Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Apokea Matembezi ya Tamasha la Mazoezi la Viungo la Kitaifa Zanzibar Uwanja wa Mao Zedong Jijini Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akiwapungia mkono Washiriki wa Mazoezi ya Viungo Zanzibar wakiingia katika Uwanja wa Mao Zedong kumalizia matembezi hayo na kufanya mazoezi ya Viungu katika Uwanja huo. 

KUADHIMISHA Siku ya Mazoezi ya Viungo Kitaifa katika mwezi wa Januari kila mwaka ni kielelezo muhimu katika historia ya ukombozi wa wananchi wa Zanzibar ambao walikandamizwa kwa miongo mingi na wakoloni.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  
aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa Mao Dzedong katika Tamasha la Siku ya Mazoezi Kitaifa baada ya kuongoza matembezi yaliyoanzia katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi la zamani kuelekea Mkunazini, Kariakoo, Magereza, Kilimani na kumalizikia katika uwanja huo wa Mao.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein ambaye pia, ni muasisi wa Tamasha hilo alisema kwamba maadhimisho hayo huwa yanaufungua mwaka mpya, tukio ambalo linashabihiana na ufunguzi wa ukurasa mpya katika utawala wa wanyonge hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa  mazoezi hayo yanafanyika mwanzoni mwa mwezi wa Januari ambao ndio mwezi wa heka heka na harakati za kuung’oa utawala wa kikoloni hapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa katika Mapinduzi hayo matukufu ya Januari 12, 1964 wananchi hawakuwa na silaha za kisasa kwa ajili ya mapambano, bali walikuwa na ari, uzalendo, hamu ya kujikomboa na kuiongoza nchi yao wenyewe.

Hivyo, alisisitiza kuwa inapoadhimishwa siku ya mazoezi ya viungo  kila mwaka katika mwezi huu wa Januari ni wajibu wa kila mmoja kutafakari umuhimu wa maadhimisho hayo kwa mnasaba wa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo yaliteta ukombozi, haki na usawa kwa wananchi wote.

“Mazoezi ya viungo ni kama chumvi katika chakula , maana chumvi ni kiungo muhimu kwenye chakula kwa kila chakula kinachopaswa kutiwa chumvi na ndio maana waimbaji wakaisifu chumvi”, alisisitiza Rais Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa sekta ya michezo hapa nchini imejenga historia kubwa katika harakati za kisiasa kuelekea Mapinduzi matukufu ya Januari 1964 ambayo yaliandaliwa na kufanywa na Chama Cha Afro Shirazi (ASP) ambacho kilitokana na Chama cha “African Association” na “Shirazi Association” ambapo “African Association” kilikuwa ni matokeo ya klabu ya michezo ya vijana wa Kiafrika.

Alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa michezo kwa maendeleo ya Zanzibar, Awamu zote Saba za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanya jitihada mbali mbali za kuimarisha sekta ya michezo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya michezo hasa viwanja vya michezo.

Aidha, alisema Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020, imeielekeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuufanyia marekebisho makubwa uwanja wa Mao Dzedong jambo ambalo limeshatekelezwa kwa mafanikio pamoja na kujenga viwanja vitano vya michezo katika kila Wilaya.

Rais Dk. Shein alitoa wito kwa Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, wazidi kushirikiana katika kuufanikisha utekelezaji wa mpango maalum wa kuendeleza michezo yaani “Sport 55” ili kufikia lengo la kuirejesha hadhi Zanzibar ya kufanya vyema katika michezo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Dk. Shein aliwanasihi wananchi wote waendelee kuithamini timu ya Taifa ya Zanzibar, “Zanzibar Heroes” na kuipa moyo na kwa pamoja kuzingatia wapi kumefanyika kosa tangu mwanzo wa matayarisho hadi katika mashindano yenyewe ili kuweza kutafuta mbinu na njia za kufanya marekebisho kwa lengo la kufanya vizuri zaidi.

Aliongeza kuwa wachezaji wa Timu hiyo ambao aliwaalika Ikulu mnamo Disemba 17, mwaka jana 2019, katika hafla ya chakula cha mchana alichowaandalia walistahiki kupongezwa kwa kuonesha upinzani na ufundi wa hali ya juu katika mchezo kiasi ya kwamba waliendelea kuwa tishio kwa timu nyengine.

Alisisitiza na kutoa wito kwa viongozi wa ZFF na BMZ waanze maandalizi ya kuiandaa timu ya “Zanzibar Heroes” mapema kwa mfano wachezaji wajulikane na maandaliwe mapema na viongozi watakaosimamia kamati za ushindi nao wajulikane mapema.

