Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMh.Balozi Seif Ali Iddi Ziarani Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiupongeza Uongozi wa Wizara ya Ujenzi kupitia Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara {UUB} kwa juhudi zao za kuimarisha miundombinu ya Bara  bara Nchini wakati akikagua Bara bara ya Ole Kengeja.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais Wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari  imeshaamua Miundombinu ya Miradi yake ya Maendeleo kusimamiwa na Wahandisi  pamoja na Washauri Waelekezi Wazawa ili kulinda Heshima ya Taaluma yao inayopaswa kufanyiwa kazi.
Alisema uamuzi huo mbali ya kupungua gharama kubwa zinazosababishwa na Wahandisi na Waelekezi Wageni  lakini pia utasaidia kuepuka urasimu unaokwaza Mikataba kati ya Serikali na  Wahandisi wa Kigeni.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiendelea na ziara yake ya Siku Tatu Kisiwani Pemba kukagua Miradi ya Maendeleo iliyo chini ya Taasisi ya Umma, Wananchi pamoja na kuelewa changamoto zinazosababisha kuzorota kwa baadhi ya Miradi hiyo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejikita kusimamia upatikanaji wa Vifaa na Zana za Kazi kwa Wahandisi Wazawa kupitia Idaya ya Utengenezaji na Utunzaji wa Bara bara Zanzibar {UUB} ili Miradi hiyo iendelezwe katika Kiwango cha ubora unaohitajika.
“ Juhudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuipatia Vifaa vya Kisasa  Idara ya Utunzaji na Utengenezaji wa Bara bara {UUB}ili wawe na uwezo kamili wa kulikabili jukumu zito wanalokabidhiwa”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wahandisi, Wataalamu na Watendaji wa Ujenzi wa Bara bara ya Ole hadi Kengeja Mkoa wa Kusini Pemba alipoikagua na kuwataka wazingatia muda wa ujenzi waliotoa ili Wananchi wafaidike na Mradi huo.
Alisema Ujenzi wa Bara bara za lami unaofanyika katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba umewakomboa Wananchi waliowengi kwa kutumia Bara bara hizo kwa kuweza kusafirisha Mazao yao sambamba na kuzitumia katika huduma zao za Kijamii za kila siku.
Mapema Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Ahmed Baucha alisema  Bara bara hiyo ya Ole hadi Kengeja yenye urefu wa Kilomita 35  kwa sasa imeshafikia Kilomita 32 kwa hatua kwanza ya uwekaji wa Lami ya Maji.
Nd. Baucha alisema Wahandisi hao wanatarajia kuanza uwekaji wa Lami ngumu ndani ya Wiki hii wakitarajia kukamilika kwake wanamatumaini ya kufikia ufuikapo Mwezi Mei au Juni Mwanzoni Mwaka 2020.
Balozi Seif katika ziara hiyo alipata wasaa wa kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Hoteli ya Wilaya ya Mkoani iliyo chini ya Usimamizi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar {ZSSF}.
Akitoa ufafanuzi wa Ujenzi wa Hoteli hiyo ya Mkoani Mhandisi wa Ujenzi huo Khamis Rashid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi huo umeongeza Ghorofa Moja juu utaokwenda sambamba na Uwekaji wa Lifti kwa kuzingatia Watu wenye mahitaji Maalum.
 Mhandisi Khamis alisema ujenzi huo umepangwa kukamilika mnamo Mwezi Mapema Mwakani lakini zipo changamoto za upatikanaji wa Kokoto na Mchanga lakini vifaa vya ndani tayari vimeshawasili Nchini kwa ajili ya kukamilisha kazi za Ujenzi.
Akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano wa Umoja ni  Nguvu Uliopo Mkoani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Uongozi wa Barala la Mji Mkoani kwa kazi kubwa ya kusimamia Ujenzi huo.
Balozi Seif alisema Ukumbi wa Mikutano wa Mkoani pamoja na Hoteli ya Wilaya hiyo ni Majengo yenye Historia ndefu inayostahiki kuheshimika pamoja na kulindwa ili kuweka Kumbukumbu kwa Kizazi cha sasa na kile kijacho.
