Habari za Punde

Wahamiaji Haramu wanaotumia Usafiri wa Treni kudhibitiwa

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Polisi Mkoani Tabora baada ya kuwasili leo  kwa ziara ya siku moja ambapo alifanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama lengo ikiwa ni kujadili na kupanga mkakati wa kudhibiti wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa kupitia usafiri wa treni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi Barnabas Mwakalukwa,akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapo 
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi Mwandamizi,Mohamed Jihadi, akitoa taarifa ya idara yake kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapo
Afisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Tabora, John Kabissi akitoa taarifa ya idara yake kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(hayupo pichani), wakati wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapo leo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na. Mwandishi Wetu
Serikali imeapa kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali  nchini kwa kutumia usafiri wa treni huku ikiwataka wananchi kuacha tabia ya kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji hao kwani kufanya hivyo ni kinyume cha  sheria.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni, mkoani Tabora  wakati wa kikao na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa baada ya kuwepo kwa taarifa za kiintelijinsia zinazohusisha baadhi ya wahamiaji haramu kutumia usafiri huo kuingia katika mikoa mbalimbali nchini
“Nchi yetu inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu,hivyo ni vyema kudhibiti watu wanaoingia nchini pasina kufuata utaratibu rasmi,na tuna taarifa juu ya wahamiaji haramu sasa kuanza kutumia njia ya treni kuingia nchini tena wengine wakisaidiwa na raia sasa natao onyo wenye tabia hiyo kuacha mara moja na vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi katika maeneo husika” alisema Masauni
Akizungumza katika Kikao hicho,Kaimu Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi,Amiru Sadiki aliiomba serikali kuweka maafisa uhamiaji katika vituo vyote vya reli nchini ili kuweza kukagua wasafiri wanaoingia katika mikoa mbalimbali kama ilivyo katika viwanja vya ndege.
Awali akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,Kamishna Msaidizi wa Polisi,Barnabas Mwakalukwa alisema hali ni shwari huku kukiripotiwa matukio machache.
“Upungufu wa makosa ya mauaji ambayo hapo awali yalikuwa kero kubwa kwa wananchi umetokana na juhudi za polisi katika kufanya doria ya kukamata waganga wa kienyeji wanaojihusisha na ramli chonganishi na tayari jeshi tumeanza operesheni maalumu inayoendelea katika mikoa ya Shinyanga,Geita,Mwanza,Kagera,Simiyu na Tabora huku kukiwa na mafanikio makubwa na hali sasa inaendelea kutulia” alisema ACP Mwakalukwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.