Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Afungua Mafunzo ya Ukusanyaji Taarifa za Afya Unaoshirikisha Nchi 23.

 
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akifungua mafunzo ya ukusanyaji taarifa za za vituo vya afya vijijini kupitia simu za mkononi katika Hoteli ya Ngarawa, Bububu Wilaya Magharibi ‘A’ Unguja.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oslow Prof. Cristen Mvinje akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo ya ya ukusanyaji taarifa za afya vya vijijini yanayofanyika Hoteli ya Ngarawa, Bububu Wilaya Magharibi ‘A’
 Picha ya pamoja ya Waziri wa Afya na washiriki wa mafunzo ya ukusanyaji taarifa za afya za vituo vya vijijini kwa kutumia simu za mkononi yanayofanyika Hoteli ya Ngarawa Wilaya Magharibi ‘A’.Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali – Maelezo.
Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Hamad Rashid Mohamed amesema kupatikana kwa taarifa sahihi za afya kupitia mfumo unaoaminika kutatoa mchango mkubwa kwa Taifa katika kuandaa mipango yake ya maendeleo
Waziri Hamad alieleza hayo alipokuwa akifungua mkutano wa mafunzo ya ukusanyaji taarifa za afya kutoka vituo vya afya vya vijijini kwa kutumia simu za mkononi kupitia mfumo mpya  wa DHIS unaofanyika Hoteli ya Ngarawa, Bububu Wilaya ya magharibi ‘A’.
Alisema mfumo huo mpya wa ukusanyaji taarifa utaisaidia Wizara yake kupata taarifa muhimu na zilizosahihi kwa haraka kutoka vituo vya afya vya mijini na vijijini ambazo zitatumika  katika maamuzi na kuongeza ufanisi.
Alisema nchi nyingi za Afrika ziliopo pembezoni mwa Jangwa la Sahara zinakabiliwa na tatizo la wafanyakazi wa sekta ya afya katika kupata taarifa sahihi na mafunzo hayo yanayozishirikisha nchi 23 kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Marekani yatasaidia kupunguza tatizo hilo.
Amebainisha kuwa mfumo huo kwa sasa unatumika katika mataifa mengi duniani na unarahisisha nchi moja kupata taarifa ya nchi nyengine zinazohusu masuala ya afya kupitia simu ya mkononi.
Katika kuhakikisha mfumo huo unakuwa endelevu nchini, Waziri wa Afya alishauri kutolewa mafunzo kwa wananchi mbali mbali wakiwemo wanasiasa ambao wanamchango mkubwa katika vituo vya afya vilivyomo katika majimbo yao .
Alisema kufanyika kwa mkutano wa Kimataifa wa ukusanyaji taarifa kupitia mfumo wa kisasa hapa Zanzibar ni fursa pekee kwa wafanyakazi wa Wizara ya Afya kujifunza na kuthibitisha hali ya utulivu na kuaminiwa kwa nchi yetu.
Akizungumza katika mafunzo hayo Prof. Cristen Mvinje kutoka Chuo Kikuu cha Oslow alisema chuo hicho kimejikita kutoa taaluma kwa watu mbali mbali na kutafsiri kwa vitendo elimu inayotokana na tafiti zilizofanywa na wataalamu katika kuleta maendeleo.
Mshauri wa masuala ya Teknolojia anaefanyakazi Chuo Kikuu Oslow nchini Norway Suleiaman Salum Ali alisema kwa kutumia mfumo huo wafanyakazi wa Wizara ya Afya hawatakuwa na haja ya kutumia Komputa kupata taarifa za vituo vya mashamba.
Alisema Wizara itaweza kufaidika kufanya maamuzi makubwa ya uhakika kwa muda muafaka baada ya kupata taarifa sahihi kutoka vituo mbali mbali vya afya vya vijijini.
Mafunzo hayo ya siku nne ya kukusanya taarifa za afya kutoka vituo vya vijijini kwa kutumia teknolojia ya simu za mkononi yanaendeshwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Oslow na Chuo kikuu cha Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.