Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Azungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais. Mhe Simbachawene.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazigira Mh. George Simbachawene wa Pili kutoka Kushoto akisisitiza jambo wakati alipofika  kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kujitambulisha rasmi.Kulia ya Mh. Simbachawene ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed, Katibu Mkuu Nd. Shaaban Seif na Mkurugenzi wa Uratibu wa Serikali Nd. Khalid Bakar Amran.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazigira Mh. George Simbachawene aliyefika kujitambulisha Rasmi baada ya kushika wadhifa huo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema upo wajibu na jukumu kubwa la kuwaelimishwa Viongozi Wachanga kutambua umuhimu wa dhana halisi  ya uwezo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kuelewa kwa kina dhana ya uwepo wa Muungano huo.
Alisema wapo baadhi ya Viongozi wanaoingia katika madaraka wakiwa bado hawajaelewa Historia ya muda mrefu iliyowaunganisha kidamu Wananchi wa pande mbili za Muungano ambao hatimae ulirasimishwa rasmi Mnamo Tarehe 26 Aprili Mwaka 1964 na kuundwa kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo Ofisini kwake Vuga wakati akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazigira Mh. George Simbachawene aliyefika kujitambulisha baada ya Kuteuliwa Hivi karibuni kushika Wadhifa huo.
Alisema kazi kubwa inayokabili Watanzania kwa wakati huu ni kuendelea kuuimarisha Muungano huo ulioleta faida kubwa Kiuchumi na Ustawi wa Jamii, faida ambayo inaweza kuwa funzo zuri la kuigwa na Mataifa mengine Ulimwenguni.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuihakikishia Waziri Simbachawene kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Ofisi yake katika Kazi kubwa iliyo mbele ya kuona Umoja na Mshikamano uliojengeka kupitia Muungano huo inaimarika na kustawi kwa maslahi ya Wananchi wote.
Balozi Seif  Alimshauri Waziri huyo anayesimamia Muungano na Mazingira ya Muungano wa Tanzania kwamba anapohisi yapo mambo yanayoashiria kukwamba katika kupeleka mbele Masuala ya Muungano asione uzito kuyatolea Taarifa kwa Viongozi wake wakati wowote ule.
Mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazigira Mh. George Simbachawene alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una shabaha Maalum iliyopelekea Waasisi wa Taifa hili kufikia mamuzi ya Kuunganisha Mataifa Mawili yaliyo Huru.
Mh. Simbachawene wakati umefika sasa kwa kizazi Kipya kilichozaliwa ndani ya Karne ya 21 kinapaswa kuelewa dhamira hasa ya Waasisi hao ambao wengi kati yao wamebahatika kusoma Historia ya Muungano ndani ya Vitabu.
Alisema wapo baadhi ya Watu wakiwemo Viongozi wamepitia kujua mfumo wa Utawala katika Madaraka waliyokabidhiwa wakati wanapokuwa kwenye Utumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayesimamia Muungano na Mazigira Mh. George Simbachawene amechukuwa wadhifa huo wa Uwaziri kufuatia Rais wa  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kutengua Uteuzi wa Mh. January Makamba aiyekuwa akishikilia nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.