Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, katika Mkutano wa Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa kipindi cha mwezi wa Julai 2018 hadi March 2019, uliofanyika Ukumbi wa Ikulu Ndogo Kibweni Zanzibar.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,ameupongeza
uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuonesha
taswira njema katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Ikulu
ndogo Kibweni mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati ulipowasilisha taarifa ya utekelezaji
wa Mpango Kazi wa Ofisi hiyo kwa Kipindi cha Julai 2018 hadi Machi 2019.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuupongeza uongozi huo kwa kutekeleza vyema majukumu yao sambamba na kutekeleza
vizuri taswira ya Ofisi hiyo kwa lengo la kuendelea kuwatumikia wananchi.
Aliongeza kuwa uongozi wa Ofisi hiyo inatakiwa
kuendelea kuwa kioo kwa Ofisi na taasisi nyengine jambo ambalo limekuwa
likitekelezwa vyema na kuweza kupata mafanikio makubwa katika utendaji wa kazi
za kila siku katika Ofisi hiyo ya Rais.
Aidha, Rais Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi
wa Ofisi hiyo kwa utayarishaji na uwasilishaji mzuri wa Mpango Kazi wa Ofisi
hiyo.
Rais Dk. Shein pia, aliupongeza uongozi wa Ofisi
hiyo chini ya Waziri wake Issa Haji Ussi Gavu kwa kuwasilisha vyema Bajeti ya
mwaka wa fedha ya Wizara hiyo kwa mwaka 2019-2020 katika Baraza la Wawakilishi
na kuweza kupita kwa wakati.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimpongeza Katibu
Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na
uongozi wake wote wa Baraza la Mapinduzi kwa
kutekeleza vyema majukumu yao na kuendelea kumsaidia vizuri
Pia, Rais Dk. Shein aliwapongeza Washauri wake
pamoja na Wasaidizi wake wote kwa kuendelea kumshauri na kumsaidia katika
kutekeleza vyema majukumu yake ya kila siku ya kuwatumikia wananchi.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji ya kuzifanyia ukarabati barabara zote zilizoharibika kutokana na
athari za mvua za masika zinazoendelea hivi sasa Unguja na Pemba.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza azma ya Serikali
kupitia Wizara hiyo ya kuendelea na ujenzi wa barabara zote inazozijenga kwa
upande wa Unguja na Pemba sambamba na kuendeleza mradi wa Huduma za Miji (ZUSP)
na ujenzi wa barabara ya Mwanakwerekwe na barabara na daraja katika eneo la
Kibondemzungu.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwapongeza watendaji wenzake wa Ofisi
hiyo kwa kuwasilisha vyema Mpango Kazi huo huku akiusisitiza uongozi wa Ofisi
hiyo kuendelea kuijenga vizuri taswira nzuri ya Rais.
Katika maelezo yake, Dk. Mzee alisisitiza haja ya
kuendeleza mashirikiano kwa viongozi na watendaji wote wa Ofisi hiyo huku
wakitambua kwamba wanabeba taswira ya Rais.
Aidha, alitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa
miongozo yake anayoitoa kwa Ofisi hiyo pamoja na nyenginezo zikiwemo Wizara
zote za Serikali na kuahidi kuendelea kumsaidia na kumuunga mkono.
Nao Washauri wa Rais walimpongeza Rais Dk. Shein
kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar sambamba na
utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Mapema, Waziri wa Ofisi hiyo, Issa Haji Ussi Gavu alieleza
muhtasari wa Mpango Kazi wa Ofisi hiyoalisema kuwa uwelewa wa wananchi juu ya
shughuli zinazotekelezwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yameongezeka kupitia utoaji
taarifa kwa njia za kisasa za mawasiliano zikiwemo mitandao ya kijamii sambamba
na kupitia sinema mbali mbali Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa Zanzibar imeendelea kushiriki katika mikutano
ya kikaanda kikamilifu ambapo imekuja na tija kwa Zanzibar katika kuleta
maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri Gavu alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imekuwa na mahusiano mema na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kupitia
makongamano yanayofanyika kila mwaka ambapo pia, Ofisi hiyo imeshiriki katika
Makongamano ya Wanadiaspora yakiwemo ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani na
Sweden.
Pamoja na hayo, Waziri Gavu alieleza kuwa Ofisi hiyo
imeandaa Sera ya Mawasiliano na Habari ya Ofisi ambayo inatarajiwa kuimarisha
utaratibu wa Mawasiliano na utoaji wa taarifa ndani na nje ya Ofisi.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment