Habari za Punde

Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi Kukamilika na Kuadhimishwa Kesho Zanzibar.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Ali Mohamed Shein kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo kwa upande wa Zanzibar maadhimisho hayo yatafanyika Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika katika eneo la Tunguu,Wilaya ya Kati Unguja ambapo baadae Rais atawahutubia wananchi katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein uliopo katika Kampasi ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), baada ya kupokea maandamano ya wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi.

Aidha, salamu mbali mbali zitatolewa zikiwemo kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), salamu za Waziri, risala ya wafanyakazi, Rais atatoa zawadi kwa wafanyakazi bora na  hatimae kuwahutubia wafanyakazi.

Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo inasema “Kuimarika kwa Uchumi wa Taifa, kuendane na Kuongezeka kwa Maslahi ya Wafanyakazi”.

Kila ifikapo Mei Mosi ya Kila mwaka, Zanzibar huungana na nchi nyengine duniani katika kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani ambapo hapo mwaka jana maadhimisho hayo yalifanyika huko Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Katika uongozi wa Rais Dk. Shein wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba aliielekeza Wizara yenye dhamana ya masuala ya kazi na Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (ZATUC) kuwa maadhimisho ya Mei Mosi yafanyike kwa utaratibu wa mzunguko ili kila Mkoa wa Zanzibar upate fursa hiyo.

Katika hotuba zake mbali mbali anazozitoa Rais Dk. Shein amekuwa akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na utaratibu wake wa kuzilinda haki za wafanyakazi na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi hatua kwa hatua.Katika hotuba yake ya Mei Mosi mwaka jana, Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba itaendelea kuhakikisha kwamba maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya umma na binafsi yanazidi kuimarika siku hadi siku kadri hali ya uchumi wa Zanzibar itakavyoruhusu.

Aliongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona kuwa maslahi ya kila mwananchi wa Zanzibar katika sekta yoyote ile anayoifanyia kazi yanaimarika bila ya kujali aina ya muajiri. 

Katika hotuba ya kuzindua Baraza la Nane la Wawakilishi aliyoitoa tarehe 11 Novemba mwaka 2010 Dk. Shein alieleza bayana mtazamo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kuhusu wafanyakazi na kusema “Rasilimali moja kubwa ya nchi ni wafanyakazi ambapo ndio msingi wa kujenga uchumi na maendeleo yote ya nchi”.

Aidha, katika kutilia mkazo suala la umuhimu wa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi alisema kuwa “Maslahi bora ya wafanyakazi popote ni ajenda yetu na tutahakikisha mashirikiano na chombo chao ‘Shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi’ na kukuza mahusiano mema”.

Kama inavyofahamika kuwa wafanyakazi ni muhimu katika maendeleo ya Taifa lolote lile kwani ni rasilimali inayotegemewa katika kuzalisha mali na kunyanyua uchumi wa nchi.

Kwa kutambua hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbali mbali kujenga mazingira mazuri kwa wafanyakazi ili waweze kuzalisha zaidi na kuongeza pato la Taifa.

Siku hii ya Mei Mosi inatokana na historia ya maandamano yaliyotokea Chicago nchini Marekani mnamo mwaka 1886 ambapo zaidi ya wafanyakazi 300,000 waliandamana wakidai haki zao za msingi.

Jumuiya za Kitaifa zilipendekeza kwamba siku ya tarehe 01 Mei ya kila mwaka iwe ni siku ya mapumziko kwa ajili ya kuwakumbuka wafanyakazi walioumia na waliofariki zama hizo na Tanzania inaungana na Jumuiya hizo kufanya siku hiyo kuwa ni siku ya kufanya maadhimisho hayo pamoja na kuwa ni siku ya mapumziko.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.