Habari za Punde

Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi Waliopata Maafa Kijiji Cha Nungwi Ukiendelea.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akifanya ziara ya kukagua ujenzi wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa katika Kijiji cha Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja.Wa kwanza kulia ni Naibu Mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Muhidin Ali Muhidin.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akiiagiza Kampuniinayojenga Nyumba za Wananchi waliokabiliwa na Maafa Nungwi kuhakikisha kwamba majengo hayo yanakuwa katika kiwango kinachokubalika.
Wahandisi wa Ujenzi wakiendelea na harakati za Ujenzi kwa ajili ya Nyumba za Wananchi waliokabiliwa na Maafa zinazojengwa katika Kijiji cha Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja.
Muonekanao wa baadhi ya majengo yatakayokabidhiwa baadhi ya Wananchi waliokabiliwa na Maafa yanayojengwa katika Kijiji cha Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja.  

Mhandisi wa kampuni ya Nagaya Construction Limited inayojenga nyumba za wananchi waliokabiliwa na Maafa huko Nungwi Bwana Ernest Mbangula akimueleza Katibu Mkuu Shaaban miongoni mwa changamoto zinaowakabili katika kazi yao.
Picha na Kassim Salum Abdi– OMPR.
Na. Rashida Abdi.OMPR.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Nd. Shaaban Seif Mohammed ameitaka kampuni ya Nagaya Constructions Limited iliyopewa dhamana ya ujenzi wa nyumba maalum zinazosimamiwa na kamisheni ya Maafa kuweka mipaka ili kulihifadhi eneo hilo na uvamizi wa Watu  walio jirani na  maeneo hilo.
Alisema ipo haja ya kuweka alama { bikoni } mapema au kulizungushia uzio eneo hilo kwa lengo la kuepusha migogoro isiokuwa ya lazima baina ya serikali na wananchi wake.
Katibu Mkuu Shaaban alieleza hayo  huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba zinazosimamiwa na Kamisheni ya Maafa kufuatia ufadhili wa Jumuiya ya Red  Cresent iliotiliana Saini na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nd. Shaaban aliiomba kampuni iliopewa dhamana ya ujenzi huo kujitahidi kumalizia nyumba hizo kwa muda uliopangwa na zikiwa katika ubora na kiwango ili kuepusha usumbufu kwa watu watakaoyatumia majengo hayo mara ya kukamilika kwake.
Alisema haipendezi wala sio jambo jema kwa kampuni za ujenzi zinazopewa dhamana na serikali kujenga majengo chini ya kiwango hali inayopekelea majengo kuchakaa na kupoteza ubora wake ndani ya kipindi kifupi baada ya kuyakabidhi kwa serikali.   
“ Niseme tu sio jambo jema kwa kampuni kubwa zinazopewa dhamana na kuaminiwa na serikali kufanya ghushi katika kutekeleza majukumu yake” Alisema Katibu Mkuu Shaaban
Pamoja na mambo mengine Nd. Shaaban  ameziomba taasisi zinazohusika na miji mipya   kupeleka huduma muhimu katika eneo hilo kutekeleza wajibu huo akitolea mfano huduma ya maji safi na salama pamoja na miundombinu ya barabra kwani kufanya hivyo kutairahisishia kampuni ya ujenzi kuzikabidhi nyumba hizo zikiwa zimekamika.
NaeMhandisi kutoka kampuni ya Nagaya Construction Limited Bwana Ernest Mbangula Alimueleza Katibu Mkuu Shaaban miongoni mwa changamoto inayowakabili ni upatikanaji wa rasillimali ya mchanga hali inayorejesha nyuma maendeleo ya ujenzi wa nyumba katika kipindi kilichopangwa.
Akitoa ufafanuzi juu ya maendeleo ya ujenzi huo Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Makame Khatib Makame alisema ujenzi katika hatua ya awali unaendelea vizuri na jumla ya nyumba kumi na tano zinatarajiwa kukamilika kama ilivypangwa.
Mkurugenzi Makame alimuomba Mhandisi Ernest anaeshughulikia ujenzi huo kutoa taarifa mapema juu ya mahitaji ya  rasilimali zinazohitajika kama mchanga ili Kamisheni iweze kuomba kibali mapema iwezekanavyo kutoka serikalini.
“Serikali imeweka utaratibu mzuri juu ya upatikanaji wa Rasilimali ya mchanga hivyo Wahandisi  inawapasa mtoe taarifa mapema kabla ya rasilimali hiyo haijamalizika” Alifafanua Mkurugenzi Makame.
Hiyo ni jumla ya muendelezo wa ziara za Katibu Mkuu ambazo zina lenga kukagua utekelezaji wa mipango ya serikali iliopangwa kupitika vikao mbali mbali vya maamuzi ya serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.