Habari za Punde

Mitihani ya kidato cha Pili Zanzbiar yafutwa

Na. Thabit Madai,Zanzibar. 

Wizara ya  Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imetangaza kufuta kwa mitihani ya kidato cha Pili iliyoanza leo Disemba 3  kutokana na kukiukwa kwa utaratibu wa ufanyaji wa mitihani ikiwemo kuvuja kwa mitihani hiyo. 

Akitoa taarifa kwa Waandishi wa habari ofisini kwake,  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali zanzibar, Riziki Pembe Juma amesema hatua hiyo imekuja mara baada ya kubaini na kujiridhisha ukiukwaji mkubwa wa Taratibu za mitihani hiyo ya kidato cha pili ilianza leo ambapo ilitarajiwa   kumalizika Decembar 11 mwaka huu. 

“Wizara ya Elimu imepata taarifa za kuaminiwa kuwa baadhi ya watu wasiohusika wamepata baadhi ya mitihani kabla ya wakati wa  kufanywa kwa mitihani hiyo na kusambazwa kwa njia za kieletroniki ambapo ni kinyume na utaratibu wa ufanywaji wa mitihani”  alisema waziri wa elimu Riziki pembe juma. 

Aidha amesema wizara imefuta mitihani hiyo ili kutenda haki na usawa kwa watahiniwa wote kwa kufuata utaratibu wa ufanywaji wa mitihani. 

Kwa upande mwingine alisema wizara inatoa onyo kali kwa watu wote walioshiriki katika uvujishaji na usambazaji wa mitihani inayoendelea kuwatafuta kwa kutumia vyombo vya husika ili kuwachukulia hatua kali za kisheria 

Alisema wizara inasikitishwa sana na kitendo hicho ambacho kimeleta usumbufu na hasara kubwa kwa serikali na kwa jamii kwa ujumla. 

 Hata hivyo waziri alitangaza kuwa wanafunzi wote wanatakiwa kuendelea na masomo hadi pale serikali itakapo tangaza tena tarehe ya kufanyika kwa mitihani hiyo 

Jumla ya wanafunzi 34,848 kati yao wanaume 16,642 na wanawake 18,206 ndio wahitimu wa kidato cha pili kwa mwaka 2018 kutoka skuli 180 za serikali na binafsi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.