi Seif shauku ya Wafanyabiashara wa Mataifa ya Muungano wa Falme za Kiarabu kutaka kuwekeza Zanzibar kutokana na mazingira mazuri ya Miradi ya Kiutalii.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif AliIddi alisema Zanzibar itaendelea kuwa karibu na Muungano wa Falme za Kiarabu {UAE} katika dhana nzima ya kuimarisha Sekta ya Uchumi na Ustawi wa Jamii wa Wananchi wa pande zote mbili.
Alisema hatua hiyo inakuja kufuatia mafungamano makubwa yaliyopo kati ya Zanzibar na Muungano wa Mataifa hayo hasa katika Sekta ya Biashara kwa usafirishaji wa bidhaa za Matunda na Viungo.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa Muungano wa Falme za Kiarabu {UAE} Bwana Khalifa Abdulrahman Mohamed Al – Marzooqi aliyefika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Alisema kutokana na utulivu mkubwa uliopo Zanzibar ulioambatana na Miundombinu sahihi ya Uwekezaji Wawekezaji wa Mataifa hayo wana fursa nzuri ya kutumia nafasi hiyo ikiwa ni njia ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo kwa sehemu hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi huyo wa Muungano wa Falme za Kiarabu { UAE} kwamba wakati umefika kwa watendaji wake kufuatilia kwa kina mambo yaliyokubalika katika Mikutano na Vikao kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar aliyoifanya katika Mataifa hayo rafiki miezi michache iliyopita.
Mapema  Balozi Mpya wa Muungano wa Falme za Kiarabu Bwana Khalifa Abdulrahman Mohamed Al – Marzooqi alisema Mataifa ya Muungano huo yamelenga kufungua Ubalozi Mdogo Visiwani Zanzibar Mwaka ujao.
Bwana  Khalifa Abdulrahman alimueleza Balozi Seif kwamba uamuzi wa kufungua Ofisi hiyo unakusudia kusogeza karibu zaidi huduma za mawasiliano pamoja na zile za Kidiplomasia Visiwani Zanzibar.
Balozi huyo wa Muungano wa Falme za Kiarabu alisema aliwahi kukutana kwa mazungumzo na Vyama vya Wafanyabiashara wenye Viwanda wa Nchi Wanachama za Sharja, Dubai na Abu Dhabi kabla ya kuripoti kazi yake ya Kidiplomasia Nchini Tanzania.
Alisema Mikutano hiyo imemuwezesha kuelewa kwamba Wafanyabiasha wengi wa Mataifa hayo wameonyesha nia ya kutaka kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar wanazozifuatilia kupitia mitandao mbali mbali ya Mawasiliano Duniani.
Bwana Khalifa Abdulrahman Mohamed Al – Marzooqi tayari ameshatumikia kazi ya Kidiplomasia katika Mataifa mbali mbali Duniani ikiwemo Brazil, Korea pamoja na Uturuki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.