Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Baraza la Eid El Hajj katika Viwanja vya Dole Wilaya ya Magharibi"A" Unguja iliofanyika Kitaifa katika Wilaya hiyo leo.
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein amewasisitiza
wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea
kutoa baraka hio ambayo haina mbadala kwa wananchi wa Zanzibar.
Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake
aliyoitoa katika Baraza la Idd El Hajj lililofanyika huko katika viwanja vya
Langoni, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambalo lilihudhuriwa na
viongozi mbali mbali pamoja na wananchi.
Katika hotuba yake hiyo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa bila
ya amani maendeleo hayawezi kupatikana na hata waumini hawatoweza kupata wasaa
wa kufanya ibada kwa utulivu.
“Tunayasikia matukio mbali mbali ya kusikitisha yanayotokea
katika mataifa mengine,ambako amani imekosekana yanayotendeka huko ni vurugu,
udhalilishji na ukatili wa kila aina, waumini wenzetu wamo ndani ya fadhaa
hawana maendeleo, hawana hata utulivu wa kufanya ibada ili waungene na wenzano
kusherehekea Sikukuu mbali mbali”,
aliongeza Alhaj Dk. Shein.
Alieleza kuwa amani ni miongoni mwa baraka ambazo Mwenyezi
Mungu amezitoa kwa wananchi na iwapo itachezewa kwa kujihusisha na vitendo vya
uvunjifu wa sharia, itakuwa neema hiyo waliyopewa wanaikufuru na Allah atakuwa
hayuko radhi.
“Tumshukuru Mola wetu kwa kutujaalia kuwa na amani katika
nchi yetu, nami kila nikipata nafasi ya kuzungumza nanyi wananchi wenzetu
nimekuwa nikisisitiza juu ya umuhimu wa kuendelea kudumisha amani” alisema
Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein ameeleza kuwa kutokana na kuendelea
kuwepo kwa amani na utulivu Zanzibar inaendelea kupiga hatua na kuimarika kwa
uchumi wake kwa kila mwaka.
Alifahamisha kuwa hali hiyo kukua kwa uchumi inaiwezesha
Serikali kupata nguvu zaidi za kuimarisha miundombinu ya uchumi na kutoa huduma
mbalimmbali ambazo wananchi wanazihitaji kwa ajili ya maisha ya kila siku
katika hali iliyo bora zaidi.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa ukuaji huo wa uchumi
umeiwezesha Serikali kuimarisha maslahi ya wafayakazi wa Serikali na kuinua
kipato chao pamoja na kupata uwezo wa kuitekeleza mipango mbalimbali
wanayoipanga.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa ni jambo la
faraja kuona kuwa hali hiyo vile vile imewawezesha baadhi ya watumishi kupata
uwezo wa kifedha kwenda kutekeleza ibada ya Hijja mapema badala ya kusubiri
fedha za kiinua mgongo kama ilivyozoeleka.
Aliongeza kuwa taarifa kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya
Amana zinaeleza kuwa jumla ya Watanzania 2,500 wamejitokeza mwaka huu kwa ibada
ya Hijja wakiwemo 1,700 kutoka Taasisi 22 za Zanzibar zinazoshughulikia masuala
ya Hijja na watu 800 kutoka Tanzania Bara.
“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha ndugu zetu
kwenda kuitekeleza ibada hio kwa hakika si kila aliyejaaliwa kupata neema hizo
hudiriki kwenda kuitekeleza ibada hio kubwa” alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein aliwahimiza waumini wa dini ya
Kiislamu kwa wale wenye uwezo wa kifedha na afya njema kuepukana na vipingamizi
visivyo na msingi ambavyo vinaweza kwenda kuitekeleza ibada ya Hijja na badala
yake waende kuitekeleza ibada hiyo.
Alhaj Dk. Shein pia, alisisitiza kuwa ni wajibu kuhimizana
ili wale wenye uwezo wawasaidie Waislamu wengine kwenda kufanya ibada hio kwa
kuzingatia miongozo ya dini iliyopo kwani watu wanaosaidia katika mambo ya
kheri bila ya shaka wana ujira mkubwa mbele ya Allah.
