Habari za Punde

Balozi Seif ayafunga Maonyesho ya 43 ya Biashara Dar

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea Mabanda Wajasiri amali wanaotengeneza Bidhaa za ngozi wa Woiso kwenye  Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Dar es salaam
 Afisa Masoko wa Benki ya Watu wa Zanzibar Mohammed Khamis Ismail akimpatia maelezo Balozi Seif alipotembelea Banda lao kwenye Maonyesho ya 43 ya Biashara Dar es salaam.
  Balozi Seif  akikagua Mabanda ya Akina Maa Wajasiri amali Kutoka Taasisi wa WIPE na kuridhika na bidhaa zinazozalishwa na wajasiri amali hao.
  Balozi Seif  akikagua Mabanda ya Akina Maa Wajasiri amali Kutoka Taasisi wa WIPE na kuridhika na bidhaa zinazozalishwa na wajasiri amali hao.
 Balozi Seif akiangalia bidhaa za vitu vya samani zinazozalishwa na Jeshi la Magereza Tanzania kwenye Maonyesho ya 43 ya Biashara Dar es salaam.
 Balozi Seif akiangalia bidhaa za vitu vya samani zinazozalishwa na Jeshi la Magereza Tanzania kwenye Maonyesho ya 43 ya Biashara Dar es salaam.
 Balozi Seif  akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Taasisi ya Viwango Zanzibar ZBS .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza wakati akiyafunga Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Dar es salaam Tanzania yanayofanyika katika Ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa ndani ya Uwanja wa Mwalimu Julius K. Nyerere.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema katika kuhakikisha mazingira bora ya Biashara yanaimarika Nchini, Serikali itashirikiana kikamilifu na Vijana, Wanawake na Watu wa Makundi maalum ili Sekta ya Biashara iwe na uwezo mkubwa wa kutengeneza Ajira.
Alisema matengenezo hayo ya fursa za ajira yanaweza kusaidia kuondosha au kupunguza kwa kiasi kikubwa umaskini wa kipato, hususan kwa watu wenye mazingira magumu hasa sehemu za Vijiji Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiyafunga Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa hapo katika Ukumbi wa Rashid Mfaume Kawawa ndani ya Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu Julius. K.  Nyerere Jijini Dar es salaam, ingawa  pia Wadau wameomba yaeendelee  na tayari yamekubaliwa hadi Tarehe 13 Julai 2019.
Alisema ushirikiano huo unathibitishwa  na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuandaa Mpango wa kuimarisha mazingira ya Biashara kupitia andiko la Blue Print ambalo utekelezaji wake umeshaanza rasmi kutumika mnamo Tarehe 01 Julai  Mwaka huu wa 2019.
Hata hivyo, Balozi Seif alisema, kabla ya kuanza kwa utaratibu huo Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeshaanza utekelezaji wa Mpango Kazi huo kwa kuondoa Tozo nyingi katika Sekta za Kilimo, Madini na Viwanda.
Alisema hatua zinazochukuliwa za kuendeleza Mazao ya ndani yanayoshughulikiwa na Wakulima wenyewe kupitia Wataalamu wazalendo yamepelekea kuhamasisha Wananchi kujenga tabia ya kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vya hapa Nchini.
Alisema mfumo huo una nia na lengo  la kutumia vyema soko la ndani ambalo ni kubwa lakini wakati huo huo kuongeza ajira kutokana na uzalishaji wa bidhaa hizo ambazo nyingi huzalishwa na Viwanda vidogo vidogo na vile vya kati na kupunguza tatizo la ajira.
Balozi Seif aliwahakikishia Washirika wa Sekta ya Biashara ndani na nje ya Nchi kwamba Serikali daima ipo pamoja nao katika kuhakikisha kwamba Sekta ya Biashara na Viwanda Nchini inakuwa kwa kasi na kuwa kichocheo kikubwa  cha kuchangia ukuaji wa Uchumi, ajira na kupanua wigo wa Kodi Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliushukuru Uongozi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tantrade} kwajitihada za kuziendeleza bidhaa za Viungo, Chumvi, Mwani na Dagaa zinazozalishwa Visiwani Zanzibar kwa kuongeza thamani ya mazao hayo na hivyo kuyawezesha kushindana katika Masoko ya ndani na nje ya Zanzibar.
Balozi Seif  pia aliupongeza Uongozi huo wa Tantrade kwa juhudi unazochukuwa wa kushirikiana na Washirika mbali mbali wa Sekta Binafsi na Umma kwa kusimamia Maonyesho hayo ya Kimataifa yaliyojenga umaarufu nje ya Mipaka ya Tanzania.
