Habari za Punde

CCM Zanzibar Yasema Sera Zake Zipo Rafiki Kulinda Haki za Watoto

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao(kulia),akimkabidhi zawadi Mdhamini wa Nyumba ya kulelea Watoto ya Mazizini Bi.Chumu Ali Abeid katika ziara hiyo ya Katibu Mwenezi.

Na.Is-haka Omar - Zanzibar.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao, amesema CCM inasimamia vyema Ilani yake kwa kuhakikisha kundi la Watoto wanapata haki zao za msingi zikiwemo kupatiwa Malezi bora,Huduma bora za Afya,Elimu na kulindwa.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kumtembelea Mtoto Hajra Abdillahi Abdalla, aliyeokotwa na Mbwa baada ya Mama yake kumzaa na kumtupa kichakani huko Pemba miezi kadhaa iliyopita kwa sasa analelewa katika Kituo cha kulelea Watoto cha Mazizini Unguja.

Alisema CCM imeweka Sera bora na rafiki za kulinda maisha ya watoto ili wapate huduma muhimu zinazowawezesha Watoto kupata mazingira bora ya Kimalezi.

Akizungumzia Tukio la kutupwa kwa Mtoto Hajra alisema vitendo vya aina hiyo vinatakiwa kupingwa vikali na jamii na yeyote atakayebainika achukuliwe hatua kali za klisheria kwani Mtoto anakuwa hana kosa lolote la kupelekea kutupwa.

Alisema Mtoto huyo aliyetupwa na Mama yake vichakani mara tu baada ya kuzaliwa kisha akaokotwa na Mbwa na kumpeleka sehemu salama za Watu ni kitendo cha kumshukru Mwenyezi Mungu.

Aliishukru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka za kulinda Maisha ya Mtoto huyo sambamba na kumpatia huduma bora za kimalezi kama walivyo Watoto wengine katika Jamii.

Katibu huyo aliwataka Walezi wa Watoto hao katika Nyumba hiyo,kuhakikisha wanawalea katika misingi Bora ya Kimaisha hasa ya Kidini na kuwajengea mazingira ya kupenda kusoma ili watakapoanza kujitegemea wawe na uwezo wa kujimudu kimaisha.

Amewasihi Watoto hao kujilinda dhidi ya Vitendo vya udhalilishwaji kwani kuna baadhi ya Watu wanatumia mbinu mbali mbali za kuwaadaa watoto kwa nia ya kuwadhalilisha.

Alitoa wito kwa Serikali kuendelea kuthibiti Vitendo vya Udhalilishaji kwani vinaharibu Maisha ya Watoto ambao ndio Viongozi na Wataalamu wa Taifa wa baadae.

Naye Mdhamini wa Nyumba ya kulelea Watoto Mazizini Bi.Chumu Ali Abeid, aliwapongeza Viongozi hao kwa kutembelea Watoto wanaolelewa katika Nyumba hiyo.

Alisema kuwa hali ya Mtoto Hajra inaendelea Vizuri na kwa sasa anapewa huduma bora kwa uangalizi mkubwa hali inayochangia Afya yake kuimarika kila siku.

"Tunawalea Watoto wa aina mbali mbali na Afya zao zipo vizuri kutokana na Malezi Bora wanayopatiwa wakati wote",alisema Mdhamini huyo Bi.Chumu.
Katibu huyo alifuatana na Viongozi mbali mbali Wanawake wa UWT pamoja na Makatibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Zanzibar, walitoa zawadi mbali mbali kwa Watoto wanaolelewa katika Nyumba hiyo.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao,akiwa amembeba Mtoto Hajra Abdillahi Abdalla aliyetupwa na Mama yake Kichakani baada ya kuzaliwa na akaokotwa na Mbwa hivi sasa analelewa na Serikali katika Nyumba ya kulelea Watoto Mazizini.
BAADHI ya Watoto wanaolelewa katika Nyumba ya kulelea Watoto ya Mazizini Zanzibar baada ya kutembelewa na KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.