Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Atembelea Mashamba Yanayomilikiwa na Serikali Kisiwani Pemba Akiwa Katika Ziara Yake leo.b

Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Kisiwani Pemba Nd. Said Juma Hamad Kushoto akitoa maelezo ya mazingira yaliyopo ya Mashamba ya Serikali Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Baadhi ya Wananchi na Wakulima wa Vijiji vya Finya na Makuwe waliojitokeza kumlaki Balozi Seif  aliyefika katika Vijiji hivyo kukagua Mashamba ya Serikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa maagizo ya utafutwaji wa Mashamba ya Serikali wakati alipofanya ziara ya kuyakagua Mashamba ya Serikali ya Finya na Makuwe Kisiwani Pemba.
Naibu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Shamata Shaame Khamis akitoa ushauri wa namna ya kusafishwa Mashamba ya Serikali kwa kutumia Vikosi vya SMZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea na kukagua Mashamba ya Serikali yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Muonekano wa Shamba la Serikali la Makuwe liliopo Mkoa wa Kaskazini Pemba  ambalo Mwaka 2017 limekodishwa Mikarafuu yake  kwa gharama ya shilingi Milioni 290,000,000/-.(Picha na OMPR)
Na.Othman Khamis. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa maamuzi mara baada ya kukamilisha zoezi la uhakiki wa Mashamba yake yote yaliyomo katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Alisema maamuzi hayo pamoja na mambo mengine yatazingatia pia kuwapa Wananchi ili wayaendeleze kwa kilimo hasa yale yaliyokosa usimamizi na kuyaendeleza kwa muda mrefu na kusababisha uzalishaji mdogo wa mazao pamoja na Karafuu.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiendelea na ziara yake ya Siku Nne Kisiwani Pemba akikagua Mashamba yanayomilikiwa na Serikali yaliyomo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema umefika wakati Mashamba ya Serikali yawe na uwezo kamili wa uzalishaji kama yalivyo ya Watu Binafsi na pale inaposhindikana kukosa huduma za usafishaji ni vyema ukaandaliwa utaratibu na Taasisi zinazohusika kuwapa Wananchi wale wenye nia ya kuyaendeleza kwa Kilimo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuridhia Wizara ya Kilimo , Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar kuandaa utaratibu wa kutoa Ajira kwa Vijana ili yasafishwe Mashamba yote ya Serikali ambayo hukaa muda mrefu na kupoteza Uzalishaji.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mbali ya usafishaji wa Mashamba hayo utakaoongeza Mapato ya Taifa lakini kwa upande mwengine fursa hiyo itatoa ajira kwa Vijana watakaokuwa tayari kufanya kazi hiyo ya Kizalendo ya kuokoa Uchumi wa Taifa.
Aliushauri Uongozi wa Wizara ya Kilimo mbali ya kufanya Uhakikishi utakaoongozwa na Wakuu wa Wilaya wa kuyatambua Mashamba ya Serikali katika Wilaya mbali mbali lakini  wakazingatia kuwahakiki Wananchi waliyojitolea kuyasafisha Baadhi ya Mashamba hayo bila ya kushurutishwa.
Alisema uhakiki huo uwaandalie Wanachi hao njia na namna ya kuandika Maombi na kuyapeleka Serikalini kupitia kwa Masheha na Wilaya zao yatakayotoa utaratibu wa kumilikishwa katika matumizi yake kama ilivyofanywa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume Mara baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Akitoa ushauri wa kunawirishwa kwa Mashamba ya Serikali, Naibu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mh. Shamata Shaame Khamis alisema ni vyema vikatumiwa Vikosi vya SMZ  wakiwemo Watu wa Chuo cha Mafunzo katika usafishaji wa Mashamba hayo.
Mh. Shamata alisema hatua hiyo ya dharura inaweza kusaidia kipindi hichi cha mpito kuelekea mafuno ya Msimu wa Vuli ambao hutegemea kuzalisha mazao mengi haza lile la Uchumi wa Taifa la Karafuu.
Alisema Vikosi cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na mambo mengine ya Ulinzi lakini pia vina utaratibu wa kushiriki kwenye shughuli za Kijamii na Kitaifa pale inapotokeza kuwepo kwa mahitaji hayo.
Mapema Mkuu wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Kisiwani Pemba Nd. Said Juma Hamad alisema yapo Mashamba Sita yanayomilikiwa na Serikali Kisiwani pemba ambayo hayako katika hali ya kuridhisha kutokana na ushughulikiaji mdogo.
Nd. Said alitolea mfano Shamba la Makuwe pekee linalotegemewa na Serikali kwa mapato Makubwa lenye ukubwa wa Ekari 200 likiwa na Wafanyakazi Watano tu wanaolihudumia.
Alisema Shamba hilo lililosheheni zaidi miti ya Mikarafuu na Minazi limefanyiwa usafi Mnamo Mwaka 2016 kukodishwa  kwa zaidi ya Shilingi Milioni 290,000,000/- katika kipindi cha Msimu wa Vuli mnamo Mwaka uliofuatia wa 2017.
Mkuu huyo wa Idara ya Misitu na Mali zisizorejesheka Pemba alifahamisha kwamba Minazi iliyomo ndani ya Shamba la Makuwe nazi zake hutumika kuoteshea Miche kwenye Vitalu vya Wizara ya Kilimo na baadhae kugaiwa kwa Wakulima.
Naye Afisa Mdhamini wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar {ZSTC} Kisiwani Pemba Ndugu Abdullah Ali Ussi alisema Shirika hilo limefurahishwa na utaratibu uliobuniwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuyafuatilia kwa uhakiki na utambuzi Mashamba yake yote.
Nd. Abdullah alisema kutokana na kutoshughulikiwa kwa mashamba ya Serikali ambayo  ndio yenye uwezo wa kuzalisha zao la Karafuu kwa wingi kumesababisha kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo katika Miaka ya karibuni na kufika Tani 8,500 wakati miaka ya nyuma uzalishaji ulifikia hadi Tani 16,000.
Akitoa ufafanuzi wa Mashamba ya Serikali Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Abdallah  Saadala alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba njia pekee ya kuyaokoa Mashamba ya Serikali na kupatikana ajira za Muda kwa Watu watakaosafisha Mashamba hao.
Bibi Maryam alisema  Mashamba Sita yaliyopo Kisiwa cha Pemba yanaweza kuwa katika mazingira bora iwapo Serikali kupitia Taasisi inayosimamia Utumishi wa Umma itaridhia kutoa baraka za upatikanaji wa Vijana watakaoajiriwa kwa muda kufanya kazi hiyo muhimu.
Alisema mfumo huu unaweza kutumika kwa muda pale  inapotokea dharura ya kutaka kusafishwa Mashamba hayo hasa ule wakati unaofuatia baada ya Msimu wa Mvua Kubwa hapa Nchini.
Akiambatana na baadhi ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Watendaji Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata wasaa wa kuyakagua Mashamba ya Serikali yaliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Maliasilini. Mifdugo ya Uvuvi yaliyopo katika Vijiji vya Finya na Makuwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.