Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akimsikiliza mgeni wake Balozi wa Jamhuri ya Korea Nchini Tanzania Mhe.CHO Taeick wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar na kusisitiza haja ya kuwepo ushirikiano katika sekta ya utalii baina
ya pande mbili hizo.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania CHO Taeick.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar imeweza kuimarika
katika sekta ya utalii kutokana na vivutio kadhaa vilivyopo sambamba na
mikakati madhubuti iliyowekwa hivyo, ni jambo la busara iwapo watalii kutoka
Jamhuri ya Korea watakuja kwa wingi kuitembelea Zanzibar.
Aliongeza kuwa katika
kuhakikisha uhusiano na ushirkiano unaimarika zaidi kati ya pande mbili hizo
hasa katika sekta ya utalii ipo haja ya kuwepo mashirikiano kati ya Zanzibar na
kisiwa cha Cheju kiliopo Jamhuri ya Korea ambacho ni maarufu duniani katika
sekta ya utalii.
Aidha, Rais Dk. Shein
alisisitiza kwamba katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana kwenye
mashirikiano katika sekta ya utalii ipo haja ya kuanzisha safari za ndege kati
ya Zanzibar na Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la ndege la Korea.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Jamhuri ya Korea imekuwa mshirika mwema wa maendeleo ya Zanzibar kwani
imekuwa ikionesha juhudi zake na kuwa bega kwa bega na Zanzibar katika
kuimarisha miradi hiyo ya maendeleo.
Alieleza kuwa mbali ya
Jamhuri ya Korea kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta hizo za
maendeleo pia, alieleza haja ya kutoa mashirikiano kwa kuisaidia Zanzibar
katika kutoa mafunzo kwa mafundi wa Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC)
Televisheni.
Alieleza haja ya
kupatiwa mafunzo hayo ni kutokana na Shirika hilo kuanza kuwa na upungufu wa
wataalamu hao ambao ndio rasilimali muhimu katika kuendesha Shirika hilo kutokana
na wakati uliopo kutokana na wataalamu hao wengi kufika muda wao wa kustaafu kazi.
Alisisitiza kwamba
kuwepo kwa mitambo mipya pamoja na vifaa kadhaa vilivyonunuliwa na Serikali
hivi karibuni kwa ajili ya kuendesha kituo hicho cha televisheni itakuwa ni
jambo la busara ikienda sambamba na uwepo wa mafundi wataalamu katika Shirika
hilo.
Rais Dk. Shein alisema
kwamba miongoni mwa sekta ambazo Jamhuri ya Korea imekuwa ikiiunga mkono
Zanzibar katika kuziimarisha hapa nchini ni pamoja na sekta ya kilimo, hasa
kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa tokea Jamhuri ya Korea kuanza ushirikiano na uhusiano wa Kidiplomasia kati
yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar mnamo mwaka 1992,
imeweza kuisaidia kwa kiasi kikubwa Zanzibar katika kuendeleza sekta za
maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, uvuvi na nyenginezo.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Korea imeweza kusaidia katika ujenzi wa
skuli ya kisasa ya Sekondari ya Kwarara ambayo pia, ina studio ya matangazo
pamoja na vifaa mbali mbali vya habari kwa ajili ya mafunzo na utoaji elimu kwa
wananchi.
Aliongeza kuwa Jamhuri
ya Korea pia, imeweza kusaidia uanzishaji wa Kituo cha kutotolea vifaranga vya
samaki wakiemo kaa na majongoo ya baharini kilichopo Beit el Ras ikiwa ni
jitihada za kuhakikisha sekta ya uvuvi na ufugaji vinaimarika sambamba na
kupanua soko la ajira kwa vijana.
Rais Dk. Shein pia,
aliipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya
Zanzibar kwa kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika mikakati yake ya kupambana na umasikini pamoja na kutekeleza Dira ya Maendeleo
ya Zanzibar ya 2020.
Nae Balozi Balozi wa
Jamhuri ya Korea nchini Tanzania CHO Taeick
aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais
Dk. Shein kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kidugu kati ya pande mbili hizo.
Balozi huyo wa Jamhuri
ya Korea alizipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuendelea
kuviweka vizuri vivutio vya kitalii sambamba na mazingira ya Zanzibar ili yaweze
kuwavutia wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar.
Alieleza kuwa ni jambo
la faraja iwapo mashirikiano yataimarishwa zaidi kati ya pande mbili hizo hasa
katika sekta ya utalii kwani Zanzibar ina vivutio vingi vya kitalii na watu wa
Korea wanapenda kuja kuviona.
Balozi huyo
alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Korea iko tayari kuiunga mkono
Zanzibar katika kuhakikisha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) Televisheni
linapata mafundi wataalamu kwa ajili ya kuliendesha Shirika hilo ili liendeleze
ubora wake.
“Jamhuri ya Korea iko
tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuwapata mafunzi wataalamu kwani kuna
methali isemayo samaki mkunje angali mbichi na pia, kuna nyengine isemayo mbuyu
ulianza kama mchicha hivyo ni vyema vijana wakapata mafunzo ili waje kuwa
wataalamu wa Shirika hilo”,alisisitiza Balozi CHO Taeick
Aidha, Balozi CHO
Taeick alimueleza Rais Dk. Shein kwamba Jamhuri ya Korea itahakikisha miradi
yote iliyoahidi inatekelezwa vyema tena kwa wakati ukiwemo mradi wa kilimo cha
mpunga wa umwagiliaji maji.
Sambamba na hayo,
Balozi CHO Taeick alimueleza Rais Dk. Shein kwamba mashirika ya Jamhuri ya
Korea likiwemo Shirika la Maendeleo la Jamhuri ya Korea (KOICA) litaendelea
kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Pia, Balozi huyo alieleza
kuwa kupitia programu ya Kijamii ya Jamhuri ya Korea (SAMAUL) imewawezesha wananchi wa kijiji cha Cheju na
Kibokwa kunufaika na mradi wa skuli ya awali, mafunzo ya amali yakiwemo kilimo
cha mpunga, mboga na ufugaji.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment