Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohemed Shein Ahudhuria Taarab Rasmin ya Kusherehekea Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar Uwanja wa Kufuruhishia Watoto Tibirinzi Pemba Jana Usiku.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa amesimama wakati ukipigwa Wimbo wa Taifa baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kufurahishia Watoto Tibirinzi Chakechake Pemba, kulia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na kushoto Waziri wa Vijana Michezo Sanaa na Utamaduni Balozi Ali Karume, Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Vijana,Utamaduni,Sanaa na Michezo Omar Hassan ‘King’
amesema tayari Wizara  hiyo imekipatia Kikundi cha Taarabu cha Taifa ofisi za kuendeshea shughuli zake pamoja na kuwa na bajeti ili kukidhi mahitaji ya msingi.

Amesema pamoja na mambo mengine, Wizara imetekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali ili kukiwezesha kikundi huicho kufanya shughuli zake kwa ufanisi pamoja na kuleta ustawi bora wa wasanii wanaokitumikia.

King, amesema hayo jana katika Uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi Chake-chake Pemba, katika taarabu maalum iliyoandaliwa, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alikuwa mgeni rasmi katika taarabu hiyo, ambapo mamia ya wananchi kutoka mikoa yote ya Zanzibar walijumuika na kukonga nyonyo zao vilivyo.

Akitoa taarifa za utekelezaji wa maagizo hayo, alisema tayari wasanii wa kikundi hicho wameanza kupokea mirahaba kutokana na nyimbo 12 walizozisajili pamoja na kujiingizia mapato kutokana na ushirikiano uliopo kati ya kikundi hicho  na baadhi ya taasisi, kama vile ZSTC.

Katika hafla hiyo, kikundi hicho kilicho chini ya Uenyekiti wa Msanii nguli Idd Suweid, kiliibuka na nyimbo kadhaa, zikiwemo zile zenye mnasaba na Mapinduzi, ambapo magwiji wa sanaa hiyo walighani na kukonga vilivyo nyonyo za watazamaji/wasikilizaji.

Miongoni mwa nyimbo zilizounogesha usiku huo  ni pamoja na ‘’miaka 55 ya Mapinduzi” iliyoimbwa na Pro. Gogo, “anaetowa ni Mola’’ iliyoghaniwa na al-anisa Sada Mohamed, ‘tarehe 11 (Idd Siweid), ‘‘Ni yeye’’ pamoja na ‘’umewashuka”  iliyoimbwa an al-anisa Amina Ramadhan.

Nyengine ni “Wahoi’’, “Njoo kwa mtu mkweli’’ (al-anisa Rukia Ramadhan), “maisha ya Vijijini’’ iliyoghaniwa na chiriku Hilda Mohamed, “mpewa hapokonyeki” , “kama kupenda ni dhara’’ iliyoimbwa na ‘sauti ya Zege’ Makame Faki pamoja na ‘’ninae’’ iliyoghaniwa vyema na mpendwa na wengi Idd Suweid.

Kikundi cha Taarabu cha Taifa kina jumla ya wasanii 35 wanaotoka katika vikundi saba vya taarabu hapa Zanzibar.

  
Abdi Shamnah, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.