Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwapongeza Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes kwa kuiwakilisha vizuri Zanzibar katika michuano ya Chalenji kwa mwaka 2019 yaliofanyika Nchini Uganda, (kulia kwa Rais) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, Jaji Mkuu wa Zanzibar.Mhe Omar Othman Makungu na Waziri wa Vijana Michezo Sanaa na Utamaduni Mhe.Balozi Ali Karume, wakijumuika na Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar katika chakula Maalum kilichofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa wachezaji wa timu ya “Zanzibar Heroes” na
viongozi wao kwa kuweza kuiwakilisha kwa nidhamu ya hali ya juu Zanzibar katika
mashindano ya Chalenji ya mwaka 2019 na kutoa upinzani mkubwa kwa timu zote
waliocheza nazo.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar katika hafla ya chakula cha mchana
alichowaandalia wachezaji wa timu ya “Zanzibar Heroes” ambao wameshiriki
mashindano ya Chalenji ya mwaka huu wa 2019 huko nchini Uganda pamoja na kuwapa
zawadi ya fedha taslim.
Akisoma hotuba kwa
niaba ya Rais Dk. Shein, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Issa Ussi Haji Gavu alisema kuwa hata hivyo kwa mara hii bahati
haikuwa kwa upande wa “Zanzibar Heroes” kama ilivyokuwa mwaka jana lakini timu
hiyo imeendelea kuwa tishio katika mashindano hayo.
“Tumepoteza mechi
mbili kwa kufungwa bao moja kwa kila mechi na tumetoka sare mechi moja,.nawapongeza
wachezaji wote mcheza kwao hutunzwa
hapigwi”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa “Zanzibar Heroes” imeonesha upinzani na ufundi wa hali ya juu
lakini kwenye mpira wataalamu wanasema kwamba kosa moja dogo linaweza
kukugharimu “One mistake One goal”.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa wananchi wote wa Zanzibar wanahisi maumivu na machungu ya kupoteza mechi
hizo kama vile wanavyohisi wao wachezaji wa “Zanzibar Heroes”.
Alitoa pongezi kwa
wananchi wote wa Zanzibar kwa hamasa waliyoionesha na kwa kuiunga mkono timu
hiyo wakati wote wa mashindano hadi hivi sasa “Baraza zote zilijaa washabiki na
wapenzi wakiwa na simanzi wakati mlipokuwa mkicheza”,alisisitiza Rais Dk.
Shein.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwapongeza wachezaji hao kwa kuiwakilisha Zanzibar kwa heshima na
nidhamu ya hali ya juu jambo ambalo limelinda sifa ya watu wa Zanzibar.
Akimnukuu Rais wa 13
wa Marekani, Marehemu Millar Fillmore ambaye alisema kuwa ‘kushindwa ikiwa bado
umelinda heshima yako ni bora kuliko kupata ushindi baada ya kuvunja heshima
yako’.
“Tunakupongezeni
wachezaji wetu wa “Zanzibar Heroes” kwa kuendelea kutuwakilisha mkiwa na
heshima kubwa na kulinda sifa njema za watu wa Zanzibar kupitia mashindano
mnayotuwakilisha”,alisema Dk. Shein.
Rais Dk. Shein
alieleza kuwa yeye anamatumaini makubwa na ubora wa timu ya “Zanzibar Heroes”
pamoja na viongozi na Mwalimu wa timu hiyo Hemed Suleiman Moroco na ndio maana
kwa mara nyengine ameamua kuwaalika
Ikulu ili wafarajike na kupata chakula cha mchana pamoja.
Alieleza kuwa Serikali
inathamini jithada za watu wote walioisaidia timu hiyo tangu hatua za
maandalizi hadi kuiwezesha kushiriki mashindano ya mwaka huu wa 2019 huko
nchini Uganda.
Akitoa nasaha zake
Rais Dk. Shein alisema kuwa kila mmoja anapaswa kuendeleza umoja na
kushirikiana zaidi katika kuisaidia timu ya Taifa ya Zanzibar, “Zanzibar
Heroes” na timu zote zinazoshiriki katika michezo ya Kitaifa na Kimataifa.
Rais Dk. Shein
alisisitiza haja ya kuendelea kupeana moyo na kuzingatia wapi timu imejikwaa
iwe kwenye maandalizi ya timu au katika mbinu za kutafuta ushindi na mambo
mengine yote ambayo yatawezesha kufanya vizuri hapo baadae.
Pamoja na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuimarisha sekta ya
michezo ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya michezo hapa Zanzibar.
Nae Kocha Mkuu wa
“Zanzibar Heroes” Hemed Suleiman Moroco alieleza kuwa Rais Dk. Shein ameonesha
ujasiri na amewapa nguvu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuahidi
kufanikisha ahadi yake ya kuiletea ushindi Zanzibar katika mashindano yajayo.
Alimpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuendelea kuwapa nguvu na amekuwa na mchango mkubwa katika timu hiyo tokea
wakiwa kambini mpaka wakati wakiendelea na mashindano hayo na kupelekea
kuwavutia watu wengi wakati wakiwa Uganda.
Kocha Moroco alitumia
fursa hiyo kutoa maombi yake kwa Serikali katika kuhakikisha timu ya “Zanzibar
Heroes” inapata maandalizi mazuri wakati wote na iwe ikishiriki mashindano
mbali mbali ya kirafiki ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema kuwa
katika maandalizi mazuri ya timu hiyo ipo haja ya kushiriki mashindano mbali
mbali yakiwemo mashidano ya nchi za visiwa huku akisisitiza kuwa Zanzibar bado mpira
unaendelea vyema.
Alimpongeza Rais Dk.
Shein kwa kuwaandalia chakula hicho cha mchana hapo Ikulu na kueleza kuwa
wanathamini jitihada za Rais wa Zanzibar
katika kuiendeleza na kuikuza sekta ya michezo hapa nchini.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment