Habari za Punde

Jimbo la Chaani Wakabidhiwa Vifaa Vya Miradi ya Maendeleo

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akikaribishwa katika Mkutano wa Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mh. Nadir Abdulatif  wa ugawaji wa vifaa na misaada ya kuimarisha Maendleo ya Jimbo hilo.
Balozi Seif akikabidhi Mipira ya kusambazia maji safi na salama pamoja na Tangi la kuhifadhia Maji kwa Wananchi wa Wadi zilizomo ndani ya Jimbo la Chaani.
Balozi Seif akimkabidhi mabati ya kuezekea Diwani ya Wadi ya Kinyasini Haji Kidawa kwa ajili ya kuezekea Jnego la Tawi la CCM la Kinyasini.
Balozi Seif akikabidhi mifuko ya saruji kwa Kiongozi wa Shehia ya Pwani Mchangani itakayosaidia kuendeleza Jengo la Soko la Kijiji hicho kilichomo ndani ya Jimbo la Chaani.
Diwani Miza wa Viti Maalum akipokea Seti ya TV kwa ajili ya Maskani ya CCM ya BBC kutoka kwa Balozi Seif iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Chaani katika Mkutano wa Mwakilishi huyo hapo Skuli ya Chaani.
Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mheshimiwa Nadir Abdulatif Ismail akizungumza katika Mkutano aliouandaa wa kugawa vifaa na misaada mbali mbali ya maendeleo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wananchi wa Jimbo la Chaani katika Mkutano wa Mwakilishi wa Jimbo hilo wa kugawa vifaa na misaada tofauti.
Na.Othman Khamis OMPR.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alitahadharisha kwamba tabia ya ubinafsi inayopenda kuendekezwa na Wapambe wa Viongozi ndio chimbuko la migongano inayozaliwa katika baadhi ya Majimbo hapa Nchini.
Alisema wapo Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanakimbiana  katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Majimbo yao kutokana na sintofahamu zinazozaliwa na wapambe wao, makundi ambayo hudumaza maendeleo yanayokusudiwa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa tahadhari hiyo katika Mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mh. Nadir Abdulatif Ismail wa kukabidhi  Vifaa vya Miradi ya maendeleo pamoja na zawadi alizoahidi ikiwa ni muendelezo wa kutekeleza Ilani ya CCM pembezoni mwa Skuli ya Chaani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Wananchi lazima wajibebeshe jukumu la kuwasaidia Viongozi wao hasa Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kuondokana na tabia ya majungu inayoonekana kuwa ugonjwa ndugu katika baadhi ya Majimbo hapa Nchini.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alitanabahisha kwamba wakati umefika kwa Wananchi kutowabebesha majukumu binafsi Viongozi wao ili kuwapa fursa na muda wa kukamilisha ahadi walizowapa wakati wa Kampeni za Uchaguzi.
Alisema hakuna kipengele ndani ya Ilani ya CCM kinachomtaka Mheshimiwa Muwakilishi au Mbunge amtekelezee Mwananchi mambo yake binafsi kama kumjengea Nyumba au hata mahari ya harusi badala yake waachiwe waendeleze na kusimamia miradi ya jamii akatolea mfano Elimu, Huduma za Afya pamoja na Maji safi na salama.
Alieleza kwamba wapo baadhi ya Wananchi humuona Mheshimiwa mkorofi kwa kuwa hakutekelezewa shida yake binafsi na hatimae kuanza kampeni ya kumpikia majungu yanayoleta makundi ndani ya Majimbo.
“ Wananchi wanapaswa kuelewa kwamba misaada binafsi sio lazima katika majukumu ya Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi”. Alisisitiza Balozi Seif.
Hata hivyo Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema Mheshimiwa ye yote anaweza kufanya hivyo kama masuala ya Kibinaadamu yalivyomzunguuka lakini sio wajibu wake kwa mujibu wa Ilani na Sera za Chama.
Balozi Seif alimpongeza Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mh. Nadir Abdulatif Ismail  kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ndani ya Jimbo lake katika kuwaletea Maendeleo Wananchi wake.
Alisema anachokifanya Mheshimiwa Nadir sio fadhila bali ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020 inayokwenda sambamba na ahadi alizowapa Wananchi wake wakati akitaka ridhaa ya kuwatumikia kwenye Uchaguzi uliopita wa Mwaka 2015.
Akizungumzia Watu wengine wan je wanaojitolea kusaidia Wananchi ndani ya Majimbo Balozi Seif alisema sio vibaya hata kidogo, lakini kinachopaswa kuzingatiwa ni uwepo wa mawasiliano baina ya Watu hao na Viongozi wanaohusika na usimamizi wa Majimbo.
Alisema hatua hiyo ya mawasiliano itasaidia kudumisha na kuendeleza Umoja na Mshikamano wa makundi yote chini ya mwamvuli wa Amani na Utulivu inayohamashishwa na viongozi kila mara wakati na mahali popote pale.
Mapema Mwakilishi wa Jimbo la Chaani Mh. Nadir Abdulatif Ismail alisema shughuli hiyo ya utowaji wa vifaa vya kuendeleza Miradi mbali mbali ndani ya Jimbo hilo tayari ni ya 27 tokea apewe dhamana ya kuliongoza Jimbo hilo.
Mheshimiwa Nadir alisema wao wakiwa wasaidizi wa kupeleka Maendeleo Majimboni nyuma ya Serikali Kuu, Wananchi wa Chaani wamekuwa wakishuhudia  Maendeleo makubwa yanayofanywa na Serikali ya CCM Chini ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Mwakilishi huyo wa Jimbo la Chaani aliwahakikishia Wananchi wa Jimbo hilo kwamba kwa yeye ndie aliyepewa jukumu la kuwatumikia atatumia nguvu na uwezo wake wa kuona Jimbo hilo linabadilika Kimaendeleo katika muda mfupi ujao.
Katika Mkutano huyo Mwakilishi wa Jimbo la Chaani alikabidhi Matofali  2,000, Tv Tatu, Printa na Mashine ya Fotokopi, Matangi ya kuhifadhia Maji, Mipira ya kusambazia Maji, Saruji Paketi 50 pamoja na shilingi Laki 850,000/- kwa Skuli ya Chaani.
Vifaa na vitu vyote hivyo alivyovitoa Mheshimiwa Nadir Abdulatif Ismail vinakisiwa kugharimu Shilingi za Kitanzania Milioni 22, Laki Nane na Ishirinini na Sita Elfu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.