Aliutaka Uongozi wa Baraza la Mji Mkoani kuendelea kufuatilia taratibu za kukamilika kwa Ujenzi wa Ukumbi huo kwa kuwasiliana na Wizara ya Fedha na Mipango ili ile azma na kujengwa kwa Ukumbi huo ifikie.
Mapema Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani Nd. Rashid Abdulla Rashid alisema Ujenzi wa Ukumbi huo unatokana na wazo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein la kuutaka Uongozi  wa Wilaya kuuujenga Ukumbi huo ili kuepuka Mikutano ya Viongozi kufanyika katika maeneo ya Skuli.
Nd. Rashid alisema Ukumbi huo ambao unatarajiwa kuchukuwa Watu 1,000 kwa wakati Mmoja na kugharimu jumla ya shilingi Milioni Mia 286,000,000/- utasaidia kuleta faraja kwa Viongozi wa Serikali na hata wa Vyama vya Kisiasa kwa kufanya Mikutano na Vikao vyao katika hali ya utulivu na Amani.
Wakati huo huo Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCMalikagua maendeleo ya  Ujenzi wa Ofisi ya CCM ya Tawi la Kanga pamoja na Ofisi ya Chama hicho ya Wilaya iliyopo Mjini Mkoani.
Katika nasaha zake Balozi Seif alisema ni vyema kwa Viongozi pamoja na Wanachama  wa Chama cha Mapinduzi wakajiandaa kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwakani wakiwa katika mazingira ya Umoja  na  Mshikamano.
Balozi Seif  aliwatahadharisha Wanachama hao  kuepuka fitna, Majungu na makundi ambayo Mwanachama atakayebainika kujihushisha na tabia hiyo Uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi hautasita kumuengua fisadi huyo endapo ataamua kugombea nafasi ya Uongozi.
Alisema Watu wenye tabia kama hizo kwa muda mrefu wamekuwa wakichangia kukiyumbisha Chama Cha Mapinduzi hasa wakati unapofikia kuanza kwa kura za maoni sambamba na kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwapongeza Viongozi na Swananchama wa CCM Tawi la Kangani na Ofisi ya Wilaya ya Mkoani kwa kitendo chao cha kuanzisha Ujenzi wa Ofisi zao zitakazolingana na hadhi ya Chama chenyewe.
Aliwahakikishia Wana CCM na Wananchi wa Wilaya ya Mkoani na Mkoa wa Kusini Pemba  kwamba Serikali zao zote mbili Nchini Tanzania Bara na Zanzibar zitaendelea kujenga mazingira ya kustawisha maisha yao ya kila Siku kwa kuimarisha Miundombinu katika Mitari ya Maendeleo na ile ya Kiuchumi.
Balozi seif alisema Serikali zote mbili zinawapenda Wananchi wake . Hivyo na wao kwa upande wao wana wajibu wa kuzilinda Rasilmali za Taifa  hasa zao la Karafuu kwa upoande wa Zanzibar ambalo mapato yake ndio yanayoshughulikia hasuama hayo.
Katika kuunga mkono Wanachama hao wa Tawi la Kangani na Ofisi ya Wilaya ya Mkoani Balozi Seif  alisema atazungumza na Viongozi kuona namna gani na yeye ataingia nguvu zake katika kuona majengo hayo yanamalizika kama yalivyopangwa.
Hamasa hiyo ya Balozi Seif  aliwashawishi Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum  Mheshimiwa Said Soud  kuahidi kuchangia Mifuko Sitini ya Saruji wakati Mwenzake  Mheshimiwa Ali Juma Khatib ambae ana asili ya Kijiji hicho Umamani aliahidi kuchangia Mifuko Sabini ya Saruji zote zikilenga kuongeza nguvu ya Ujenzi wa Tawi la Kangani.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mkoani Nd. Mohamed Ali Mohamed akimkaguza Balozi Seif  akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa kuangalia maendeleo ya Ujenzi wa Tawi la CCM Kangani Wilaya ya Mkoani.
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.