Rais Dk. Shein alitoa wito kwa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Idara ya Watu wenye Ulemavu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wapange mkakati maalum wa kuwashirikisha Watu wenye Ulemavu katika michezo mbali mbali ambayo wanaimudu kutokana na hali zao za viwiliwili.

Rais Dk. Shein ameutoa wito huo kutokana na kuona kwamba katika jitihada za kukuza sekta ya michezo, bado hawajashirikishwa ipasavyo Watu wenye Ulemavu.

Hivyo, alisisitiza kwamba itakuwa ni jambo la busara na la kupendeza iwapo vijana wenye ulemavu watatayarishwa vizuri katika michezo wanaoimudu na kushirikishwa kuicheza katika Tamasha la Elimu bila Mapilipo au katika shamrashamra za maandhimisho ya Sherehe za Mapinduzi.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud alieleza azma ya Tamasha hilo na kusisitiza umuhimu wake katika kukuza umoja, ushirikiano na mshikamano sambamba na kuhuisha afya kwa wafanyaji wa mazoezi.

Nae Kamishna wa Michezo Zanzibar, Sharifa Khamis alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuliunga mkono Tamasha hilo sambamba na kuendelea kuiimarisha sekta ya michezo hapa nchini.

Nao wafanyamazoezi ya viungo katika risala yao iliyosomwa na Sihaba Mohamed walieleza jinsi walivyofarajika na uongozi wa Rais Dk. Shein na kumpongeza kwa dhati kwa kuijenga Zanzibar katika kipindi cha uongozi wake wa miaka 10 na kumuomba Mwenyezi Mungu amjaalie amalize salama muda wake wa Urais kwa uzima na afya.

Walieleza kuwa ni dhahiri kwamba Rais Dk. Shein ameitumikia Zanzibar ipasavyo na kwa moyo wake wote katika uhakikisha kwamba anailetea maendeleo katika nyanja ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hali ambayo kila mmoja anaiona.

Aidha, walieleza kuwa wao wanamazoezi amewawekea kumbukumbu ya kujivunia tangu alipolitangaza tamasha hilo kuwa la Kimataifa mwaka 2014 walipomualika kuwa Mgeni Rasmi kwenye Bonanza lao la lililofanyika huko katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu aendelee kukupa imani ya kuitumikia nchi yetu na tunakuomba hata pale utakapopumzika basi ibaki akilini mwako kuwa Tamasha hili bado ni lako na uendelee kujumuika nasi mwaka hadi mwaka”, walieleza wanamazoezi hao.

Rais Dk. Shein aliungana na wanamazoezi hao kwa kumshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Joseph Pombe Magufuli kwa kumteua Amina Talib ambaye ni Katibu wa (ZABESA), kuwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora.

Alisisitiza haja kwa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale pamoja na Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushierikiana pamoja kulitumia Tamasha la Utalii la Zanzibar ili kuingiza michezo ya riadha, kuogelea na resi za baiskeli ambayo anaamini kwamba watalii wataifurahia sana.

Wanamazoezi hao waliiomba Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Maendeleo ya Wanawake na Watoto kwa kushirikiana na Chama cha Mazoezi Zanzibar (ZABESA) kuandaa mpango wa kuwapatia taaluma ya ujasiriamali na mikopo ili waweze kujikwamua kimaisha.

Kwa maelezo ya wanamazoezi hao, ujumbe wa mwaka huu wa 2020 wa Tamasha hilo unalenga kwenye umuhimu wa mazoezi lakini pia, mikusanyiko yao hiyo iwaletee maendeleo kwa maana ya kwamba walenge pia, kujikwamua kiuchumi.

Sambamba na hayo, wanamazoezi hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuilinda na kuitunza amani na utulivu wa nchi sambamba na kuwaletea maendeleo makubwa ambayo leo hii wananchi wanajivunia.

Pia, walitumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la Bandari Zanzibar kwa kuendelea kuwasaidia kufanikisha Tamasha hilo na kumpongeza Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa kuwasidia kutokana na kuelewa umuhimu wa mazoezi na kuwapongeza wanamazoezi wa Unguja, Pemba na Tanzania Bara pamoja na wananchi wote kwa ushiriki wao.

Katika Tamasha hilo, Rais Dk. Shein alitoa vyeti maalum kwa washiriki wa Tamasha hilo kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara ambapo mapema wanamazoezi hao walipita mbele ya jukwa kuu alilokaa Rais huku wakionesha umahiri wao wa mazoezi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.