STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 01.01.2019

Kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa maendeleo ya Zanzibar
Awamu zote Saba za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanya
jitihada mbali mbali za kuimarisha sekta ya michezo ikiwemo miundombinu ya michezo
hasa ujenzi wa viwanja.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema
hayo leo huko katika uwanja wa Gombani Pemba mara baada ya kushiriki kikamilifu
katika Bonanza maalum la Mazoezi ya Viungo ambalo lilianzia Wawi Matrekta hadi uwanja
wa Gombani Chake Chake Pemba.
Mazoezi
hayo ya viungo yalivishirikisha vikundi mbali mbali vya mazoezi kutoka Unguja,
Tanzania Bara pamoja na wenyewe kutoka Pemba ambapo pia, yaliwashirikisha
viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd
pamoja na wananchi.
Katika
hotuba yake aliyoitoa mara baada ya mazoezi hayo ambayo hufanyika Kitaifa kila
mwaka mnamo tarehe mosi ya mwezi wa Januari, Dk. Shein alisema kuwa katika
Awamu ya mwanzo ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ulijengwa uwanja wa Amaan
ambao ni wa kisasa wenye viwango vya Kimataifa uliofunguliwa rasmi mwaka 1970.
Aidha,
katika Awamu ya Nne Marehemu Sheikh Idriss Abdulwakil alianzisha ujenzi wa
uwanja wa Gombani Pemba.
Katika
utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba imefanya jitihada kubwa za kuimarisha
miundombinu ya michezo ikiwa ni pamoja na kukifanyia matengenezo na kukiwekea
majani ya bandia na mpira wa kukimbilia kiwanja cha Amaan na Gombani.
Vile
Vile, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China kimejengwa upya kiwanja cha michezo cha Mao Tse Tung ambacho
kinaweza kutumika kwa michezo mbali mbali .
Kwa
maelezo ya Rais Dk. Shein kiwanja hicho kinaweza kutumika kwa michezo ya mpira
wa mikono, mpira wa wavu, mpira wa vikapu, mpira wa pete na mpira wa miguu
hatua ambayo itaondokana na tatizo la uhaba wa viwanja vya michezo na kusaidia
kuimarisha sekta ya michezo.
Pia,
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali imeanza hatua ya ujenzi wa kiwanja kimoja
cha michezo kwa kila Wilaya ya Zanzibar kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya CCM
ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020.
Aliongeza
kuwa Serikali imekamilisha ujenzi wa uwanja wa
Kitogani katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja na hatua za
ujenzi wa kiwanja cha michezo cha Kishindeni katika Wilaya ya Micheweni na
kiwanja cha Kangani katika Wilaya ya Mkoani zinaendelea.
Rais
Dk. Shein alieleza kuwa maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa Wilaya ya Kaskazini A
huko Mkokotoni nayo yataanza hivi karibuni.
Pamoja
na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa bado ana imani kuwa iwapo utawekwa
mbele uzalendo, ubunifu na kurudisha ari na hamasa ya kupenda timu za nyumbani
kuliko za nje timu za nyumbani zitaweza kufanya vizuri katika mashindano.
Aliwahimiza
wananchi kuzionea ufahari na kuzipenda timu za za nyumbani kwani mtu kukipenda
chake si ila isipokuwa ni wajibu jambo ambalo ni ishara ya uzalendo na
litasaidia kuwapa moyo wachezaji ili michezo iimarike zaidi nchini.
Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafanyabiashara na sekta binafsi kuziunga
mkono juhudi za Serikali katika sekta ya michezo kwani michezo ina nafasi nzuri
katika kuzitangaza biashara na inasaidia katika matamasha na kampeni za
shughuli zinazofanywa na asasi za kiraia.
Alieleza
jinsi anavyothamini jitihada za wawekezaji wote walioahamasika kuweka huduma za
michezo katika hoteli za kitalii akiwemo Said Salim Bakhressa aliyeanzisha
kichezo ya maji katika hteli ya Verde pamoja na mwekezaji Subash Patel
aliyejenga kiwanja cha gofu katika hoteli ya Sea Cliff, Magapwani.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein alitoa wito kwa
Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Habari,
Utalii na Mambo ya Kale kuendelea kushirikiana ili walitumie Tamasha la Utalii
la Zanzibar la kila mwaka katika kukuza michezo na kuimarisha sekta ya utalii
ambayo inachangia pato la Zanzibar.
Dk.
Shein aliupongeza uongozi wa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Baraza la Taifa la Michezo pamoja na Chama cha Mazoezi ya Viungo (ZABESA) kwa
maandalizi mazuri ya bonaza la mwaka huu ambalo kwa mara ya kwanza limefanyika
kisiwani Pemba.
Nae
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Micezho Balozi Ali Abeid Karume alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya michezo.
Mapema
Kamishna wa Michezo Sharifa Khamis alieleza kuwa Wanamichezo wamefarajika na
juhudi za Rais Dk. Shein anazozichukua katika kuhakikisha michezo inakua na
kuendelea na ndio maana akaamua kufanya matengenezo ya viwanja vya Amaan,
Gombani, Mao Tse Tung.
Nao
Uongozi wa ZABESA katika risala yao walieleza umuhimu wa mazoezi kwa mwanaadamu
huku wakitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kuwakubalia maombi yao
likiwemo kufanyika kwa Bonanza hilo kisiwani Pemba mwaka huu.
Pia,
ujenzi wa viwanja vya kila Wilaya, kuwapatia eneo kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja
wa Taifa pamoja na kuziwezesha timu za Taifa kushiriki mashindano ya Kitaifa.
Pia,
Kamishna huyo alimuarifu Rais Dk. Shein kuwa eneo la ujenzi wa Uwanja wa kisasa
wa michezo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 huko Tunguu Wilaya ya Kati
Mkoa wa Kusini Unguja limeshapatikana na limeshaanza kupimwa.
Katika
hafla hiyo Rais Dk. Shein alitoa vyeti maalum kwa Vikundi Shiriki pamoja na
waazilishi na viongozi wa ZABESA ambapo pia, Balozi Seif Ali Idd nae alitoa
vyeti maalum kwa wadhamini wa Bonanza hilo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment