Habari za Punde


WANANCHI wa Mkanyageni wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuwafutarisha wazee, ndugu na jamaa zake hali ambayo inaonesha jinsi anavyowajali na kuwathamini.

Akitoa pongezi na shukurani hizo kwa niaba ya wananchi, ndugu, jamaa na wazee wa Mkanyageni, mzee Suleiman Amour alieleza kuwa utamaduni huo aliouanzisha Rais Dk. Shein tokea miaka ya tisini unaonesha wazi jinsi anavyowajali na jinsi anavyotekeleza fadhila za mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mzee Suleiman aliyasema hayo, mara baada ya futari maalum aliyoiandaa Rais Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkanyageni ukiwa ni utamaduni anaouendeleza hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya  Sekondari ya Mohamed Juma Pindua iliyopo Mkanyageni, Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Mzee Suleiman alitumia fursa hiyo kwa niaba ya wananchi wa Mganyageni kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, baraka na uongozi wenye busara na hekima Rais Dk. Shein ili Zanzibar izidi kupata neema na maendeleo zaidi.

Alieleza kuwa wananchi wa Mkanyageni wanaridhika na uongozi wake na kuahidi kuendelea kumuuunga mkono pamoja na Serikali anayoiongoza huku wakisisitiza kuwa wao hawana cha kumlipa ila ni kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu, afya na kumzidishia hekima katika uongozi wake.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliwasisitiza wananchi hao wa Mkanyageni kuendeleza umoja na mshikamano wao ili maendeleo zaidi yazidi kupatikana.

Aidha, Rais Dk. Shein aliwataka Wazanzibari wote pamoja na wananchi wa Tanzania kwa jumla kuendeleza upendo na mshikamano walionao hasa ikizingatiwa kuwa wao wote ni wamoja.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi hao kuyatumia vyema mafunzo ya Ramadhani na kuwasisitiza kuzidisha ibada pamoja na kusoma sana Qur-an kwani mwezi huu ndio mwezi ulioshuka kitabu hicho kitukufu.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Hemed Suleiman alisema kuwa Dk.Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa Mkanyageni kuendelea kufuata miongozo ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kufanya bidii ya kusoma sana Qur-an.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya Rais, Mkuu wa Mkoa huo Hemed Suleiman alieleza kuwa wananchi na waumini wote wa Dini ya Kiislamu wanapaswa kufanya vitendo vinavyompwekesha Mwenyezi Mungu na kukatazana mabaya ili wazidi kupata baraka na neema za mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Alisistiza kuwa maendeleo makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar yametokana na amani, utulivu na mshikamano uliopo hivyo wanapaswa kuiendeleza hali hiyo iliwazidi kuishi salama kwani bila ya amani hakuna maendeleo.

Aidha, aliwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vya unyanyasaji wa wanawake na watoto kwani vitendo hivyo havileti taswira nzuri katika jamii ya Kizanzibari na pia havimridhishi Mwenyezi Mungu.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kusini Pemba alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa  maendeleo makubwa yaliopatikana chini ya uongozi wa wake Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa maendeleo yaliopatikana ikiwa ni pamoja na uimarishwaji wa miradi ya maendeleo kisiwani humo zikiwemo barabara yanastahiki pongezi kwa Rais Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote waliohudhuria katika futari hiyo aliyowaandalia na kupongeza jinsi walivyoonesha upendo mkubwa kwake kwa kukubali muwaliko wake huo.

Wakati huohuo, nae Mama Mwanamwema Shein kwa upande wake aliungana pamoja na wazee, ndugu na jamaa wote wa Mkanyageni katika futari hiyo maalum aliyoianda  Dk. Shein.

Rais Dk. Shein amemaliza ziara yake hiyo ya kuwafutarisha wananchi kisiwani Pemba na leo anatarajiwa kurejea Unguja.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.