Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Mradi wa Uzalishaji wa Mayai wa Kuku

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuridhia uwepo wa Miradi ya Uwekezaji Nchini ni katika jitihada zake za kuimarisha Mapato ya Taifa yatakayokwenda sambamba na ongezeko la fursa za Ajira hasa kwa Vijana.
Alisema Wananchi katika baadhi ya maeneo Nchini tayari wanaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Wawekezaji waliokwishaanzisha Miradi yao jambo ambalo huleta faraja kwa Serikali Kuu licha ya maeneo mengine kuibuka malalamiko yanayotokana na masuala ya ulipaji fidia.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi Mkubwa wa ufugaji Kuku wa Mayai { Modern Agricultural Product - MAP} ulioanzishwa katika Kijiji cha Kandwi Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema Sekta ya Uwekezaji katika miradi mbali mbali imeanza kuleta mafanikio akatolea mfano Mradi huo wa Ufugaji Kuku utakaosaidia pia Sekta ya Utalii inayohitaji bidhaa ya Mayai katika utoaji huduma zake za kila siku kwa Wageni wanaofika.
Balozi Seif aliushauri Uongozi wa Mradi huo wa Kuku wa Mayai katika malengo yake ya baadae kufikiria uanzishaji wa utotoaji wa vifaranga hapa Nchini ili kuwasaidia wafugaji Wadogo kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa Vifaranga hivyo.
Alisema mahitaji ya bidhaa zinazotokana na Kuku yapo mengi Nchini yaliyopelekea Wananchi wengi kujishughulisha na Miradi ya Ufugaji lakini bado kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa vifaranga kinawakumba ambapo wakati mwengine inalazimika kuagizwa nje ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Modern Agricultural Product kwa uamuzi wake wa kuwekeza katika Kijiji cha Kandwi na kuwapongeza Wananchi wa eneo hilo kwa jinsi walivyotoa ushirikiano wa karibu wakati wa kuupokea mradi huo.
“ Nimefarajika sana kwa kutosikia malalamiko wala mgongano kati ya Wananchi wa eneo hili na Muwekezaji huyu wa Mradi wa Kuku wa Mayai ambayo wakati mwengine tumeshayazoea katika maeneo mengine hasa wakati wa ulipaji wa fidia”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alieleza kwamba Mradi huo wa Ufugaji wa Kuku wa Mayai kwa kiasi kikubwa utasaidia sana Sekta ya Utalii  inayosimamiwa vyema na Serikali Kuu hasa katika Mumo wake wa Utalii kwa wote unaomtaka kila Mwananchi kuwajibika kutoa mchango wake wakiwemo Wawekezaji.
Mapema Mkuu wa Mradi wa Ufugaji Kuku wa { Modern Agricultural Product - MAP} Mzee Jaffar Hussein alisema mradi huo ulioanzishwa na Wawekezaji Wazawa umeridhiwa na Wananchi wa Kijiji cha Kandwi na kuanza rasmi Ujenzi wake Mwaka huu wa 2019.
Mzee Jaffar alisema Wananchi wa Zanzibar wanapaswa kujenga matumaini ya kupata huduma za bidhaa ya mayai kwa bei nafuu ya Shilingi Elfu 5,000/- kwa Trea Moja mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Mradi huo ifikapo Mwaka 2020.
Alisema Taasisi yake tayari imeshawekeza miradi mingi ya Kijamii Nchini Tanzania na baadhi ya Mataifa Duniani na kufikiria azma ya kuwekeza Nyumbani Zanzibar wazo ambalo limepokelewa na kukubaliwa moja kwa moja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“ Wananchi wajiadae kula mayai kwa bei hafifu ya shilingi elfu Tano tuu kwa Trea Moja”. Alisisitiza Mkuu huyo wa Mradi wa Kukuwa Mayai wa { Modern Agricultural Product - MAP}.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Modern Agricultural Product – MAP Bwana Mahir Abdulrahman alisema uzalishaji wa mayai katika Mradi huo Mkubwa Nchini Tanzania utazingatia zaidi mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Uendeshaji wa Mashine zake.
Bwana Abdulrahman alisema licha ya kutotaja idadi halisi ya ajira lakini alisema Uongozi wa Mradi huo utazingatia zaidi kuajiri Wananchi Vijana wanaozunguuka eneo hilo pamoja na wale waliomo ndani ya Jimbo la Chaani na Wilaya ya Kaskazini “A”.
Mradi wa Kuku wa Mayai wa Agricultural Product – MAP unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 3.2 sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni Saba Nukta Nane.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.