Habari za Punde

Zanzibar Itaendelea Kushirikiana na Wawekezaji Katika Usafiri wa Uhakika wa Baharini Kufanya Safari za Kila Siku.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Boti ya Kisasa ya Kampuni ya Azam Marine na Kilimanjaro Fast Ferries ya Kilimanjaro VII,uliofanyika katika eneo ,la Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar (kulia kwa Rais) Mwenyekiti wa Makampuni ya Kilimanjaro Fast Ferries na Azam Marine.Ndg. Said Salim Bakhressa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar.Mhe.Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika kuhakikisha kunakuwa na usafiri wa uhakika wa baharini ili kuweza kufanya safari za kila siku kati ya visiwa vya Zanzibar na Tanzania Bara pamoja na nchi za jirani.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo katika sherehe za uzinduzi wa boti mpya ya Kilimanjaro VII zilizofanyika huko katika eneo la Hoteli ya Verde Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa usafiri wa baharini ndio ulioipelekea Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara na hatimae kuwa sehemu mashuhuri duniani kote hadi hivi sasa kwani bahari ina historia kubwa katika maendeleo ya visiwa vya Zanzibar na watu wake.

Aliongeza kuwa ni jambo la kufurahisha kuona kwamba juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha huduma za usafiri wa baharini zinakwenda sambamba na juhudi zinazochukuliwa na sekta binafsi katika suala hilo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendelea na juhudi zake katika kuwawezesha na kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji wazalendo wanaotaka kuwekeza katika miradi mbali mbali hapa nchini sambamba na kuongeza fursa zilizopo ili kumuwezesha kila mwananchi kuzitumia fursa hizo kwa kutegemea uwezo wake.

Alieleza kuwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi ambayo inajumuisha wawekezaji wazalendo na wageni ni suala lililopewa umuhimu mkubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba.

Alisisitiza kwamba ushirikiano huo vile vile, umeelezwa bayana katika mipango mikuu ya Maendeleo ambapo Ibara ya 69 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ina bainisha dhamira ya kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wawekezaji.

Alitoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kwa kushirikiana vizuri na Kampuni ya “ Kilimanjaro Fast Ferries” katika kukamilisha hatua na taratibu zinazohitajika kufuatwa hadi chombo hicho kikanunuliwa, kikasafirishwa kuja nchini, kikasajiliwa hadi kuzinduliwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa Sheikh Said Salim Bakhresa  na wawekezaji wote wazalendo waliowekeza katika sekta ya usafiri wa bahari huku akisisitiza kuwa Serikali inaziona juhudi zao hizo na inazithamini.

Rais Dk. Shein alimpongeza muwekezaji huyo mzalendo kwa imani, upendo na uzalendo wake kwa Zanzibar na wananchi wenzake na kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa miradi mikubwa na yenye tija katika sekta mbali mbali.

Aliongeza kuwa Sheikh Said Salim Bakhresa ameonyesha njia na kufungua milango katika utekelezaji wa mipago ya kuimarisha na kuyaendeleza maeneo huru,kuendeleza viwanda,ujenzi wa miundombinu pamoja na usafirishaji.

Dk. Shein alisema kuwa Mfanyabiashara huyo Mzalendo kupitia miradi mbali mbali anayoiendesha amekuwa akirejesha faida kwa jamii kwa kuimarisha elimu kwa kutoa michango kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa ya skuli za Sekondari kwa kushirikiana na Serikali.

Kadhalika, alieleza kuwa miradi ya Sheikh Bakhresa imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara, usalama wa chakula pamoja na kuendeleza sekta ya utalii.

“Bila ya shaka, Sheikh Said Salim Bakhresa na wafanyabiashra wengine wana nafasi muhimu katika historia ya maendeleo ya Zanzibar kwani mambo wanayoyafanya yatakumbukwa na vizazi vijavyo kwa miaka mingi hapo baadae”, alisema Dk. Sheikh.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa upande mwengine ununuzi wa vyombo vya usafiri vya baharini unaofanywa na Serikali pamoja na wawekezaji wazalendo ni hatua muhimu katika kuendeleza uchumi wa bahari pamoja na sekta ya utalii, usafirishaji na biashara.

Alieleza kuwa sekta ya utalii hivi sasa ndio muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar na imekuwa ikikua kwa kasi sana na tayari imeshapindukia lengo lililowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 la kupokea watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020.

