Habari za Punde

Asasi za Kiraia Zina Nafasi Kubwa Katika Jamii Kuwaelimisha Wananchi Katika Kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Na Masanja Mabula –Pemba….8/3/2019.
MWAKILISHI  wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa –UNDP-Zanzibar  Rukiya Wadoud amesema asasi  za kiraia zinanafasi kubwa katika kuwaelimisha na kuwashajihisha wananchi kushiriki katika kutelekeza malengo ya maendeleo endelevu. 
 Akizungumza na viongozi wa shehia, dini na watu mashuhuri wa Wilaya ya Micheweni , Rukiya Wadoud amesema ili malengo hayo yaweze kufanikiwa ,lazima kuwepo na ushirikiano wa viongozi kutoka asasi mbali mbali.
Amesema kuwa iwapo asasi za kiraia zitatumia vyema nafasi yake, uwelewa juu ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu utafikiwa kwa ufanisi.
“Viongozi wa dini wanaouwezo wa kuufikisha ujumbe kwa jamii kwa wakati muafaka, kutokana na nafasi waliyonayo katika jamii”alisema.
Kwa upande wao viongozi wa dini akiwemo Mohammed Nassor Khamis na John Shimba Shija wameahidi kuifikishia jamii elimu waliyoipata ili kuona wanashiriki kikamilifu katika kutekeleza malengo hayo.
Mohammed amesema kwamba mbali na kutumia nyumba za ibada pia atatumia sehemu za mkusa nyiko wa watu kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii.
“Nitatumia vyuo vya madrasa ya Quran kuufikisha ujumbe , pamoja na sehemu za mikusanyiko ya watu ikiwemo kwenye vijiwe vya kahawa”alileza.
Aidha John Simba Shija Mwenyekiti wa Parokia ya Wete , Kanisa Katoliki ameishukuru ANGOZA, kupitia Tume ya Mipango Zanzibar kwa kuona umuhimu wa taasisi za dini kupewa elimu hiyo.
“Sisi wakristo tunakawaida ya kukutana kwenye jumuiya, na nafasi hii tutaitumia kufikisha ujembe kwa waumini wetu”alifahamisha.
 Mapema akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Mtadao wa Asasi za Kiraia Zanzibar –ANGOZA- , Asha Aboud Mzee amewataka viongozi hao  kutumia nafasi kuihamasisha jamii kushiriki kutelekeza malengo ya maendeleo endelevu.
Asha amesema mtandao wa asasi za kiraia –ANGOZA- umeona iko haja ya kukutana na viongozi wa dini na asasi za kiraia lengo ni kuwapa taaluma ili waifanye jamii kushiriki kutekeleza malengo hayo.
“Tumieni nafasi zenu kuwaelimisha wananchi na kuwashajihisha kushiriki kutekeleza malengo hayo”alisisitiza.
Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na mtandao wa asazi za kiraia, na kuratibiwa na Tume ya Mipango Zanzibar kwa ufadhili wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa –UNDP.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.