Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Akizungumza na Wafanyakazi wa ZBC leo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar.(ZBC TV) mkutano uliofanyika ukumbi wa Kituo cha ZBC TV mnazi mmoja Zanzibar, kulia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Ndg. Chande Omar na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi.Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleze azma ya Serikali ya kuliimarisha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), pamoja na kuzingatia maslahi mazuri ya wafanyakazi wake.

Dk. Shein amesema hayo wakati alipokutana na Uongozi na wafanyakazi wa Shirika hilo, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Shirika hilo uliopo Mnazimmoja mjini hapa.

Alisema ZBC ni shirika jipya lililoundwa miaka sita iliyopita, hivyo aliwataka wafanyakazi kufahamu ulazima wa kuwepo kwa changamoto mbali mbali katika kipindi hiki  kuelekea hatua ya mafanikio.

Alisema Serikali imelazimika kutumia fedha nyingi katika uundaji wa Shirika hilo na kulipatia mitambo mipya ili liweze kuondokana na matumizi ya mfumo wa Analojia kuelekea ule wa  Digitali.

“Kuunda Shirika sio jambo dogo ni jambo linalohitaji fedha nyingi sana ilikuwa lazima tuunde na kufanyakazi, miaka sita haitoshi kupata chombo madhubuti”, alisema.

Aidha, alisema kuna umuhimu kwa shirika hilo kujiendesha wenyewe, jambo alilobainisha kuwa bado halijafanikiwa kwa kuwa linategemea ruzuku kutoka Serikalini.

Alieleza kuwa Wizara ya Habari, Utalii  na mambo ya Kale ina dhima ya kuongoza kuelekea mabadiliko ya shirika hilo, akibainisha umuhimu wa kuwepo mipango ya jumla kwa ajili ya ZBC ya kesho, huku akisitiza kuwa jambo hilo sio la mkato.

Dk. Shein alilitaka Shirika hilo kupitia Wizara kuainisha vipaumbele katika bajeti yake, kulingana na mahitaji yaliopo na kusisistiza azma ya serikali ya kuliendeleza shirika hilo kwa kulipatia vifaa vyote vinavyohitajika,

“Kupanga na kuchaguwa ni lazima muainishe mambo gani ya msingi mnataka kununuwa”, alisema.

Alieleza kuwa Serikali ina nia njema ya kuliendeleza shirika hilo ili lifanane na mashirika mbali mbali duniani, na ndio maana juhudi mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa kuliimarisha.

Alisema muundo wa Shirika hilo unapaswa kuwiana na ule wa Wizara ili kuwepo mustakbali mwema katika uendeshaji wake,chini ya usimamizi wa Bodi ya Shirika.

Aidha,  alisistiza mashirikiano, mapenzi na mshikamano katika utendaji wa kazi, huku akiwaaahidi wafanayakazi  hao kuimarishwa maslahi na stahiki zao mbali mbali kupitia Bodi ya Shirika hilo.

Alisema ZBC ni sawa an televisheni nyengine Duniani zinazomilikiwa na Seriklai na kubainisha tofauti iliyopo kati yake ni uwezo, huku akielezea mwelekeo wa shirika hilo kwua wa mafanikio.

“Naithamini sana ZBC, nawathamini wafanyakazi, natamani Serikali iwe na uwezo mkubwa tufanye yote, lakini nataka mtuamini tunataka kuleta mabadiliko”, alisema.

Katika hatua nyengine Dk. Shein slisema ni umuhimu kuhakikisha wafanyakazi wanaojitolea katika shirika hilo kwa kipindi kirefu kupatiwa ajira kwa kuzingatia kuwa wametumia miaka mingi kulitumikia kwa ufanisi.

Ameutaka uongozi wa  ZBC, kuwasilisha Serikalini taarifa za wafanyakazi 16 ambao wamekuwepo katika shirika hilo kwa kipindi cha kujitoleya , ili hatua za kuwapatia ajira ziweze kuchukuliwa.

Alisema suala la ajira kwa wafanyakazi wanaojitolea ni la kiutawala, ambapo tayari Serikali  ililitoleya muongozo muda mrefu uliiopita.

Dk. Shein alipongeza utaratibu ulioanzishwa na uongozi wa ZBC kuwakutanisha pamoja Viongozi na wafanyakazi kila mwezi ili waweze kuwasilisha matatizo yao kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi.

Aliwataka wafanyaakzi kufanya juhudi kuvutia sekta ya Utalii kwa kuutangaza katika vyombo vya habari (Tv na Redio), sambamba na kutaka kuwepo mashirikano ya karibu na Uongozi wa Wizara husika.

Aidha, aliutaka Uongozi wa Shirika hilo kuweka mazingira bora ya kuvutia wafanyakazi wao ili waweze  kuipenda kazi yao na kufanyakazi kwa bidii, huku akitowa pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na wafanayakazi wa shirika hilo, kiasi cha kuvutia watazamaji wengi.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema serikali itazingatia kwa makini usalama wa wafanyakazi wa shriika hilo katika matukio makubwa, ikiwemo wakati wa Uchaguzi mkuu.

Aliwataka wafanyakazi hao kufanyakazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi za uandishi wa habari na kuondokana na utartibu wa kuegemea upande mmoja pale inapoibuka hoja inayoyoihusus Serikali, ili kuepuka kuigawa.

