Habari za Punde

Rais Mstaafu wa Kenya Daniel Arap Moi Afariki Dunia leo

Rais Mstaafu wa Kenya Daniel arap Moi afariki dunia akiwa na miaka 95, rais Uhuru Kenyatta athibitisha.
"Kwa masikitiko makubwa natangaza kifo cha kiongozi mkubwa Afrika, Daniel Toroitich arap Moi, rais wa pili wa Kenya. Raisi mstaafu amefariki katika Hospitali ya Nairobi mapema asubuhi ya leo Februari 4 akiwa na familia yake.
Msemaji wa Mzee Moi Lee Njiru pia ameongea na BBC Swahili punde tu taarifa hizo zilipochomoza na kabla ya Ikulu kutoa tamko.
"...alikuwa Nairobi Hospital ambapo alilazwa tarehe 10 mwezi wa kumi mwaka uliopita, hiyo ni zaidi ya miezi mitatu," bwana Njiru amesema.
Kwa mujibu wa Njiru mipango yote ya mazishi ipo chini ya jeshi la Kenya kwa kuwa Mzee Moi alikuwa amiri jeshi mstaafu wa nchi hiyo.
Runinga ya taifa ya Kenya (KBC), pamoja na vyombo binafsi vya Capital FM, Citizen TV na NTV vimeripoti taarifa hiyo ya msiba asubuhi ya leo Jumanne, Februari 4.
Mzee Moi alizaliwa Septemba 2, 1924 na alitawala Kenya kwa miaka 24 kutoka 1978 mpaka 2002.
Tangazo kutoka Ikulu limesema kuwa mzee Moi, hata baada ya kuondoka madarakani aliendelea kulitumikia taifa la Kenya na Afrika kwa kuwafundisha viongozi wa Kenya na nje ya Kenya, akiendelea kushiriki kwenye maendeleo ya miradi mbalimbali na kazi za misaada akiihubiri amani, upendo na umoja barani Afrika na duniani.
Mzee Moi aliiongoza Kenya kuelekea kurudisha mfumo wa vyama vingi na katika vipindi vingine vingi vya changamoto; na kumalizika kwa mchakato wa kukabidhi madaraka kwa amani mwezi Desemba mwaka 2002, wakati huo mchakato ambao ulikuwa nadra kufanyika Afrika, ambao uliweka mfano barani afrika na nje ya bara tangu wakati huo.
''Hiba yake inaishi Kenya hata leo. Filosofia ya Nyayo kuhusu 'amani, upendo na umoja' ilikuwa wimbo wake kipindi chake kama kiongozi wa nchi na serikali''. Ilieleza taarifa ya Ikulu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.