Habari za Punde


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein na Mrithi wa Utawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, wakishuhudia utiaji wa saini, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umewakilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Balozi.Mohamed Ramia Abdiwawa na kwa upande wa Mfuko wa "Khalifa Fund" umewakilisha na Mwenyekiti wa Mfuko wa “Khalifa Fund” Sheikh. Hussain Ali Nowais alisaini kwa niaba ya Serikali ya (UAE). 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameshiriki katika utiaji saini Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kupitia Mfuko wa “Khalifa Fund” kwa ajili ya kuwasaidia Vijana wa Zanzibar.

Makubaliano hayo yataipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata Dola za Kimarekani Milioni 10 sawa na Shilingi za Kitanzani Bilioni 23 kupitia Mfuko huo ambazo zitasaidia kuwajengea uwezo Vijana wa Zanzibar.

Hafla hiyo ya utiliaji saini pia ulihudhuriwa na Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, Mrithi wa Mtawala wa Abu Dhabi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi wa Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambao ulifanyika katika makaazi yake yaliopo mjini Abudhabi ambako ndio Makao Makuu ya Nchi za Umoja huo.

Utiaji saini Mkataba huo wa Makubaliano kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulifanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa  niaba ya Serikali na Mwenyekiti wa Mfuko wa “Khalifa Fund” Hussain Ali Nowais alisaini kwa niaba ya Serikali ya (UAE).

Rais Dk. Shein na mwenyeji wake Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, walishuhudia tukio hilo kubwa na la kihistoria ambalo linatokana na matunda ya ziara ya Dk. Shein aliyoifanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) mnamo mwezi Januari mwaka 2018 kufuatia mwaliko wa Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan.

Fedha hizo zitakazopatikana katika Mkataba huo wa Makubaliano ni kwa ajili ya vijana wa Zanzibar kuelekea kujitegemea kimaisha hasa kwenye kujishughulisha na miradi midogo midogo na  ya kati, biashara pamoja na kazi za ujasiriamali.

Aidha, fedha hizo zitasimamiwa na Mfuko huo wa “Khalifa Fund” kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar kwa mwaka huu wa fedha 2019 hadi 2013 ambapo itakuwa ndani ya miaka mitano.

Wakati huo huo, katika tukio hilo Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na mwenyeji wake Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan walipata fursa ya kufanya mazungumzo ambapo mazungumzo hayo yalijikita zaidi katika kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya pande mbili hizo.

Katika mazungumzo yao viongozi hao walisisitiza ushirikiano huo wa kidugu na kueleza kuwa utaendelea kuimarika kutokana na utiaji huo wa saini kwa makubaliano baina ya pande mbili hizo ambapo utasaidia katika kuwainua vijana wa Zanzibar kiuchumi.

Pamoja na hayo, viongozi hao walizungumza kuhusu ushirikiano katika maeneo mengine muhimu ikiwa ni pamoja na biashara, kuimarisha sekta ya utalii, kilimo kikiwemo kilimo cha umwagiliaji maji, miundombinu, sekta za kijamii sambamba na kubadilishana uzoefu katika kupanga mipango ya kiuchumi.

Kiongozi wa Abudhabi kwa upande wake alimuhakikishia Rais wa Zanzibar kuwa yale yote waliyokubaliana wakati wa ziara yake Dk. Shein aliyoifanya nchini humo mwezi Februari mwaka jana 2018 yatatekelezwa ipasavyo.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa shukurani kwa kiongozi huyo wa Abudhabi na Umoja wa Nchi za Falme ya Kiarabu (UAE) kwa namna wanavyowathamini ndugu zao wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wataendeleza uhusiano na ushirikiano mliopo wa kihistoria baina ya pande mbili hizo huku akisisitiza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuendeleza azma ya Serikali ya kuwasaidia vijana wa Zanzibar ili kuweza kujikwamua kimaisha.
Miongoni mwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  walioshuhudia tukio hilo ni Waziri Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said pamoja na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk.
Hapo jana jioni (trh 27.9.2019), Rais Dk. Shein alihudhuria dhifa maalum ya chakula cha usiku aliyoandaliwa na mwenyeji wake Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi huko katika Hoteli ya “The Ritz Carlton” katika Jangwa la Wadi ya hifadhi ya asili iliyopo nje kidogo ya mji wa Ras Al Khaimah.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi hapo jana (trh 27.9.2019) pia, zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano (MOU) juu ya ujenzi na matengenezo ya Hospitali ya Wete Pemba.

Makubaliano hayo yataipelekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupata Dola za Kimarekani Milioni 10 sawa na Shilingi za Kitanzani Bilioni 23 kupitia Mfuko huo ambazo zitasaidia katika ujenzi na matengenezo makubwa ya Hospitali hiyo ikiwewa ni pamoja na upanuzi wake.
Ziara hiyo ya Dk. Shein nchini Ras Al Khaimah ilianza tarehe 23 na kumaliza leo tarehe 28 Septemba mwaka huu na kesho tarehe 29 asubuhi  anatarajiwa kurudi nyumbani  ambapo katika ziara hiyo alipata fursa ya kuzungumza na mwenyeji wake Mtawala wa Ras-Al-Khaimah  Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi.
Pia, Rais Dk. Shein alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali wa nchi hiyo, kutembelea miradi ya maendeleo pamoja na kushiriki katika utiaji saini Mkataba wa Makubaliano kati ya SMZ na UAE, kupitia Mfuko wa Maendeleo wa “Khalifa Fund” pamoja na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa UAE mwenye makao makuu yake mjini Abudhabi.
Dk. Shein katika ziara hiyo alifuatana mefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein, Waziri wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu, Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib.
Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Said Hassan Said, Balozi Mohamed Haji Hamza Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa upande wa Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Serikali. 
 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.