Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar,Ikulu leo, kuhusiana na Maendeleo ya Miradi mbalimbali ya Wizara hiyo,uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na
Mazao ya Bahari ili kwenda sambamba na Sera ya uchumi wa bahari.
Hayo aliyasema leo
wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Ikulu
mjini Zanzibar ambapo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd
nae alihudhuria ambapo uongozi huo ulieleza maendeleo ya miradi mbali mbali
inayoendeshwa katika Wizara hiyo.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuwa na Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na Mazao ya Bahari hasa
ikizingatiwa mazingira ya Zanzibar na uchumi wake.
Alieleza kuwa ni jambo
la busara kuwepo kwa Taasisi hiyo hapa Zanzibar ambayo itakuwa na umuhimu
mkubwa kwa Zanzibar pamoja na wananchi wake na kuipelekea Zanzibar kutekeleza
ipasavyo uchumi wa bahari kwa vitendo.
Alieleza kuwa tayari
Zanzibar ni mwanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazopakana na Bahari ya Hindi
(IORA), hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati madhubuti katika kufikia
malengo, makubaliano na maazimio ya Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kutekeleza
kwa vitendo uchumi wa bahari.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa mbali ya uwepo wa Jumuiya hiyo ya (IORA) pia, Novemba mwaka jana
2018 alihudhuria Mkutano wa Uchumi wa Bahari uliofanyika mjini Nairobi Kenya
kuanzia Novemba 26 hadi 28 ambapo mbali ya mambo mengineyo mkutano huo pia, ulijikita
na masuala ya uchumi wa bahari hasa kwa nchi zilizopakana na Bahari ya Hindi.
Rais Dk. Shein pia,
alieleza juhudi za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kuanzisha viwanda vya uvuvi hapa nchini, azma ya kuanzisha
Chuo cha Ubaharia pamoja na kuiimarisha Kampuni yake ya Uvuvi.
Akieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji
maji, Rais Dk. Shein alisema kuwa umefika wakati kwa Zanzibar kuongeza ukubwa
wa eneo la kilimo cha umwagiliaji maji kwani mradi huo una umuhimu mkubwa kwa
Wazanzibari hasa ikizingatiwa kuwa chakula cha wali ndio kilichopewa kipaumbele
na jamii.
Alieleza kuwa
matarajio ya Serikali ni kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji wa mpunga
kutokana na mradi huo mkubwa.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliupongeza uongozi wa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa mashirikiano katika kazi ni
suala la lazima sambamba na kufanya kazi kwa kufuata maadili, sheria na kanuni
za kazi ambayo yanaleta usalama mkubwa kazini.
Akisisitiza suala zima
la mashirikiano kazini, Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuendelea
kuwaongoza vyema watendaji waliochini yao huku akiwaeleza malengo na madhumuni
ya kuwepo kwa vyeo na utofauti uliopo kati ya kiongozi na anaeongozwa.
Dk. Shein alisisitiza
umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja hasa ikizingatiwa kuwa kila mmoja ana
majukumu yake hasa wakizingatia kuwa wanaowafanyia kazi ni wananchi.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alitoa pongezi kwa uongozi wa Wizara hiyo
na kusisitiza haja ya kufanya kazi kwa juhudi hasa ikizingatiwa kuwa Wizara
hiyo ni tegemeo kubwa kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na kubeba mambo muhimu
katika maisha yao.
Mapema Waziri wa ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Rashid Ali Juma alieleza maendeleo ya mradi
wa Usimamizi wa shughuli za Uvuvi wa Kanda ya Kusini Magharibi mwa Bahari ya
Hindi (SWIOFish) ambao ni mradi wa miaka sita ulioanza Juni 22,2015 hadi
Septemba 2021.
Alieleza kuwa mradi
huo umetayarishwa kwa dhamira ya kuongeza faida kiuchumi, kijamii na
kimazingira kwa nchi za Kusini Magharibi mwa Barahari ya Hindi (SWIO) kutokana
na matumizi endelevu ya uvuvi wa bahari ambao hivi sasa unatekelezwa na nchi
tatu ambazo ni Tanzania, Msumbiji na Comoro.
Pia, Waziri Juma alieleza
kuwa Ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji maji unaotekelezwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo wa Benki ya Exim-Korea ambao ni miongoni
mwa juhudi na mikakati ya Serikali kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo.
Pia, alieleza kuwa
mradi huo pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Umwagiliaji maji wa
Zanzibar ambapo mkataba wake ulitiwa saini tarehe 6 Disemba 2018 baina ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya hiyo na Kampuni ya Ujenzi
ya KOLON- HANSON JV kutoka Korea utakaogharimu Dola za Kimarekani milioni 64.3.
Aliongeza kuwa Mradi
huo utajumuisha ujenzi wa miundombinu ya mitaro ya umwagiliaji, mabwawa manne
makubwa, kuchimba visima 49 na kuweka pampu zake, ujenzi wa maeneo ya kuanikia
mpunga na kukata vishamba pamoja na kuweka sawa ardhi.
Alieleza kuwa mradi
huo utajenga na kuendeleza eneo litakalokuwa na jumla ya hekta 1,524 (Eka
3,810) zitakazojengwa katika mabonde saba ya umwagiliaji maji kwa Unguja na
Pemba ambayo ni Cheju, Kinyasini, Kibokwa, Kilombero,Chaani, Makwararani na
Mlemele.
Alisisitiza kuwa lengo
kuu la mradi huo ni kuimarisha usimamizi makini wa uvuvi wa kipaumbele kuanzia
ngazi ya Kikanda, Kitaifa na Kijamii.
Pamoja na hayo, Waziri
huyo alieleza lengo kuu la usimamizi wa Serikali katika uchimbaji wa mchanga na
usafirishaji wake ambalo ni kuhakikisha kuwa rasilimali hiyo inapatikana
kikawaida kwa matumizi ya wananchi na kwa bei nafuu kwa mujibu wa kanuni na
Sheria zilizopo.
Uongozi wa Wizara hiyo
ulieleza kufarajika na ushauri, maelekezo wanayoyapata kutoa kwa Rais Dk. Shein
ambayo yamekuwa chachu katika utendaji wa kazi zao huku wakitumia fursa hiyo
kusisitiza kuwa wataendelea na ushirikiano mkubwa walio nao ili kuweza
kuendelea kupata mafanikio makubwa zaidi katika Wizara hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment