Habari za Punde

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTEKELEZA MKAKATI WA TAIFADHIDI YA RUSHWA ILI KUBORESHA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)akiteta jambo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) kabla ya kufungua Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Dkt. Moses Kusiluka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)akifungua Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)(katikati mstari wa mbele) na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (wa tatu kutoka kulia mstari wa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Umma, baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.

Na.Happiness Shayo – Dodoma
Taasisi za Umma nchini zimetakiwa kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpangokazi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila taasisi inakuwa na Kamati ya Kusimamia Uadilifu ili kudhibiti vitendo vya rushwa na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati akifungua kongamano la kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu katika ukumbi wa Pius Msekwa Bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Mkuchika amesema utekelezaji wa Mkakati huo umejikita kwenye sekta za kimkakati zikiwemo za Manunuzi ya Umma, Ukusanyaji wa Mapato, Utoaji wa Haki, Maliasili na Utalii, Madini, Nishati, Mafuta na Gesi, Afya, Elimu na Ardhi ambapo mkakati huo unatekelezwa catlike ngazi za Kijiji/Mtaa, Kata, Tarafa, Wilaya, MkoanaTaifa.

‘‘Kila taasisi inatakiwa kuwa na Kamati ya Kusimamia Uadilifu ili kuweza kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mkakati wa taifa dhidi ya rushwa’’,Mhe.  Mkuchika amesisitiza.

Mhe, Mkuchika ameongeza kuwa,malengo makuu ya mkakati huo ni kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa utoaji huduma catlike sekta za Umma na sekta Binafsi, ufanisi catlike utekelezaji wa mikakati ya mapambano dhidi ya rushwa, kuzijengea uwezo taasisi simamizi za masuala ya Utawala Bora na kuwa na Uongozi wa Kisiasa madhubuti unaoshiriki kwa dhati catlike mapambano dhidi ya rushwa.

Mhe. Mkuchika amesema, Mkakati huo wa Taifa Dhidi ya Rushwa ulizinduliwa rasmi tarehe 10 Desemba, 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Mendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Bw. Paul Wilson Mlemya amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji nguvu ya pamoja kati ya serikali na wananchi ili kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

“Rasilimali nyingi zinazopotea katika njia za rushwa zikiweza kuzuiliwa zitaleta maendeleo kwa wananchi katika sekta za elimu, afya na miundombinu kwa ujumla wake ” Bw. Mlemya amesisitiza.

Kwa upande wake, Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Mhe. Jaji (Mst.) Harold R. Nsekela amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za  Binadamu ni muhimu kwa sababu yanatoa fursa kwa Taifa kujitathmini kama limefanya juhudi za kutosha katika kuhakikisha maadili yanazingatiwa, vitendo vya rushwa vimepungua, uwajibikaji umeongezeka na misingi ya Utawala Bora inazingatiwa.

Kongamano la Siku ya Maadili na Haki za Binadamu hufanyika Desemba 10 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu, limehudhuriwa na Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Taasisi za Serikali, Viongozi wa Serikali Wastaafu na Watumishiwa Umma kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.