Habari za Punde

Kamati inayoandaa tamasha la vyakula vya asili yashauriwa kupanua wigo

 Meneja wa Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Haji Hamad Fundi akitoa ripoti ya utafiti uliofanywa katika Tamasha la vyakula vya asili Makunduchi na kuhitimisha Mradi wa mwaka mmoja wa kuwajengea uwezo wananchi kujikinga na maradhi hayo.
 Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Meneja wa Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Haji Hamad Fundi (hayupo pichani) alipokuwa akiwasilisha ripoti ya utafiti wa maradhi hayo uliofanywa wakati wa Tamasha la vyakula vya asili Makunduchi.
 Bi. Sada Ali Mohd kutoka Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza akiwashukuru wananchi wa Makunduchi wakati wa kutolewa ripoti ya utafiti wa maradhi hayo katika Mkutano uliofanyika Skuli ya Makunduchi.
Picha na Ramadhani Ali Maelezo Zanzibar

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar                             
Meneja wa Jumuiya ya Muungano wa Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Haji Hamad Fundi ameishauri Kamati inayoandaa Tamasha la vyakula vya Asili linalofanyika Kijiji cha Makunduchi kila mwaka, kupanua wigo na kulifanya la Wilaya na hatimae Zanzibar nzima.
Amesema vyakula vya asili, vilivyokuwa vikitumiwa na wazee wa zamani, ni kinga kubwa ya kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza kwani havina kemikali ambazo ni miongoni mwa vichocheo vya maradhi hayo.
Meneja Haji alieleza hayo katika Skuli ya Makunduchi alipokuwa akitoa ripoti ya utafiti wa maradhi yasiyoambukiza uliofanywa wakati wa Tamashala la vyakula vya Asili lililofanyika mwezi Ogasti mwaka jana katika kijiji hicho.
Alisema dhana iliyojengeka kuwa maradhi yasiyoambukiza yanawapata  zaidi watu wenye kipato cha juu hivi sasa haipo kutokana na wananchi kubadili utaratibu wa maisha na kupenda zaidi kutumia vyakula vya mafuta.
Aliwaeleza wananchi wa Makunduchi kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kupitia Mradi maalumu wa kuwajengea uwezo wanajamii katika kujikinga na kudhibiti maradhi yasiyoambukiza imebainika kuwa wapo wananchi wanayo maradhi ya kisukari na sindikizo la damu katika kijiji hicho.
Aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao kila baada ya kipindi kujua afya zao ili waweze kupatiwa ushauri mapema na kufanya mazoezi kwa vile ni moja ya tiba ya maradhi hayo.
Aidha aliwashauri wananchi wanaopatikana na maradhi yasiyoambukiza kutumia dawa wanazopewa na madaktari kwa ukamilifu kwani hakuna njia mbadala ya kutibu maradhi hayo.
Wakieleza kufaidika na Mradi huo, Mzee Ali Hassan na Maryam Haji Manzi walisema wananchi wamepata uelewa mkubwa juu ya maradhi yasiyoambukiza ikiwemo kujuwa sababu zake, njia za kujikinga na athari zinazoweza kumpata mgonjwa maradhi hayo.
Wameahidi watafanya juhudi ya kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi wenzao kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza kwa kutilia mkazo kutumia vyakula vya asili ambavyo vinapatikana muda wote  katika kijiji cha Makunduchi.
Hata hivyo wameishauri Jumuiya ya Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar utakapotokea Mradi mwengine wa kutoa elimu ya maradhi hayo waupeleke ili kuwanufaisha watu wengi zaidi .
Kutolewa kwa ripoti ya utafiti wa maradhi yasiyoambukiza uliofanywa wakati wa Tamasha la vyakula vya asili Makunduchi ni kuhitimisha Mradi wa mwaka mmoja wa kuwajengea uwezo wananchi katika kujikinga na kudhibiti maradhi yasiyoambukiza uliokuwa maalum kwa kijiji cha Makunduchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.