Alisema kuwa mwaka jana 2018 idadi ya watalii ilifika 520,809 na matumaini yake kwamba idadi hiyo itaongezeka  kwa mwaka huu wa 2019 na anatarajia ifikapo mwaka 2020 huenda idadi hiyo ikafikia watalii 600,000.

Rais Dk. Shein, alizitaka taasisi za Serikali zinazoshughulikia sekta ya utalii kuhakikisha zinakaa pamoja na kutafakari namna ya kasi ya ukuaji wa utalii iende sambamba na kasi ya uwekezaji katika sekta hiyo ili kuhakikisha Zanzibar haiachwi nyuma katika maendeleo ya sketa ya utalii hivi sasa duniani.

Pia, aliwataka wale wote waliobahatika kuajiriwa katika boti hiyo mpya na vyombo mbali mbali vya baharini, kuwa makini katika kufuata sheria na kanuni za usalama wa chombo na abiria.

Alieleza jinsi alivyofurahishwa na mambo mazuri aliyoyaona katika boti hiyo ya kisasa kwa viwango na vigezo vilivyowekwa ambapo teknolojia ya hali ya juu imetumika katika ujenzi wa boti hiyo katika mifumo ya injini, viti,mipangilio ya utoaji wa huduma pamoja na usalama wa boti yenyewe na abiria huku akieleza umuhimu wa kuingizwa vyombo vipya na vyenye hadhi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza jinsi Serikali ilivyodhamiria kununua boti ndogo tano 5, za kusafirisha abiria katika visiwa vidogo vidogo vya Unguja na Pemba, hatua iliyolenga kuondoa changamoto mbali mbali wanazozipata wananchi wanaoishi katika visiwa vidogo vidogo.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alimpongeza Sheikh Said Salim Bakhresa kwa uthubutu wake, ubunifu, ujasiri na uzalendo alionao na kueleza kuwa Wizara anayoiongoza imevutiwa na uzalendo wake huo.

Balozi Ramia alieleza mipango na mikakati iliyowekwa na Wizara yake ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia njia za elektroniki katika usajili wa miradi huku akieleza Sheria na Sera zilizowekwa na Serikali katika kuimarisha miradi kupitia Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).

Mapema taarifa kutoka kwa mmiliki wa mradi huo iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji Abubakar Aziz Salim  kutoka Kampuni ya “Kilimanjaro Fast Ferries pamoja na “Azam Marine” alisema kuwa Kampuni hizo zimetoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya wafanyakazi 400 na kusafirisha abiria wapatao Milioni mbili kwa mwaka baina ya Zanzibar na Tanzania Bara wakiwemo raia wa kigeni laki moja na themanini elfu.

Alieleza kuwa hiyo ni wastani wa abiria 5000 wanaohudumiwa kwa siku moja ambapo wana uwezo wa kusafirisha abiria mpaka 9000 kwa siku.

Alisisitiza kuwa Kampuni hizo zinachangia pato la taifa kwa kulipa kodi na tozo mbali mbali ambapo tokea mwaka 2010 hadi hivi leo zimechangia kwa kulipa tozo la kodi mbali mbali kwa jumla ya TZS Bilioni 93.

Aidha, alieleza kuwa chombo hicho kimejengwa kwa muda wa miezi 18 huko mjini Hobart nchini Australia ambacho ni cha kisasa chenye uwezo wa kubeba abiria 510, chenye tabaka nne ambazo ni Economy abiria (202), Economy Premium abiria (218), VIP abiria (72) na Royal abiria (18).

Sambamba na hayo, alieleza kuwa boti hiyo ina sifa mbili kubwa za kipekee na za kidunia ikiwemo injini za kisasa mbili aina ya ‘Cummins zenye ‘Horsepower’ 7,200 pamoja na ‘Rolls Royce Jet’ yenye uwezo wa kwenda kasi ya ‘knots’ 39.

Vile vile, ni boti ya kwanza na pekee duniani yenye aina ya viti vilivyopo katika daraja la Royal ambapo pia, ni meli yenye vifaa na muundo maalum ambao unaiwezesha kuhimili mchafuko wa bahari wakati wa upepo mkali kwa wimbi hadi metre 4.5.

Wasanii mbali mbali wakiongozwa na msanii mahiri Makombora na kikundi chake cha  ‘Makombora Art Group’ walitumbuiza katika sherehe hiyo ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya siasa, wawekezaji pamoja na wananchi.  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.