Aidha,  alisistiza mashirikiano, mapenzi na mshikamano katika utendaji wa kazi, huku akiwaaahidi wafanayakazi  hao kuimarishwa maslahi na stahiki zao mbali mbali kupitia Bodi ya Shirika hilo.

“Naithamini sana ZBC, nawathamini wafanyakazi, natamani Serikali iwe na uwezo mkubwa tufanye yote, lakini nataka mtuamini tunataka kuleta mabadiliko”, alisema.

Mapema, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema suala la ajira kwa wafanyakazi waliojitolea siku nyingi, lina uwezekano mkubwa wa kupatikana ufumbuzi wake pale uongozi wa shirika hilo utakapowasilisha serikalini taarifa na jinsi litakavyoweza kuwalipa mishahara wafanyakazi hao.

“Kama kuna wafanyakazi wanajitolea na kama fedha zipo, niandikieni mimi nitatowa kibali cha kuajiriwa”, alisema.

Aliutaka uongozi wa shirika hilo kujiendesha kwa kuzingatia vipaumbele vinavyohitajika kwa ukufuata taratibu wa kuzishirikisha maeneo yote ya kazi ya Shirika hilo.

Alisistiza umuhimu wa kuwepo mpango maalum wa mafunzo kwa watumishi wa shirika hilo kwa mwaka, kuambatana na mahitaji halisi ya taasisi.

Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, Abdulhamid alisema serikali imetowa muongozo kwa kila Shirika kuwa na daraja lake, akibainisha kuwa mashrika yote yanayojitregemea tayari yameanza kutumia miongozo ya kimaslahi yaliowekwa na serikali.

Kuhusiana na uendaji wa likizo ya kila mwaka kwa wafanyakazi, alisema likizo ni haki ya mfanyakazi na kufafanua kuwa Posho la mazingira magumu halina uhusiano na posho la malipo ya ziada ya kazi (over time), huku akiwataka viongozi wa taasisi kuratibu vyema upatikanaji w ‘overtime’ili kuepuka ujanja unaofanywa na baadhi ya wafanyaakazi wa kutega kazi ili kupata posho hilo

Aliwataka wafanyakazi kuwa watundu katika kutafuta fursa za masomo  katika taasisi na vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, aliutaka uongozi wa Shirika hilo kuibuwa mahitaji ya kitaalamu kupitia kada tofauti na kuyawasilisha Serikali ili yaweze kuwasilishwa katika Idara ya Elimu ya juu kwa utekelezaji.

Dk. Abdulhamid aliitaka Menejment ya ZBC kulipatia ufumbuzi suala la usafiri wa wafanyakazi ili waweze kuondokana na kadhia ya kukosa usafiri wa kuwafikisha na kuwarudisha kazini , hatua aliyosema itawajengea heshima na kuwahakikishia usalama wao.

Aliikumbusha Idara ya Habari na Maelezo wajibu wa kuwataka Mawaziri kutekeleza muongozo wa kutoa taarifa za utekelezaji wa Wizara zao kila baada ya miezi mitatu, sambamba na kusisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kutafuta habari na kuondokana na urasimu wakati huu wa ushindani.

Aidha, alieleza umuhimu wa wafanyakazi wa Shirika hilo kufanyakazi kwa mashirkiano na kuweka utaifa mbele kwa kufuata sera na miongozo ya Serikali na sheria za Utumishi wa umma pamoja na kuondokana na makundi.

Nae, Waziri wa Habari, Utalii na Mmabo ya Kale, Mahamoud Thabiti Kombo alisema atasimamia kikamilifu kuhakikisha wafanyaakzi wanaojitolea kipindi kirefu wanaajiriwa awamu kwa awamu pamoja na wale wenye ulemavu.

Aidha, alisema kuna mashirikiano ya kutosha kati ya Uongozi wa Wizara hiyo na wafanyakazi wa ZBC, sambamba na kuuutaka uongozi wa Shirika hilo kufanya juhudi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Kampuni ya Azam TV  kwa maslahi ya wafanyakazi,Shirika na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Chande Omar, aliahidi kufanya juhudi kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazolikabili Shirika hilo, ikiwemo suala la ajira , mafunzo na usafiri.

Alisema suala la mafunzo linakwenda kwa kasi kubwa, akibainisha hatua mbali mbali zinazochukuliwa kulingana na Bajeti iliyopo.

Alisema kuna mwamko mkubwa kwa wafanyakazi kupenda kusoma, hivyo Uongozi wa ZBC unafanya juhudi ya  kuwapatia fursa za mafunzo katika taasisi mbali mbali nchini pamoja na kupokea wataalamu kutoka nje ya nchi kuendesha mafunzo mbalimbali, ikiwemo uzalishaji wa vipindi.

 Katika mkutano huo, ambapo pia uliwashirikia viongozi mbali mbali wa serikali, ikiwemo Washauri wa Rais,    wafanyakazi walipata fursa ya kutoa maoni, mapendekezo na ushauri kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika maeneo mbali mbali, ikiwemo ajira, mafunzo, usafiri, usalama na usafiri.   

   
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
E-mail: abdya062@gmail.com


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.