Habari za Punde

Mfanyabiashara Maarufu na Mwanamichezo Zanzibar Mhe Mohammed Raza Akabifdhi Vifaa Vya Michezo Kwa Timu za Ligi ya Zanzibar Kwa Mwaka 2018/2019.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Mabingwa wa Soka wa Ligi Kuu ya Zanzibar kwa Mwaka 2018/2019 Timu za JKU na Zimamoto walipofika Ofisini kwake Vuga kukabidhiwa zawadi zao zilizotolewa na Mdau wa Michezo Mohamedraza Hassanaali. 
Baadhi ya Viongozi wa Timu ya JKU wakifuatilia Hotuba ya Balozi Seif hayupo pichani wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa ya kukabidhiwa zawadi zao.
Mdau wa Sekta ya Michezo Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassanaali akisisitiza lengo lake la kuendelea kuunga mkono Sekta ya Michezo.
Balozi Seif Kushoto akimkabidhi zawadi mbali mbali Kamishna wa Zimamoto na Uokozi Zanzibar Abdullah Ali Malimus Timu yake ikishikilia nafasi ya Pili katika Ligi Kuu ya Zanzibar Msimu wa Mwaka 2018/2019.
Kamanda wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar JKU Ali Mtumweni akitoa shukrani kwa niaba ya Wanamichezo wenzake baada ya kupokea zawadi mbali mbali kufuatia Timy yake kuibuka na Ushindi wa Ligi Kuu ya Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha    Wanamichezo Nchini kutumia nafasi yao kwa kuongeza mapambano dhidi ya  kupinga vitendo vya udhalilishaji vinavyoleta sura mbaya katika Jamii na Taifa kwa ujumla.
Alisema Sekta ya Michezo kwa vile ina ushawishi mkubwa miongoni mwa Jamii inaweza kutumika vyema katika mapambano hayo na kuleta mafanikio makubwa katika jitihada za kukabiliana na kadhia hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi ametoa kumbusho hilo wakati akikabidhi zawadi kwa Timu ya Soka ya Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} iliyotwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar kwa Mwaka 2018/2019 na Mshindi wa Pili Timu ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi hafla iliyofanyika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Vifaa hivyo vilivyoambatana na Silingi Milioni 2,000,000/- kwa JKU na Milioni 1,000,000/- kwa Zimamoto vilivyotolewa na Mdau wa Michezo Mohamedraza Hassanaali ni pamoja na Seti za Jezi, Viatu, Mipira, , Pair 40 za Viatu kwa Timu ya Wanawake ya Mpira wa Pete ya JKU pamoja na seti ya Jezi kwa Timu zote za Vikosi vya SMZ.
Balozi Seif alisema suala la udhalilishaji wa kijinsia linalowakumba zaidi Watoto na Akinamama linaleta athari pia katika Nyanja ya Michezo vitendo ambavyo vinapaswa kulaaniwa na Wadau wote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alihimiza uendelezwaji wa nidhamu Michezoni ambayo kwa kiasi kikubwa huleta Heshima kwa Mchezaji mwenyewe pamoja na Taifa kwa ujumla.
Balozi Seif  alisema ni vyema Timu hasa zile za Vikosi zikaonekana kuzingatia zaidi nidhamu kwa kuheshimu maamuzi yanayotolewa na Muamuzi wa mchezo ambayo yanakuwa hayana mjadala kwa Wachezaji.
Amempongeza Mdau wa Michezo Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassanaali kutokana na mchango wake mkubwa ndani ya Sekta ya Michezo kwa kipindi kirefu sasa.
Balozi Seif alisema Mohamedraza ambae ameshafikia hatua ya kuteuliwa kuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya Michezo kipindi kilichopita kutokana na mchango wake mkubwa anastahiki kuitwa Gurudumu la Michezo.
Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo Zanzibar kupitia Serikali yake ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaamua kuimarisha Sekta ya Michezo ili irejee katika hadhi yake ya kutambulika kuwa kituo cha Michezo Kimataifa.
Alikumbusha kwamba Zanzibar imeshawahi kubwa bingwa wa michezo mbali mbali Kimataifa akatolea Mfano Mchezo wa Vinyoya, Soka, Mpira wa Pete pamoja na ule wa Meza.
Mapema mdau wa Michezo Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mohamedraza Hassanaali alisema washirika wa Michezo Nchini wana wajibu wa kuunga mkono Michezo mbali mbali ili kuwapa ari washiriki wa Michezo hiyo hasa wanapokuwa kwenye Mashindano.
Mohamedraza alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba Timu nyingi nchini humalizia mashindano yao katika mazingira magumu hata zile zinazochukuwa ubingwa.
Alisema alilazimika kutekeleza Ahadi yake aliyoitoa kwa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar {ZFA} ya kuwapatia zawadi washindi wa kwanza na wa pili wa Ligi Kuu ya Zanzibar ikiwa kama motisha ya Wachezaji ya kuwaongezea nguvu na ari ya kuendelea kushiriki tena kwenye Mashindano yajayo.
Wakitoa shukrani kwa niaba ya Wanamichezo wenzao Kamanda wa JKU Kanali Ali Mtumweni na Kamishna wa Zimamoto na Uokozi Abdullah Ali Malimus wameupongeza Uongozi wa Kampuni ya ZAT kwa Uzalendo wake wa kusaidia Sekta ya Michezo Nchini.
Makamanda hao walisema kwa pamoja msaada waliopewa na Mdau huyo umekuja wakati muwafaka wakijiandaa kuelekea katika Mashindano tofauti na kuongeza ari kwa Wanamichezo mbali mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.