“Ilivyokuwa leo tunasherehekea sikukuu ya Idd el Hajj, ni
wajibu kuhakikisha kuwa furaha hio ipo katika familia kwa kula vizuri, kuvaa
vizuri na kuendeleza furaha kwa ndugu na majirani”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Aliwataka wananchi kujitahidi kuwalea watoto sambamba na
kuwarithisha misingi ya kuheshimu, kukinai na kuthamini vilivyo vyao kwani hiyo
ni misingi ya uzalendo pamoja na kuwafunza maadili mema, silka, desturi na
utamaduni waliourithisha kutoka kwa wazee.
Aliongeza kuwa miongoni mwa mapenzi makubwa ambayo mzazi
anawajibika kwa mtoto wake ni kuhakikisha kuwa anapata elimu ya dini na dunia
kwani kumpa mtoto elimu ni haki yake ili aweze kupata ufunguo huo muhimu wa
maisha yake.
Alhaj Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kueleza kuwa
Wazanzibari wote wanaungana na Watanzania wenzao katika maombolezo kama
alivyotangaza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli
siku tatu kuanzia juzi Jumaamosi tarehe 10, Agosti 2019 ambapobendera zote
zitapepea nusu mlingoti katika maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hatua hiyo imetokana na ajali ya kuanguka na kuripuka kwa
lori la mafuta katika eneo la Msamvu Mkoani Morogoro na kusabisha vifo vya watu
Zaidi ya 64 na majeruhi kadhaa ambapo tukio hilo limetokea wakati wananchi
wakiwa katika matayarisho ya sikukuu ya Idd el Hajj tarehe 10, Agosti, 2019.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana wote
waliofaulu kwa daraja za juu katika mitihani yao ya Kidato cha Sita mwaka 2019
kwani anaamini kwamba wale waliojitahidi na waliojiandaa vizuri ndio wengi
katika waliopata matokeo bora zaidi kwani juhudi ndio shina la mafanikio huku
akiwapongeza wazazi, walimu na skuli zote zilizofanya vizuri.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuiagiza
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wazitafute sababu zilizopelekea baadhi ya
skuli kuwa miongoni mwa skuli kumi za mwisho katika matokeo hayo na hatimae
waandae mbinu za ufumbuzi ambazo zitaleta mafanikio hapo baadae.
Katika hotuba yake hiyo pia, Alhaj Dk. Shein
aliwahakikishia wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga
fedha za kutosha, ili kuendelea kutoa huduma za afya na elimu bure kama
zilivyoelezwa kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015/2020.
Alhaj Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya
kazi kwa bidiii ili uchumi ukue kwa kasi kubwa na hatimae iweze kutekelezwa
mipango yote kwa ufanisi zaidi.
Rais Dk. Shein kwa mara nyengine tena alitumia fursa hiyo
kuwakumbusha viongozi na watendaji wote wa Serikali kwamba waengeze kasi, bidii
na ari katika kuyatekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi kwa
kuzingatia bajeti iliyopitishwa na fedha zilizoidhinishwa kwa mwaka 2019/2020.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Makamo wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid
Karume na viongozi wengineo wa vyama vya siasa, serikali pamoja na Taasisi za
Kijamii.
Mapema asubuhi Alhaj Dk. Shein aliungana na waumini mbalimbali
wa Dini ya Kiislamu katika Sala ya Idd el Hajj pamoja na hotuba vyote
vilivyofanyika katika viwanja vya Beit Al Raas ambayo vyote kwa pamoja
viliongozwa na Sheikh Twaha Hussein Twaha kutoka Kianga.
Katika hotuba yake hiyo ya Idd Sheikh Twaha alieleza
umuhimu wa ibada ya Hijja kwa Waumini wa Dini ya Kislamu huku akisisitiza haja
ya kuimarisha amani na utulivu nchini na kuepuka kuivunja kwa maneno na hata
vitendo.
Baada ya hapo Alhaj Dk. Shein alifika Ikulu ndogo ya
Kibweni ambako alisalimiana na Masheikh mbalimbali wakiwemo Masheikh kutoka
Wilaya ya Magharibi “A” na kutakiana kheir ya Sikukuu ya Idd El Hajj.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment