Habari za Punde

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YAAHIDI KUFANYIA KAZI MAPENDEKEZO YA WANAMIPANGO

Kamishana Msaidizi wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akichangia mada zilizokuwa zikiendelea katika Kongamano la Wanamipango lililofanyika katika Ukumbi wa Kambarage, wizarani hapo, Jijini Dodoma.
Na Farida Ramadhani na Saidina MsangiWFM, Dodoma
Wizara ya Fedha na Mipango imeahidi kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu wa mipango ili kuboresha usimamizi wa sera na mipango ya maendeleo ya nchi.
Hayo yameelezwa na Kamshina wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. William Mhoja wakati wa kuhitimisha kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2019 lililofanyika Jijini Dodoma.
Bw. Mhoja alisema kuwa kongamano hilo limetoa mapendekezo muhimu ambayo yatasaidia kuboresha upangaji na utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali ya maendeleo nchini.
Aliwashukuru washiriki wote kwa michango, mawazo na fikra pevu wakati wa kongamano ambayo itasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu taaluma ya mipango.
Naye Mchumi Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Adam Msumule ,ambaye ni miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo amepongeza waandaaji wa kongamano hilo muhimu kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kuboresha mipango ya nchi.
Bw. Msumule alishauri kongamano hilo kufanyika kila mwaka ili kutoa fursa kwa wataalamu kufanya tathmnini ya mipango iliyopo, iliyotekelezwa na kuona namna ya kuiboresha.
Kongamano hilo lililokuwa na kauli mbiu ugharamiaji wa maendeleo, lilitoa fursa kwa washiriki kujadili mawasilisho mbalimbali ikiwemo vyanzo bunifu vya ugharamiaji mipango ya maendeleo ya Taifa, Sera, Sheria na mfumo wa kitaasisi unaosimamia ugharamiaji wa maendeleo nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.