Habari za Punde

NAIBU WAZIRI KANYASU AWATAKA WASOMI WAZIHUDUMIE JAMII ZAO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu( wa pili kulia) akiwa na Waziri wa Habari  Utalii na Mambokale wa Zanzibar, Mhe. Mahamoud Kombo wakiwa kwenye picha ya pamoja na mhitimu wa Chuo Kikuu, Kalmat Tamal aliyetunukiwa zawadi ya hundi yenye thamani ya laki tano  kufuatia kuitumia vizuri elimu yake katika kujitolea mchango wake mkubwa kwa jamiii alikotoka.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewataka wahitimu waliomaliza Vyuo vikuu waliosomeshwa kupitia mradi wa kuzisaidia familia duni katika vijiji vinavyopakana  na maeneo ya Hifadhi wakumbuke kurudi katika vijiji vyao ili wakawahudumie wananchi wa maeneo hayo.

Pia, Amewataka wahitimu hao wakawe mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa jamii zao juu ya umuhimu wa kulinda Hifadhi kwa vile wao miongoni mwa  wanufaika wa shughuli za Uhifadhi nchini.

Akizungumza kwenye hafla ya kuwapongeza wahitimu 50 katika ngazi ya Astashahada na Shadada katika kozi tofauti iliyofanyika Jana usiku mkoani Arusha,  Mhe.Kanyasu ameitaja  Asasi isiyo ya Kiserikali ya  Africa Foundation kupitia  kuwa ni  moja ya wadau muhimu  wa Uhifadhi ambao ni mfano wa kuigwa katika kuzisaidia familia masikini.

Africa Foundationi ni Asasi  inayotekeleza  mradi wake  kwa kusaidia  kulipa ada kwa wanafunzi kutoka familia  duni zinazoishi karibu na Hifadhi kujiunga  na vyuo vikuu nchini kama inavyofanya  Bodi ya Mikopo ya Vyuo Vikuu ( HESLB).

Asasi hiyo inayoendesha baadhi ya Hoteli za kitalii ndani ya Hifadhi za Taifa nchini na imekuwa ikisaidia familia duni kwa kuwalipia ada wanafunzi hao ikiwa kurudisha kwa jamii kile walichopata kupitia Hoteli hizo.


Mkopo huo ni tofauti na ule wa HESLB ambapo mara baada ya kusomeshwa na Africa Foundation wanafunzi hao hulipa mkopo huo kwa kuihudumia jamii alikotoka kulingana na kozi aliyoisomea badala ya kurudisha pesa.

Naye, Waziri wa Habari, Utalii na Mambokale, Mhe.Mahamoud amewataka wahitimu hao wakaitumie elimu hiyo kwa kuwasaidia vijana wengine waweze kutambua thamani ya elimu katika maisha yao

'' Nendeni huko mkaibadilishe jamii yenu ianze kutambua umuhimu wa  kutunza maliasili tulizonazo,  alisisitiza Mhe, Waziri Kombo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa mkoa Arusha, Jerry Muro  amewataka wanafunzi hao wakaitumie vizuri elimu yao kwa kuanza kuzibadili kifikra familia zao pamoja na jamii kuhusu umuhimu wa  kutunza Hifadhi  na kuachana na vitendo vya ujangili ili watalii waendelee kuja nchini

" Elimu yenu ikawe silaha kwa wale wote wanajihusisha na vitendo vya ujangili" alisisitiza Mhe.Muro.

Naye Mkurugenzi wa Africa Foundation kwa nchi za Africa Mashariki, Dkt. Mkomeni Mgonho amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuzifanya familia hizo kuthamini na kuona thamani ya shughuli za Uhifadhi.

Aidha, Amesema kuwa pia ni mchango wao wanaourudisha katika jamii kwa kile wanachopata kupitia Hoteli za kitalii.

Mbarouk Salum ambaye ni mhitimu wa fani ya Udaktari katika Chuo Kikuu kishiriki cha Muhimbili amesema kitendo cha Asasi hiyo kuwasaidia kwa kuwalipia ada ni moja ya alama kubwa za matumaini kwa familia hizo ambapo zitaweza kubadili maisha kwa kuandaa kizazi bora kitakachopenda na kuthamini shughuli za Uhifadhi.

Africa Foundation imesaidia kuwalipia ada wanafunzi 45 wa Kitanzania pamoja wanafunzi wa 5 wa kutoka nchini Kenya wote wakiwa wanaishi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.