Habari za Punde

DIRISHA LA MAOMBI YA MKOPO KWA NJIA YA MTANDAO KUFUNGULIWA JULAI 1, 2019


Tunapenda kuwafahamisha waombaji mikopo ya elimu ya 
juu kwa mwaka wa masomo 2019/2020 kuwa dirisha la 
kuomba mkopo kwa njia ya mtandao litafunguliwa 
rasmi Jumatatu, Julai 1, 2019 na kufungwa Alhamisi, 
Agosti 15, 2019. Maombi yote yatafanywa kupitia mtandao 
utakaopatikana kupitia www.heslb.go.tz.
Kati ya leo (Jumanne, Juni 25) na Julai 1, 2019 wakati 
dirisha litakapofunguliwa, wanafunzi wanashauriwa 
kuhakikisha wanakamilisha nyaraka muhimu zinazotajwa 
katika‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa 
2019/2020’ unaopatikana katika tovuti ya HESLB 
Nyaraka hizo na maelezo mengine ya ufafanuzi pia 
yanapatikana katika kitabu kidogo cha ‘Maswali na 
Majibu 26’ kuhusu uombaji mkopo kinachopatikana katika tovuti hiyohiyo.
 Kwa ajili ya kumbukumbu, nyaraka muhimu ni pamoja na:
i.  Nakala ya cheti cha kuzaliwa cha mwombaji wa 
mkopo iliyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi 
na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa 
Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA);
ii.  Nakala ya cheti cha kifo cha mzazi wa mwombaji mkopo iliyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi 
na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa 
Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA);
iii. Barua ya Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) au Mganga wa 
Hospitali ya Halmashauri ya Mji, Wilaya, Manispaa 
au Jiji inayothibitisha ulemavu wa mwombaji 
mkopo au mzazi wake; na
iv.  Barua kutoka kwa taasisi iliyofadhili masomo ya sekondari au stashahada ya mwombaji mkopo.

Ufafanuzi kwa wanafunzi waliomaliza 
kidato cha sita na stashahada mwaka huu
Baada ya wanafunzi waliomaliza kidato cha sita au 
stashahada (diploma) wamekuwa wakiuliza maswali kadhaa 
kuhusu utaratibu wa ujazaji wa fomu za uombaji mkopo 
wakiwa katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na 
iwapo wanaweza kujaza fomu kabla matokeo ya mitihani 
hayajatoka. 
Ufafanuzi ni kuwa HESLB inawasiliana na Makao Makuu ya 
JKT ili kuweka utaratibu bora kuwawezesha wanafunzi 
wahitaji waliopo katika kambi za JKT kuwasilisha maombi 
kwa njia ya mtandao. 
Aidha, mfumo wa uombaji mikopo kwa njia ya mtandao 
utakaofunguliwa Julai 1 mwaka huu haumlazimishi 
mwombaji kuwa na matokeo ya kidato cha sita. Mwombaji 
atapaswa kuwa na namba ya mtihani wake wa kidato cha nne 
tu.
Wito
Waombaji wa mikopo watarajiwa wanashauriwa kusoma 
mwongozo uliotolewa na kuandaa nyaraka zote muhimu 
zinazohitajika kuthibitisha uhitaji wao kabla ya kuingia 
katika mfumo wa uombaji. Uzoefu unaonesha kuwa 
mwombaji mkopo anaweza kutumia dakika 30 kukamilisha 
maombi yake katika mfumo ikiwa ana nyaraka zote muhimu. 
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mtendaji,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
Dar es salaam
Jumanne, Juni 25, 2019

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.