Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Ujenzi wa Miradi ya Maendeleo

Msimamizi wa Miradi ya Ujenzi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Ali Juma Ali akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  kwenye majengo ya Skuli ya Sekondari Kibuteni Mkoa Kusini Unguja inayoendelea kujenga baada ya kusita kwa karibu Miaka Mitano sasa.
Na.Othman Khamis.OMPR.                                                                                             
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Taasisi za Umma na Hata zile binafsi Nchini umefika wakati walazimike kujifunza kwa kuwatumia Wahandisi Wazalendo katika ujenzi wa Miradi yao ili kujiepusha na ulaghai unaoshuhudiwa na Wahandisi wa kigeni.
Alisema ipo miradi mingi iliyojengwa na kusimamiwa na Wahandisi wageni ambayo imesababisha kuitia hasara kubwa Serikali kutokana na baadhi ya ulaghai uliokuwa ukifanywa na Wataalam hao wasio na uchungu na mali za Umma.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati alipofanya ziara maalum ya kukagua Miradi ya Maendeleo katika Sekta ya Elimu Wilaya ya Kusini na kujionea baadhi ya Miradi hiyo hasa Majengo mapya ya Skuli za Sekondari zilizochelewa kukamilika kwa wakati kutokana na mabadiliko ya Wahandisi waaliohusika na ujenzi huo.
Alisema Zipo Kampuni, Taasisi  na Wataalamu Wazalendo wenye uwezo kamili wa kujenga au kuendesha Miradi mikubwa ya ujenzi wanaoweza kutumia muda mfupi na gharama ndogo lakini wanachokizalisha au kukijenga kinakubalika katika viwango vya kuridhisha.
Balozi Seif  akikagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kibuteni, Chuo cha Amali Makunduchi na kuweka jiwe la Msingi la Nyumba ya Walimu Paje aliutahadharisha Uongozi wa Wizara ya Elimu lazima uwe na uangalifu wakati wa kutafuta Wajenzi wa Majengo yao mapya.
“ Lazima ufike wakati kwa Taasisi za Umma kuwepuka Wakandarasi wa Kigeni ambao mara nyingi huhitilafiana kutokana na kila mmoja kutumia Usomi wake unaosababisha kuleta mgongano”. Alisema Balozi Seif.
Aliuhimiza Uongozi huo kuhakikisha kwamba unasimamia vyema katika kuona majengo ya Kibuteni na      Chuo cha Amali vinamalizika kwa muda uliopangwa ili majengo hayo yaweze kutoa huduma kwa Wanafunzi.
Balozi Seif  alisema Wanafunzi wa Visiwa hivi lazima wafurahie matunda ya Mapinduzi kwa vile hawana sababu ya kutokusoma vizuri kutokana na kujengewa mazingira rafiki yenye kuwapa utulivu wa kuendelea na masomo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini kwa uamuzi wake wa ujenzi wa Nyumba ya Walimu hapo katika Kijiji cha Paje ambao utasaidia kupunguza Wanafunzi kuzurura ovyo kutokana na ukosefu wa Walimu.
Alisema kuna haja kwa Halmashauri nyengine kuiga mfano huo ili kupunguza changamoto  za makaazi zinazowakabili Walimu wengi ambao kisera wanawajibika kuwa karibu na Wanafunzi wao katika dhana nzima ya kuongeza ufaulu wao.
Akitoa Taarifa ya Maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kibuteni na Kituo cha Aamali Kisongo Makunduchi  Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dr. Idriss Muslih Hijja alisema miradi yote miwili imeshafikia asilimia 55/% ya ujenzi wake.
Dr. Idriss alisema ule wa Kibuteni ulichelewa kumalizika kutokana na mabadiliko ya Mshauri muelekezi hatua iliyosababisha kutafutwa Mwengine pamoja na Mjenzi Mpya wakati ule wa Chuo cha  Amali umechelewa kidogo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa Mchanga kumalizia kazi ya kupiga plasta.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Elimu alisema Wizara inaendelea na jitihada katika kuhakikisha Miradi yote miwili inamalizika ili iwahi kufungulkiuwa ndani ya shamra shamra za Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo  mapema Mwakani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kusini Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema asilimia kubwa ya Walimu wanaofundisha Skuli zilizomo ndani ya Mkoa huo wanaishi Mjini jambo ambalo ni tatizo katika maendeleo ya Kielimu ya Wanafunzi wa Skuli hizo.
Mheshimiwa Ayoub alisema Uongozi wa Mkoa huo kupitia Halmashauri zake kwa sasa umeshaamua kuanzisha Miradi ya Ujenzi wa Nyumba za Walimu  kwa lengo la kukabiliana na changamoto hilo.
Akizungumza na Wananchi pamoja na Viongozi wa Mkoa Kusini alipoutembelea Mradi wa Maji safi na salama uliopo Bwejuu unotarajiwa kusambaza huduma hiyo hadi Michamvi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} kwa jitihada inazochukuwa za kuwapatia huduma za Maji Wananchi walio wengi Unguja na Pemba.
Balozi Seif  alisema Miradi ya Maji safi inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ikiungwa mkono na washirika wa Maendeleo ndani na nje ya nchi ni muhimu kwa maisha na ustawi wa Jamii ya Visiwa hivi.
Akitoa Taarifa ya Maradi huo wa Maji safi uliopo Bwejuu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} Mussa Ramadhan alisema mradiu huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kutoa maji takriban Lita Laki 120,000 katika Visima viwili vilivyochimbwa katika eneo hilo.
Nd. Mussa Ramadhan alisema mabomba yanayolazwa kwenye mradi huo yanatarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita  18, sita kufika kwenye Tangi na zilizobaki Kilomita 16 zitaishia kwenye Vijiji.
Alisema zaidi ya shilingi Bilioni 2.26 zitatumika kukamilisha Mradi huo ambao Bilioni 1.8 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na zilizobakia ni kutoka Serikali ya Rasa L- Khaimah.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar {ZAWA} alifahamisha kwamba mradi huo ambao ni muendelezo wa Ahadi zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  unatarajiwa kukamilika kabla ya Mwaka 2020.
Balozi Seif  akisalimiana na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kibuteni baada ya kuyakagua majengo ya Skuli Mpya ya Kijiji hicho yanayojengwa kuhudumia Wanafunzi wa Wilaya nzima ya Kusini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Majengo ya Chuo cha Amali yaliyopo katika Kijiji cha Kisongo Makundichi akiwa katika ziara ya Siku mbili Mkoani humo.
Balozi Seif akiongozwa na Mkuu wa Mkoa Kusini Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud kukagua Mradi wa Maji safi na salama uliopo Bwejuu Wilaya ya Kusini.
Naibu Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mh. Juma Makungu akiwaomba Viongozi wa Majimbo yanayopitia Mradi wa Maji safi wa Bwejuu kusaidia changamoto zinazowakabili Wataalamu wa Zawa wanaosimamia Mradi huo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.