Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ameutaka Uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ. Kutoka Elimu Juu ya Camera za CCTV Kwa Wananchi Juu ya Matumizi Yake.UONGOZI wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ umetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya Kamera pamoja na manufaa ya Mradi wa Mji Salama tangu kuanzishwa kwake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ wakati ilipowasilisha Utekelezaji wa Mpango Kazi  kwa kipindi cha Julai hadi Disemba kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Ofisi hiyo inapaswa kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa kuonesha vipindi vya matukio yanayopatikana kutokana na msaada wa mradi wa Mji Salama kupitia CCTV zilizowekwa katika Jiji la Zanzibar hatua ambayo itawapelekea wananchi kuuamini kuwa mradi huo unafanya kazi ipasavyo.

Alieleza kuwa matukio hayo yakiwemo uvunjifu wa sheria iwapo yataoneshwa katika vyombo va habari ikiwemo ZBC Televisheni wananchi watapata kujua umuhimu na kazi za mradi huo kupitia CCTV zilizowekwa katika maeneo yote ya Jiji la Zanzibar.

Rais Dk. Shein alisema kuwa wapo watu ambao bado hawaamini kuwa kamera hizo za CCTV zilizowekwa katika eneo la Jiji la Zanzibar zinafanya kazi na matukio kadhaa yanaonekana hiyo ni kutokana na kutokuwa na elimu yoyote juu ya mradi huo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa hatua hiyo pia, itawapelekea wananchi kujua kuwa mradi huo unafanya kazi zake vyema na unayagundua matukio kadhaa yanayofanywa katika Jiji la Zanzibar.

Alifahamisha kuwa wananchi hawaoni matukio ya kazi za mradi huo kupitia vyombo vya habari kutokana na kutooneshwa hasa kwa yale ya  uvunjaji wa sheria na kueleza haja ya kuoneshwa kwa wale wote wanaosimamia na wanaovunja sheria zikiwemo zie za  barabarani.

Alieleza kuwa kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana hapa Unguja Serikali hivi sasa imo katika mchakato wa kuuendeleza mradi huo kisiwani Pemba hivyo, ipo haja kwa wananchi kuendelea kupewa elimu na kuelezwa mafanikio ya mradi huo.

Aidha, Dk. aliongeza kuwa katika kuhakikisha vitendo vyote vinavyohatarisha amani na usalama vinadhibitiwa ipasavyo Serikali imetekeleza mradi huo ili wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea Zanzibar wakiwemo watalii wanakuwa salama.

Alieleza kuwa Serikali imeamua kuweka vifaa vya kisasa vya ulinzi kwa lengo la kuimarisha  usalama katika mji wa Zanzibar kwani vifaa hivyo vina uwezo mkubwa wa kuwabaini wahusika wa matukio mbali mbali kwa haraka na ufanisi mkubwa.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ameutaka uongozi wa Ofisi hiyo kuongeza juhudi katika kufanya tafiti zinazohusiana na Ofisi hiyo kwa kuzingatia miongozo na maeneo ya Ajenda ya Utafiti ya Zanzibar ya mwaka 2015-2020  sambamba na kuibua maeneo mapya ya utafiti ambayo hayakubainishwa katika mpango huo. Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisisitiza haja kwa Ofisi hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya matokeo yanayopatikana kutoka kwa mradi huo wa Mji Salama kupitia CCTV zilizowekwa katika Jiji la Zanzibar.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha Ofisi yake inazijenga barabara za ndani.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Radhia Rashid Haroub alisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi na kueleza hatua zinazochukuliwa na Ofisi hiyo katika kuhakikisha inatoa huduma zinazopaswa kwa wananchi.

Mradi wa  huo wa Mji Salama ulizinduliwa rasmi mnamo Oktoba 3, mwaka 2018 na Rais Dk. Shein ambapo hatua zote hizo ni kuhakikisha Zanzibar inaendelea kuwa salama huku amani na utulivu ikiendelea kudumishwa hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.