Habari za Punde

Rais Dk Shein ampongeza mtawala wa Ras Al KhaimahSTATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                12.01.2020
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi kwa kutuma mjumbe aliyemwakilisha katika sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dk. Shein alipongeza ujio wa Bwana Mohamed Ali Musabeh Al Nuaimi ambaye alifanya nae mazungumzo Ikulu ndogo Migombani na kusisitiza kuwa Zanzibar inathamni uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Ras Al Khaimah na kusema kuwa ujumbe huo unathibitisha ukweli huo.

Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo kuwa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar zimefana kwa kiasi kikubwa ambapo kabla ya kilele hulitanguliwa na shamrashamra za uzinduzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa katika miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar maendeleo makubwa yamefikiwa Unguja na Pemba huku akitumia fursa hiyo kuwaponegza wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki wka wingi katika kilele cha sherehe hizo zilizofanyika huko katika uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Nae Bwana Mohamed Ali Masabel Al Nuaimi alimpongeza Rais Dk. Shein pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa kusherehekea miaka 56 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar kwa aina yake na kutoa shukurani kwa mwaliko huo.

Kiongozi huyo alipongeza mapokezi makubwa aliyoyapata yeye na ujumbe wake huku akitumia fursa hiyo kupongeza maendeleo makubwa yaliopatikana hapa Zanzibar na kusisitiza kuwa Ras Al Khaimah itaendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Katika mazungumzo hayo kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Mtawala wa Ras-Al-Khaimah Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi anaungana na wananchi wote wa Zanzibar katika kusherehekea miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kiongozi huyo alifuatana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) nchini Tanzania  Khalifa Abdulrahman Almarzooqi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa RAK Gas Nishant Dighe.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.