Alisema kwa Vile Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tantrade} kwa vile ni Taasisi ya Muungano yenye Ofisi yake Zanzibar, alitoa wito kwa Uongozi wa Taasisi hiyo kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar kutafuta Wabia wa kuwekeza kwa pamoja katika Ujenzi wa Miundombinu ya Uwanja wa Maonyesho Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshalitenga eneo Maalum kwa ajili ya Mradi huo liliopo Fumba nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ili kuwawezesha Wafanyabiashara kutumia jukwa hilo kwa ajili ya kupata masoko ya kudumu ya bidhaa wanazozalisha.
Alifahamisha kwamba SMZ ina mpango wa kuwekeza kwa Ubia katika Ujenzi wa Uwanja wa Kisasa wa Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa kwa lengo la kuonyesho Bidhaa na huduma zinazozalisha Nchini na kuimarisha Sekya ya Biashara kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alielezea matumaini yake kutokana na Maonyesho hayo ya Bishara ya Kimataifa Dar es saam kutoa fursa kubwa ya kujifunza kutoka kwa Washiriki mbali mbali wa Nje kutokana na Taaluma waliyonayo iliyowawezesha kupata mafanikio waliyonayo hususan suala la Teknolojia na Vifungashio vya Bidhaa.
Alisema mafanikio hayo yataongeza chachu kwa wale washirika wa Sekta ya Biashara hasa Wafanyabiashara wadogo wadogo wa ndani ambao bado wapo kwenye  hatua za msingi katika Biashara na Viwanda vyao.
Aliwasihi Washirika hao wa ndani kupitia Mitandao mbali mbali ya Biashara waliyoipata na kujifunza, waitumie ipasavyo katika kuendeleza bidhaa zao wanazozalisha kila siku.
Alieleza kwamba ili zoezi hilo liwe la kudumu, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tantrade}iendelee kuhifadhi kumbukumbu ili wengine nao wapate fursa ya kujifunza  kupitia Taaluma waliyoipata ndani ya Maonyesho hayo.
Alisema Maonyesho ya Mwaka huu yamepata Mafanikio makubwa kutokana na ongezeko la Washiriki, Kampuni za ndani zaidi ya Elfu 3,250 zilishiriki ikilinganishwa na Kampuni Elfu 2,956 zilizoshiriki Mwaka 2018.
Alisema kwa upande wa Kampuni za Nje Mwaka huu walipatikana Washiriki Mia 580 ikilinganishwa na  Washiriki 508 Mwaka uliopita, wakati Nchi zipatazo 35 zilikuwepo kwenye Maonyesho hayo ikilinganishwa na Nchi 33 Mwaka jana.
Alieleza kwamba ongezeko hilo ni ishara ya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es salaam yanaendelea kupata umaarufu  na kuwa Jukwaa linalotegemewa na wazalishaji na Washirika mbali mbali wa Biashara kutoka ndani na Nje ya Nchi, kutangaza na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa na huduma zao.
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya  Mamlaka ya Maendeleo ya Viwanda Tanzania Nd. Ng’wanza  Kamata Soko amewapongeza Washiriki wote kwa uthubutu wao uliopelekea kufanikisha Maonyesho ya Mwaka huu kuwa bora zaidi ikilinganishwa na yale ya Mwaka uliopita.
Nd. Kamata Soko amewahakikishia kuwa Bodi pamoja na Serikali iko pamoja nao katika kuweka mazingira bora na rafiki ya ufanyaji Biashara Nchini ili kuwezesha Sekta ya Biashara na Viwanda kukua, kuvutia Wawekezaji na hatimae kuchangia katika Uchumi wa Taifa.
Alifahamisha kwamba ufanisi wa Maonyesho hayo umetokana na michango ya Wadhamini tofauti akiwataja kuwa ni pamoja na Benki ya Biashara {NBC} MIC Tanzania, Tigo, Barmedas, TBC, Channel Ten Redio na TV, Amimza, Tropical Power LTD na Waja General Enteprises.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania Mh. Innocent Bashungwa alisema Maonyesho hayo yalikuwa na matukio mbali mbali ikiwemo Mikutano ya Kibiashara.
Waziri Innocent alisema Siku Maalum zilitengwa kwa lengo la kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbali mbali ikiwemo siku ya kujadili mapambano dhidi ya Rushwa, Amani na Mazingira, kuendeleza mazao ya Korosho, Kahawa, Chai, Karafuu, pamoja na Pamba.
Alisema mafunzo ya kuwahamasisha Wananchi kujenga tabia ya kupenda  na kutumia bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vya Hapa Nchini yalitolewa na kuwafikia walengwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.