Habari za Punde

Wanafunzi watakiwa kujikinga na vitendo vya udhalilishaji

Na Mwashungi Tahir  - Maelezo        
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Tunu Juma Kondo amewataka wanafunzi wa Skuli ya Chumbuni kujikinga na vitendo vya udhalilishaji na mimba za utotoni.
Akitoa elimu ya kujikinga na vitendo hivyo katika Skuli ya Chumbuni Msingi, Tunu amewataka wanafunzi kujiepusha kupokea zawadi ama pesa kwa watu wasiowafahamu.
Amewashauri wanafunzi wa skuli hiyo kutokubali kupakiwa kwenye gari za watu ambao hawawajui kwani ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na vijana wanaofanya vitendo vya udhalilishaji kukamilisha malengo yao.
Aliwambia kwamba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amefanya juhudi kubwa ya kuimarisha sekta ya elimu na kuendeleza azma ya Mapinduzi ya mwaka 1964 hivyo amewata kutumia fursa hiyo kutafuta elimu ili waweze kujenga maisha ya kujitegemea hapo baadae.
Aliwaeleza wanafunzi wa Chumbuni kujiwekea malengo na kuelewa kuwa miongoni mwao watakuwa wataalamu wa fani mbali mbali wa kuliongoza Taifa lao.
“Tunatarajia miongoni mwenu watatoka viongozi, madaktari, walimu, waendesha ndege na wataalamu wa fani nyengine hivyo ongezeni juhudi katika masomo yenu.” Naibu Katibu Mkuu UWT alisisitiza.
Tunu Juma aliwanasihi watoto wa kiume wa skuli hiyo kuacha tabia ya kuwadhalilisha wanafunzi wenzao wa kike kwani kufanya hivyo vinaweza kuwaharibia maisha yao.
Nae Katibu wa UWT Wilaya ya Amani Asha Mzee Omar aliwataka wanafunzi hao kuacha ukimya wanapofanyiwa vitendo hivyo na amewashauri kutoa taarifa kwa wazazi wao wanapofanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Nao  wanafunzi wameiomba Serikali itoe adhabu kali kwa wahusika wa vitendo hivyo kwani adhabu wanazopewa zinaonekana kuwa ni ndogo na wamekua wakirudia kufanya vitendo hivyo mara kwa mara.
Naibu Katibu Mkuu UWT amepanga kufanya ziara ya aina hiyo katika skuli zote za wilaya ya Mjini kwa lengo la kutokomeza vitendo vya udhalilishaji.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.