RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amemuapisha Major Said Ali Juma Shamuhuna kuwa Mkuu wa Kikosi cha Valantia
Zanzibar (KVZ).
Hafla ya kuapishwa kwa Major Shamuhuna, imefanyika
leo Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu
wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd pamoja na Wakuu wa vikosi vya Ulinzi vya SMZ
na SMT.
Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said
Hassan Said, Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na Naibu Kadhi wa Zanzibar Sheikh
Hassan Othman Ngwali.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo
ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub
Mohamed Mahmoud, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri
wa Rais wa Zanzibar, na viongozi wengine wa Serikali pamoja na wanafamilia.
Major Shamuhuna aliteuliwa hivi karibuni mnamo
Juni 13, 2019 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya Kifungu cha 9(1) cha Sheria
ya Kikosi cha Valantia Namba 5 ya mwaka 2004.
Major Said Ali Juma Shamuhuna anachukua
nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Kikosi hicho Lt. Col. Mohamed Mwinjuma Kombo ambaye
amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa kwakwe,
Major Shamuhuna alisema kuwa uteuzi huo alioupata kutoka kwa Rais Dk. Shein unathibitisha
kwa kiasi gani Serikali inavyothamini utendaji wake wa kazi.
Aidha, Major Shamuhuna aliahidi kuwa
atakiongoza kikosi hicho cha Valantia Zanzibar (KVZ) kwa kuzingatia Sheria, kanuni,
taratibu, hekima na busara katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana huku
akisisitiza mashirikiano ya pamoja ndani ya Kikosi hicho.
Sambamba na hayo, Major Shamununa alieleza
kuwa atahakikisha anasimamia nidhamu na utekelezaji bora wa majukumu kwa
viongozi na askari wa kikosi hicho ili kufanikisha majukumu ya kila siku katika
maendeleo ya Jeshi hilo.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment