Habari za Punde

Maandalizi ya Siku ya Wauguzi Duniani Kukamilika

 Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi Zanzibar Prof. Amina Abdulkadir Ali akizungumza na wandishi wa Habari kuhusu siku ya Wakunga Duniani, mazungumzo yaliyofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.


Na Ramadhani Ali - Maelezo Zanzibar                                   03.05.2019
Upungufu wa Wafanyakazi na vitendea kazi katika Kada ya Ukunga na Uuguzi unazorotesha ufanisi wa kazi katika Hospitali na vituo vingi vya Afya Zanzibar na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi wanaofika kupata huduma.
Katibu wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Omar Abdalla Ali alieleza hayo katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Hospitali ya Mnazimmoja kuhusu maadhimisho ya siku ya Wuguzi Duniani ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe tano mwezi wa tano kila mwaka.
Omar alisema tathmini iliyofanywa hivi karibuni inaonyesha upungufu wa Wakunga na Wauguzi vijijini ni asilimia 40 na hali hiyo inaweza kuongeza katika kipindi cha miaka mitano ijayo kutokana na kuongezeka vituo vya afya na baadhi ya vituo kupandishwa daraja na kuruhusiwa kutoa huduma ya mama na mtoto.
Katika kupunguza tatizo hilo, Katibu wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar aliishauri Serikali kuwapa ajira wahitimu wa kada hizo mbili ambao hivi sasa wapo wengi mitaani wanasubiri ajira na kuongeza vitendea kazi kwenye vituo vya afya.
Alitaja changamoto nyengine inayoikabili kada ya Uuguzi na Ukunga ni wafanyakazi wa kada hiyo kupangwa katika daraja la usaidizi na Tume ya Utumishi Serikalini ambalo hawastahiki kuwemo kwa mujibu wa taaluma waliyosomea.
Omar alisema pamoja na changamoto hizo, Wakunga na Wauguzi wanaendelea kufanyakazi kwa juhudi na uzalendo mkubwa na wameweza kupunguza idadi ya vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Aliweka wazi kuwa lengo la wafanyakazi wa kada hiyo sio kupunguza idadi ya vifo vya mama na watoto tu bali ni kutaka kuhakikisha hakuna mama mjamzito anaepoteza maisha kutokana na sababu ya uzazi.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi Zanzibar Bi. Amina Abdukadir alisema lengo la kuwa na siku maalumu ya Wakunga na Wauguzi Duniani ni kuwaunganisha pamoja na kuangalia changamoto zinazokabili kada hiyo na kuzitafutia ufumbuzi kwani majukumu yao yanafanana duniani kote.
Alisema kada ya Uuguzi na Ukunga ni miongoni mwa kada muhimu zinazopaswa kupewa heshma kubwa kama zilivyo kada nyengine za kitaalamu na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kuwabeza wafanyakazi wa kada hiyo..
Alisema vyuo vinavyotoa taaluma hizo vimeamua kuimarisha mitaala na kufundisha kada zote mbili kwa pamoja ili kuwapa uelewa mkubwa zaidi wahitimu ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa ufanisi zaidi.
Mrajisi wa Baraza la Wauguzi Zanzibar Vuai Kombo Haji alisema Baraza litaendelea kutoa leseni kwa wahitimu kuanzia stashahada na kuendelea waliosoma katika vyuo vilivyosajiliwa na vinavyotambulika ili kuhakikisha wanaofanya kazi ya Ukunga na Uuguzi wanaelimu inayokubali.
Alisema Baraza limetoa leseni kwa Vyuo vinne hadi sasa kufundisha fani ya Ukunga na Uuguzi Zanzibar vikiwemo vitatu vya binafsi na kimoja cha Serikali na kipo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar.
Katibu wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Omar Abdalla Ali akieleza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa kada hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi Zanzibar Prof. Amina Abdulkadir Ali akizungumza na wandishi wa Habari kuhusu siku ya Wakunga Duniani, mazungumzo yaliyofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Muuguzi dhamana wa Hospitali ya Mnazimmoja Asha Mkamba Khamis akisaidia kutoa ufafanuzi wa masuala yaliyoulizwa na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.