Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar, wakati akipokea taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 /2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na (kulia kwa Rais) Katibu Mkuu Jiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuna umuhimu wa kutizama upya
sheria zinazosimamia mwenendo wa usalama wa chakula nchini, ili kuondokana na
malalamiko mbali mbali ya wafanyabiashara.
Dk. Shein ametowa ufafanuzi huo, wakati akipokea taarifa ya
utekelezaji wa mpango kazi ya Wizara ya Afya, kwa kipindi cha kuanzia Julai
hadi Disemba, 2019, hafla iliyofanyika Ikulu mjini hapa.
Alisema kuna umuhimu kwa Uongozi wa Wizara hiyo kuziangalia upya
sheria zinazosimamia usalama wa chakula, hususan katika suala zima la ukaguzi wa
bidhaa zinazotoka na kuingia nchini, kwa kigezo cha kuwepo malalamiko kutoka kwa
wafanyabaishara juu ya tozo wanayolipa kugharamia ukaguzi huo.
Alisema wafanyabishara wamekuwa wakilalamikia gharama hizo, kwa
kigezo kuwa dhima ya kuthibitisha ubora wa bidhaa uko mikononi kwa Serikali badala ya wao
kubebeshwa mzigo huo.
Alisema pamoja na
sheria zilizopo kuwa na uwiano katika nchi nne za Afrika Mashariki, kuna
umuhimu wa kuzipitia upya kwa kuzingatia kuwa Serikali ndio yenye dhima katika
kufanya utafiti na kupata matokeo.
Dk. Shein alieleza wafanyabiashara wamekuwa wakilalamikia
kuwepo kwa utitiri wa taasisi za uchunguzi, jambo linaloongeza urasimu.
Alieleza kuwa mbali na taasisi hizo kuongozwa na sheria yake kila moja, kuna umuhimu wa viongozi
kukaa pamoja ili kuwa na mfumo maalum wa utoaji wa tozo moja.
Alisema Serikali haiwezi kupuuza malalamiko ya wafanyabiashara
hao na kubainisha kuwa itafanya juhudi za kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo
ili kuondokana na malalamiko.
Aidha, aliitaka Wizara
hiyo kujikita katika suala la kusomesha na kuwaendeleza wafanyakazi wake katika nyanja tofauti,
ikiwemo za Injinia na nyengine zenye upungufu ili waweze kufanyakazi kwa ufanisi.
Alisema kuna umuhimu wa kuwa na program maalum ya mafunzo ,
itakayotoa fursa kwa wafanyakazi kusoma ndani na nje ya nchi, hatua
aliyobainisha itaiwezesha Wizara kuwa na wataalamu wa kutosha katika kipindi
kifupi.
Sambamba na hilo Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanya
tafiti mbali mbali , ikiwa ni hatua muafaka katika kuzipatia ufumbuzi
changamoto mbali mbali zinazojitokeza.
Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha
huduma zote za Maabara zinafanyika ndani ya Hospitali za Serikali badala ya
kufanyika taasisi zanje, kwa kigezo kuwa Serikali imekuwa ikitenga kiwango
kikubwa cha fedha na kubainisha kuwa huduma za maabara ndio msingi wa matibabu.
Aliushauri uongozi wa Wizara hiyo kuendleea kuviimarisha vituo
vya Afya , hususan vile vilioko vijijini kisiwani Pemba kwa kuvipatia nyenzo,
vifaa tiba na dawa, ili wagonjwa wasikimbilie hospitali ya Abdalla Mzee.
Aidha, aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi kubwa inazoendelea
kuchukuwa katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria, sambamba na kupunguza
kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka asilimia 0.6 hadi kufikia
asilimia 0.4.
Vile vile aliipongeza Wizara hiyo kwa kuandaa mpango mzuri wa
taarifa yake, pamoja na hatua mbali mbali ilizozichukuwa kuimarisha huduma za
Afya hapa nchini.
Nae, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,
Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uongozi wa Wizara ya Afya kwa kuandaa
vyema taarifa hiyo ya utekelezaji.
Aidha, aumeutaka uongozi huo kufanya juhudi kukiimarisha
kitengo cha mifupa katika Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja, ikizingatiwa mahitaji
makubwa yaliopo kutokana na kuwepo ongezeko kubwa la ajali za barabarani hapa
nchini.
Mapema, Waziri wa Wizara Afya Hamad Rashid Mohamed
akiwasilisha muhtasari wa utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara hiyo, alisema
katika kipindi hicho Wizara ilipanga kutumia zaidi ya shilingi Bilioni 57.8 ,
kati yake shilingi Bilioni 47.8 kwa ajili ya Idara na taasisi zilizozomo ndani
ya Wizara hiyo na shilingi Bilioni 9.9 kwa ajili ya Hospitali ya Mnazimmoja.
Alisema Wizara ilipanga kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni
4.6 kutoka vyanzo mbali mbali vya mapato ili kuchangia mfuko mkuu wa Serikali.
Alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo imefanikiwa
kutekeleza shughuli mbali mbali kwa mafanikio makubwa ikiwemo ununuzi wa dawa (shilingi
bilioni nane), hivyo kuwezesha upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya Afya
na Hospitali kwa asilimia 90.
Aidha, alisema katika kipindi hicho gharama za usafirishaji wa
wagonjwa nje ya nchi zilipungua kutoka shilingi 341,292,993 hadi kufikia shilingi 32,186,488 .
Waziri Rashid alisema Wizara ilifanikiwa kuajiri wafanyakazi 479,
ikiwemo madaktari , wauguzi, fundi sanifu maabara na wataalamu wengine.
Alisema kupatikana kwa mashine ya CT Scan mpya katika Hospital
ya Mnazimmoja kutapunguza mrundikano wa wagonjwa wanaosubiri huduma hiyo.
Kuhusiana na uimarishaji wa
miundombinu na majengo, Waziri huyo alisema ujenzi wa Bohari kuu kisiwani Pemba
unaendelea vizuri na unategemewa kukamilika ifikapo mwezi April, mwaka huu.
Alisema miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika
utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na
mabadailiko ya ushuru kutoka Mamlaka ya Kukusaya ushuru Tanzania (TRA),
ambayo kwa kiasi kikubwa umeathiri usafirishaji wa dawa muhimu kutoka MSD
kwenda Bohari ya Dawa (CMS).
Nae, Mshauri wa Waziri katika Wizara hiyo, Dr. Mohamed Saleh
Jidawi, alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya
uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein katika kuimarisha huduma za afya nchini.
No comments:
Post a Comment