Habari za Punde

Kamati za Maskuli na Walimu Kusimamia Mwenendo wa Wanafunzi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akiwakabidhi Mabati  kwa Madiwani wa Kata zilizomo ndani ya Jimbo la Kishapu iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Chambi kukamilishaujenzi wa Miradi yao waliyoianzisha.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema maandalizi ya ufinyazi wa Watoto kuelekea katika maadili mema ndani ya mfumo wa  Kielimu na Heshima ya Utamaduni yanategemewa zaidi ushirikiano wa kina kati ya Wazazi na Walimu.
Alisema Walimu pamoja na kamati zinazoundwa za Uongozi wa Maskuli  kusimamia mwenendo wa Wanafunzi kamwe hazitakuwa na uwezo kamili wa kuwachunga Watoto Maskulini.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo kwenye ufunguzi wa Jengo Jipya la Skuli ya Maandalizi ya Kata ya Somagedi Jimbo la Kishapu wakati akizungumza na Wananchi wa Jimbo hilo mwishoni mwa ziara yake ya Siku Tano kukagua  Miradi ya Maendeleo pamoja na kuangalia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkoani Shinyanga akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama.
Alisema katika muelekeo mwema wa Maadili ya Mwanaadamu utotoni anahitajika kuandaliwa vyema katika ngazi ya msingi ili aingiapo Sekondari iwe rahisi kujinyooshea njia ya Chuo Kikuu na baadae kuwa  na dhima ya kutumikia Taifa lake katika misingi inayokubalika Kitaaluma na Maadili.
Balozi Seif  aliwapongeza Viongozi wa Majimbo na Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kuwatumikia Wananchi wao hasa suala zima la uimarishaji wa Sekta ya Elimu inayotoa fursa ya Kuwafinyanga Vijana kuwa Watumishi waliobobea wa hapo baadae.
Hata hivyo Balozi Seif  aliendelea kukumbusha kwamba Chama katika ngazi ya Taifa hakitasita kumuweka pembeni Kiongozi ye yote hasa yule wa Jimbo aliyechaguliwa na Wananchi lakini anashindwa kuwatumikia kwa kujiweka mbali nao bila ya kuelewa matatizo na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru Wananchi, Wazazi na Walimu wa Kata ya Somagedi Jimboni Kishapu kwa wazo lao lililopelekea kuanzisha mradi huo wa Skuli ambao utakuwa Mkombozi kwa Wanafunzi pamoja na Vizazi vyao hapo vya baadae.
Alisema kitendo hicho ni Ukombozi mkubwa kwa Watoto wao Wadogo ambacho kitawasaidia kuepuka usumbufu wa kufuata Elimu katika masafa marefu ya Vijiji jirani na eneo hilo.
Akigusia Kilimo cha Pamba na Tumbaku Mkoani Shinyanga baada ya kupokea changamoto ya soko la mazao hayo kutoka kwa Wakulima Balozi Seif  aliwaeleza Wananchi hao kwamba ameshawasiliana na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa kwa njia ya simu akiwa Mkoani humo na tayari Serikali Kuu  imesharidhia kutoa kibali cha ununuzi wa Mazao hayo kutoka  kwa Makampuni.
Alisema utaratibu wa ununuzi wa mazao hayo ambao tayari umeshaandaliwa na Uongozi wa Serikali ya Mkoa huo kwa kuvihusisha Vyama vya Ushirika utawawezesha Wakulima hao kuuza Bidhaa zao zinazotokana na vilimo hivyo kwa Makampuni yatayopata Mikopo ya Fedha kupitia Mabenki mbali mbali.
Balozi Seif  akiwashukuru Wakulima hao kwa ustahamilivu waliouchukuwa alisema uamuzi huo wa Serikali utaleta faraja kwao na kuweza kuongeza mapato ili kujikimu kimaisha lakini pia utawasaidia kupata nguvu za kujiandaa na ukulima wa msimu ujao unaokaribia kuanza mwezi ujao.
Wakiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika kipindi cha Miaka Minne, Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh. Suleiman Masoud Chambi na yule wa Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Aza Hilal Hamad walisema yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Ustawi wa Jamii tokea kuanza kwa Utekelezaji huo Mnamo Mwaka 2015
Wabunge hao walisema huduma za Afya zimeimarika mara dufu kuokana na kuongezeka kwa miundombinu ya ujenzi wa Vituo vya Afya pamoja na Zahanati katika kata mbali mbali zilizomo kwenye Majimbo ya Mkoa wa Shinyanga unaoongoza kwa maendeleo ikilinganishwa na Mikoa mengine ya Ukanda wa Ziwa.
Walisema katika kuunga Mkono nguvu za Wananchi wamelazimika kuzidisha uwezeshaji kwa kusaidia Saruji na Mabati yatakayoongeza chachu ya  kukamilishwa kwa Majengo tofauti ya Maendeleo kwenye Kata hizo.
