Habari za Punde

Uzinduzi wa Barabara Mpya ya Kiwango cha Lami Kutoka Kijitoupele Hafi Fuoni Mambosasa Wilaya ya Magharibi B Unguja.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika viwanja vya Mzee Mgeni Fuoni Mambosasa, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Barabara ya Kijitoupele hadi Fuoni Mambosasa iliojengwa kwa kiwango cha lami.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yameleta usafiri wa uhakika wa barabara  bora mjini na vijijini hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa Barabara ya Kijitoupele hadi Fuoni Mambosasa huko katika uwanja wa Mzee Mgeni Fuoni Mambosasa Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 55 ya Mapinduzi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 mipango ya maendeleo ndipo iliopoanza ikiwa ni pamoja na kujenga barabara zilizo bora.

Rais Dk. Shein alisema kuwa kabla ya Mapinduzi hapakuwa na barabara zenye hadhi na kiwango cha ubora kama ilivyo hivi sasa katika maeneo yote ya Zanzibar.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa mafanikio hayo yote yametokana na uongozi bora wa ASP hadi  hivi leo kuwa CCM, ambapo kwa kutambua umuhimu wa miundombinu ya barabara, ndipo imeweka kipaumbele hicho.

AlIeleza kuwa kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeimarika zaidi, mara baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 tofauti na  ilivyokuwa hapo kabla ya Mapinduzi hayo.

Dk. Shein aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Serikali ya wananchi wote wa Zanzibar na kamwe hakuna Serikali nyengine, hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuithamini Serikali yao na kuachana na wale wanaoibeza.

Akieleza historia na umuhimu wa Mapinduzi, Rais Dk. Shein alisema kuwa kabla ya kuingia wakoloni wa Kireno, Zanzibar ilikuwa haikutawaliwa na badala yake iliongozwa na viongozi wenyeji wa kijadi wakiwemo Masheha, Maliwali, Madiwani na wengineo.

Aliongeza kuwa kukandamizwa, kunyonywa, kunyanyaswa pamoja na kunyimwa haki kwa Wazanzibari ikiwa ni pamoja na kunyimwa uhuru kutokana na ushindi wa kura za ASP kila pale uchaguzi unapofanyika ndiko kulikopelekea kufanyika kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kumaliza ujenzi wa Barabara, kuanzia eneo la Fuoni Polisi hadi Tunguu, na kubainisha kuwa utekelezaji huo utafanyika kwa awamu mbili tofauti

“Tunatarajia pia kumalizia barabara itokayo Fuoni Mambo sasa hadi Mwera, na nitafurahi ujenzi huo ukimalizika kabla ya muda wangu wa kuwa madarakani kwisha”, alisema
Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa,Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Radhia Rashid Haroub, akitowa taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi huo,  alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita mbili na upana wa mita saba ina uwezo wa kupitisha gari zenye uzito wa hadi tani 20 pamoja na kuwa na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa mita 1,000.

Alisema ujenzi huo uliogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.4 umetekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Barabara, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020, Ibara ya 88 (c) (i) nukta ya 18.

Alieleza kuwa uzinduzi huo unakwenda sambamba na ule wa barabara iliyoanzia Magogoni Kwamabata hadi Nyarugusu yenye urefu wa kilomita mbili, iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.1.

Aidha, alisema ni muendelezo wa barabara iliyoanzia Nyarugusu hadi Kijitoupele yenye urefu wa kilomita 1.65 iliyogharimu zaidi ya shilingi Bilioni moja.

"Huu ni utekelezaji wa ahadi yako Mheshimiwa Rais iliyotutaka tukamilishe barabara hii kwa kiwango cha lami hadi kufikia Kijitoupele, ambapo ilikamilika mwaka jana', alisema.

Radhia alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo (Nyarugusu - Kijitoupele) kwa kiasi kikubwa  imetatua tatizo la msongamano wa magari katika barabara ya Mwanakwerekwe katika kipindi cha mvua za masika mwaka uliopita, kwa wananchi wanaotumia barabara ya Fuoni kwenda na kurudi mjini.

Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu huyo alisema kwa kipindi cha miaka mitatu sasa Wizara hiyo imefanikiwa kuzifanyia matengenezo barabara kadhaa za ndani kwa kiwango  cha lami Unguja na Pemba.

Alizitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na barabara ya Hospitali ya Chakechake hadi Tibirinzi, barabara ya Misufini - Kwabiziredi, Mitiulaya, mzunguko wa nje wa Mnara wa Mapinduzi Michenzani , barabara ya Kilimani nyumba za maendeleo pamoja na ile ya Kikwajuni juu msikitini.

Alibainisha kuwa barabara zote hizo; pamoja na iliyozinduliwa leo , zina jumla ya urefu wa kilomita 8.35.

Alisema kwa sasa barabara zinazoendelea kufanyiwa matengenezo na Wizara hiyo  ni pamoja na ile ya Msingini Pemba pamoja na barabara ya Soko kongwe kuelekea skuli ya Ngomeni.

"Taratibu za ujenzi wa barabara ya kuelekea skuli ya Kinuni zimeshaanza kwa kutangaza zabuni na tunatarjia kuanza ujenzi huo ndani ya mwezi wa February mwaka huu', alisema.

Nae, Waziri wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir alisema la ujenzi wa barabara za ndani unaendelea kufanyika nchini kote, unalenga kupunguza msongamano wa magari katika barabara kuu.

Aidha, Alisema Wizara hiyo itaendelea kuzishughulikia barabara zote zilizoainishwa ikiwemo ya Mtofaani - Hawaii na ile ya  Fuoni Kibondeni,  ili kurahisisha huduma za usafiri kutoka eneo moja kwenda jengine.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.