Habari za Punde

Mhe. Rais Anawathamini Wafanyakazi na Kutambua Mchango Wao - Kassim Majaliwa.

Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli anawathamini na kutambua mchango mkubwa unatolewa na Wafanyakazi katika kuhudumia Watanzania na kamwe hata waangusha.
Waziri Mkuu ameyasema hayo, leo Jijini Dodoma baada ya kuyapokea maandamano ya Shirkisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) yenye lengo la kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusitisha utekelezaji wa kikokotoo kipya na kuagiza kikokotoo kilichokuwepo kiendelee mpaka mwaka 2023 baada ya kuboreshwa.
"Rais anawapongeza kwa maamuzi yenu na kutambua kile alichokifanya kwa kusitisha kikokotoo kipya na amesema hata waangusha," amesema Waziri Mkuu.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi nchini katika hatua zote zitakazopitia katika uandaaji wa kikokotoo kipya kwa kupokea maoni yao kabla ya kuanza utekelezaji wake mwaka 2023.
 Aidha, amewapongeza Wafanyakazi wote nchini kwa kuchapa kazi kwani hata huduma kwa Wananchi zimeboreka. Amesema, Serikali itajitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wafanyakazi wanapewa motisha ya kutosha ili waweze kufanya kazi kwa juhudi na hatimaye kulikomboa Taifa katika umaskini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema ofisi yake imetoa miongozo kwa Wakuu wa Taasisi na Idara za Serikali kupitia Makatibu Wakuu kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais kuhusu kikokotoo.
"Mimi na timu yangu tunaanza ziara nchi nzima kuhakikisha maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais yanatekelezwa kama yalivyotolewa. Vyama vya Wafanyakazi vitusaidie kufuatilia watendaji mikoani kama wanafuata maagizo yaliyotolewa na Mhe. Rais na kama kuna ukiukwaji basi taarifa zitolewe." amefafanua Waziri Jenista.
Nae, Makamu wa Rais TUCTA, Qambos Sule amesema wafanyakazi wamefarijika kwa maamuzi aliyoyafanya Mhe. Rais ya kusitisha kikokotoo kipya. Amesema, wao kama vyama vya wafanyakazi wako  pamoja na Serikali kuhakikisha wafanyakazi wanaishi maisha mazuri ya kustaafu.
Mnamo Desemba 28, 2018,  Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alikutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini, watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii na Mawaziri wa wizara husika, kwa ajili ya kujadili masuala yahusuyo mafao ya wafanyakazi ikiwemo kuhusu kanuni mpya ya kukokotoa mafao ya wastaafu ambapo.
Katika kikao hicho Rais Magufuli alisitisha kutumika kwa kikokotoo hicho kwa wastaafu ambapo mafao ya mstaafu yalishushwa kutoka kulipwa asilimia 50  kutoka  kikokotoo cha zamani mpaka asilimia 25 kama kikokotoo kipya.
Nikinukuu kauli yake katika kikao hicho Rais Magufuli alisema kuwa; "Mtu anayestaafu anatakiwa kuheshimiwa, amelitumikia taifa hili, amejitoa, ni shujaa, kustaafu bila kufukuzwa ni heshima, hatakiwi kupata shida, nimeamua kikokotoo kiendelee katika kipindi hiki cha mpito, ambapo ni hadi mwaka 2023."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.