Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Aweja Jiwe la Msingi Kituo Cha Afya Magirisi Jimbo la Kijitoupele Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud, wakimsikiliza Daktari Dhamana wa Manispa ya Wilaya ya Magharib i BM, Unguja Dk.Rahma Abdallah Maisara, akitowa maelezo ya picha za Kituo cha Afya cha Magirisi baada ya kuweka Jiwe la Msingi Wilaya ya Magharibi Unguja.wakati wa ziara yake leo.


Na.Abdi Shamnah.Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Shein aliendelea na ziara yake kwa uwekaji wa Jiwe la msingi wa Kituo cha Afya Magirisi, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Akizungumza na wananchi Dk. Shein alisema ujenzi wa kituo hicho cha Afya ni jambo la faraja kwa wananachi wa Jimbo la Kijitoupele, akiwashukuru viongozi wa jimbo hilo kwa uamuzi wao wa busara.

Alisema Ilani za Uchaguzi za Chama cya ASP za mwaka 1961 na 1965 ziliweka bayana azma ya Serikali kutowa  huduma za Afya  bila malipo, jambo ambalo Serikali ya Mapinduzi inaliendeleza.

Alisema Mapinduzi ya 1964 yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya  na elimu, mbali na kuwepo kwa changamoto ya ongezeko la watu hapa nchini.

Akinasibishana  kauli hilo, Dk. Shein alisema kituo hicho kina uwezo wa kutoa huduma kwa wastani wa watu 15,000 pekee hivyo hakitoshelezi mahitaji kwa kuzingatia  wananchi 93,119 wanaotarajiwa kukitumia.

Aliishukuru taasisi ya Direct AID kutoka Kuwait kwa kuunga mkono juhudi za viongozi wa jimbo hilo baada ya kukubali kukamilisha hatua iliypobaki ya ujenzi.

Alisema kituo hicho kitakapokamilika kitaweza kutoa elimu ya kinga ya maradhi mbali mbali na kubainisha wazi upatikanaji wa uhakika wa dawa, kutokana na juhudi za Serikali za kuimarisha bajeti ya Wizara ya Afya katika mwaka wa fedha unaoendelea.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/19 Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 12.7  kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya, hususan katika suala zima la upatikanaji wa dawa, akibainisha huduma zote muhimu ikiwemo uchunguzi wa magonjwa mbali mbali kupatikana bure.

Dk. Shein aliiagiza Wizara ya Afya kujiandaa vyema, ili pale kituo hicho kitakapofunguliwa kiwe na waataalamu na wafanyakazi wanaotosheleza ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Maghribi “B” Kepteni Silima Haji Haji alisema ujenzi wa kituo hicho kwa kiasi kikubwa kutavipungumzia mzigo vituo vyengine , ikiwemo kituo cha Afya Mwera katika kutoa huduma za Afya.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR)Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaaa, Idara maalum na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir alisema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara Afya itajenga uzio pamoja na kukipatia wataalamu an wafanyakazi kituo hicho.

Aliipongeza taasisi ya Direct Aid kwa kuendelea kutoa misaada ya kijamii  kwa wananchi wa Jimbo la Kijitoupele baada ya kufanikisha ujenzi wa kisima.

Nae, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi “B” Ali Abdalla Said alisema ujenzi wa kituio hicho umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 90 ambapo miongoni mwa fedha hizo zinatoka Halmashauri na  mfuko wa Jimbo kupitia Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele.

Alisema ni matarajio ya kituo hicho pale kitakapokamilika kuweza kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wapatao 93,119.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.