Walieleza kwamba Vikundi vya wajasiri Amali ikiwemo waendesha Boda Boda na Mama Ntilie vimewezeshwa kwa kupatiwa Mikopo ya Piki piki 26 pamoja na kujengewa Jengo lao la Soko la Mama Shery.
Hata hivyo Wabunge hao walisema zipo changamoto zinazokwamisha kasi ya Maendeleo ya Wananchi wa Majimbo yao wakizitaja baadhi yao kuwa ni pamoja na ufinyu wa upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama katika baadhi ya Kata, na Uongozi wa Jimbo umelazimika kufanya tathmini na michoro katika kata zote za Jimbo la Kishapu.
Wamesema wamelazimika kufanya kazi hiyo  ili kujiweka tayari ya huduma hiyo itakapowadia kwa vile bomba Kuu la Maji kutoka Ziwa Victoria limeshapitishwa katika maeneo hayo na ije kuwa rahisi kusamabaza huduma hiyo mara moja.
Akitoa salamu za Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Bibi Nyabaganga Tataba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo alisema Wana Shinyanga wana haki ya kuishukuru Serikali Kuu kwa hatua iliyochukuwa ya kusaidia nguvu za Wananchi katika Uimarishaji wa Sekta ya Elimu.
Bibi Nyabaganga alisema Mkoa huo umebahatika kuwa na Skuli za Sekondari Kila Kata zikiwa na  nafasi ya kutosha kuliko mahitaji halisi  inayowapa fursa pana Wananfunzi wa Kata hizo kusoma katika mazingira bora na utulivu mkubwa.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akiwa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi alikagua  maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Chama hicho Wilaya ya Kishapu.
Ofisi hiyo iliyoanza kujengwa mnamo Mwaka 2016  itakapokamilika mbali ya kutoa huduma za Kiofisi  ikiwa na Vyumba 16  lakini pia imetengewa sehemu nyengine maalum kwa mahitaji ya Uwekezaji Vitega Uchumi vitakavyoiongezea Mapato Wilaya hiyo.
Balozi Seif  katika kuunga mkono jitihada za Wana CCM hao za kujijengea Jengo Jipya na la Kisasa badala ya lile la zamani lililokuwepo tokea Miaka ya 1964 na kuchakaa ameahidi kuchangia shilingi Milioni 3,000,000/- kuwaongezea nguvu Wanachama hao.
Akionyesha kuridhika na hatua za ujenzi huo Balozi Seif alisema ujenzi wa Jengo hilo kubwa ni muendelezo wa Falsafa ya Chama cha Mapinduzi ya kuwa na Ofisi na Majengo yake yenye hadhi inayofanana na Chama chenyewe.
Ukitoa Taarifa fupi ya Ujenzi wa Jengo hilo Uongozi wa CCM Wilaya ya Kishapu ulimueleza Balozi Seif kwamba jitihada kubwa za Mbunge wa Kishapu Mheshimiwa Suleiman Masoud Chambi ndizo zilizofanikisha kufikia hatua hiyo ya uwezekaji.
Walisema kwa sasa Ujenzi huo unakadiriwa kugharimu shilingi Milioni 55.6 wakati mahitaji halisi kwa ajili ya ukamilishaji wa Jengo zima yanakisiwa kufikia shilingi Milioni 80,000,000/-.
Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akilikagua Jengo Jipya la Ofisi ya CCM Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga linaloendelea kujengwa.
Balozi Seif akielekea kwenye uwanja wa Mkutano wa Mbunge wa Kishapu baada ya kulikzindua na kulikagua JengoJipya la Skuli ya Maandalizi ya Kata ya Somagedi Jimbo la Kishapu Mkoa wa Shinyanga. 
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh. Suleiman Masoud Chambi aliyeruka juu mwenye shati ya Kijani akipanda mdadi kucheza ngoma ya Wafugaji wa Jimbo la Kishapu kwenye Mkutano wake wa kutoa Taarifa ya Utekelezaji waIlani ya Uchaguzi.
Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mh. Aza Hilal Hamadi akitoa Taariofa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika Kipindi cha Mwaka Mmoja.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh. Suleiman Masoud Chambi akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa Mwaka 2015 -2019 katika Mkutano uliofanyika katika Kata ya Somagedi.
Balozi Seif akiwakabidhi saruji Madiwani wa Kata zilizomo ndani ya Jimbo la Kishapu iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Chambi kukamilishaujenzi wa Miradi yao waliyoianzisha.
Balozi Seif  akitembelea Kitengo ya matibabu ya Meno katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambacho kinaendelea kutoa huduma vizuri baada ya kukipatia msaada wa Vifaa MieziMitano iliyopita.
Wa kwanza kushoto anayetoa maelezo ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ambae pia ni Kaimu Daktari Mkuu wa Wilaya Dr. Masoud Mkumbwa.

Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.