Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar,wakati wa mkutano wa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa mwezi wa Julai hadi Disemba 2019 /2020, uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, (kulia kwa Rais) Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi.Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar. Mhe.Dr. Sira Ubwa.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka
uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuongeza kasi katika
kuitumikia Wizara hiyo kutokana na huduma inazozitoa kuwa muhimu kwa wananchi.
Hayo aliyasema leo, Ikulu
Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji wakati ilipowasilisha Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Disemba kwa mwaka
wa fedha 2019/2020.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein aliipongeza Wizara
hiyo na kuutaka uongozi huo kuendela na kasi ya kufanya kazi vyema ili
mafanikio zaidi yaweze kupatikana kwani wananchi waliowengi wanategemea huduma
zake.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza madhumuni
ya Mkonga wa Taifa hasa Serikalini na kueleza umhimu wa Wizara hiyo kuhakikisha
kuwa kwa upande wa taasisi za Serikali Zaidi inachojali ni kutoa huduma zaidi
kuliko kufanya biashara.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa uongozi wa
Wizara hiyo kuwwaekewa mazingira mazuri zaidi wafanyakazi wake ikiwemo
kuwatunza na kuwapa stahiki zao hasa kwa wale wanaofanya kazi za barabara na
baharini.
Kwa upande mwengine Rais Dk. Shein alieleza kuwa
wapo wale ambao hawana nia nzuri na Wizara hiyo hivyo, ni vyema uongozi
ukawaelewa na kutowawacha wakaendelea
kuharibu na badala yake wawachukulie hatua za kisheria.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kukaa pamoja kwa
Taasisi za Serikali wakati wa maandalizi ya miradi ili kuepuka athari
zinazoweza kutokea hapo baadae.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza umuhimu wa kuwepo
kwa Wakala wa Serikali wa Karakana Kuu ya Vyombo vya Moto Zanzibar ya kisasa itakayotoa huduma bora kutokana na
uwepo wa wataalamu sambamba na vifaa vinavyokwenda na wakati uliopo.
Dk. Shein pia, alisisitiza haja ya kufuatwa sheria
za barabarani hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya madereva hawafuati sheria za
barabarani na kuwataka askari Polisi kufanya wajibu wao kwa kuwakamata na
kuwapeleka mahakamani.
Akitoa wito wa kupambana na muhali kwa wale
wanaovunja sheria zikiwemo za barabarani, Rais Dk. Shein alisema haja ya
kufuatwa sheria na kuondokana na muhali kwani huo ndio unaopelekea watu walio
wengi kuvunja sheria.
Rais Dk. Shein aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi
inazozichukua katika kufuatia miradi ya barabara hasa kisiwani Pemba na kuusifu
uongozi wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wa Wizara hiyo kwa ufuatiliaji wao
huo.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliupongeza uwasilishaji na utayarishaji wa
taarifa hiyo na kueleza kuwa Wizara hiyo imekusanya vyanzo vingi vya mapato
ukiwemo uwanja wa ndege na bandarini hivyo ni lazima watendaji wa wafanyakazi wake
wasiwe wa kubahatisha.
Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza kuwa maeneo
hayo ni ya kiuchumi hivyo masuala ya ulinzi na usalama ni vyema yafanyiwe kazi
kwa azma ya kukuza uchumi wa nchi.
Nae Waziri wa Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji Sira Ubwa Mamboya alisema kuwa kwa kipindi cha robo
mbili (Julai-Disemba 2019) Wizara hiyo imefanikiwa kukamilisha sehemu ya ujenzi
wa barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha lami ikiwemo barabara
ya Ole-Kengeja yenye urefu wa kilomita 35.
Alieleza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unaendelea
na kwa sasa jumla ya kilomita 22.5 zimeshawekwa lami na kazi ya usafishaji kwa
barabara yote umekamilika na ujenzi wa barabara hiyo unaendelea kwa hatua mbali
mbali za kifusi.
Aliongeza kuwa kati ya kilomita 33.8 za barabara
ya Bububu-Mahonda- Mkokotoni, ni kilomita 31 tu zimekamilika kwa kiwango cha
lami ambazo zimo kwenye mradi wa ADB na tayari barabara hii imezinduliwa rasmi
tarehe 10 Januari 2020, matayarisho ya ujenzi kwa kilomita 2.8 zilizobakia kutoka
KwaNyanya hadi Bububu Polisi yameanza.
Kadhalika, alisema kuwa barabara ya kutoka Matemwe
hadi Muyuni (Km7.5) nayo imekamilika kwa kiwango cha lami na barabara ya
Koani-Jumbi imeshawekwa lami kilomita moja kati ya kilomita 6.3 na kazi ya
ujenzi inaendelea.
Alisema kuwa Barabara ya Jozani-Charawe-Ukongoroni
yenye urefu wa kilomita 23 kazi ya ujenzi imeanza rasmi ambapo jumla ya
kilomita 7 zimekamilika kwa kiwango cha kifusi na matayarisho ya kuweka lami
yameanza.
Vile vile, ujenzi wa barabara kutoka Fuoni Polisi
hadi Kibonde Mzungu yenye urefu wa Kilomita 1.2 inaendelea kwa hatua mbali
mbali za kifusi na mategemeo ni kumalizika mwishoni mwa mwezi huu wa Machi
2020.
Aidha, alieleza kuwa ni matarajio ya Wizara hiyo
kuwa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume litakamilika
katika muda uliopangwa hasa ikizingatiwa kuwa Serikali imetenga fedha zake za
ndani ili kukamilisha ujenzi huo..
Alisema kuwa Wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege imefanikiwa kuimarisha huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amani Karume (AAKIA) kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa uwanja kwa
kuzifanyia matengenezo mashine za X-ray nane (8) za ukaguzi pamoja na kuliimarisha
eneo la mizigo na abiria.
Pia, Waziri huyo alieleza kuwa Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege imeanza ujenzi wa uwanja mdogo wa Ndege wa Kigunda (Nungwi) kwa
kujenga maegesho ya Ndege, barabara ya kutulia na kurukia ndege pamoja na
barabara ya kupitia ndege kwa kiwango cha kifusi na sasa kiwanja hicho kimeanza
kazi kwa majaribio.
Pamoja na hayo, Waziri Mamboya alieleza jinsi
Wizara kupitia Shirika la Meli inavyoendelea kuzifanyia matengenezo meli zake
ili ziweze kuendelea kutoa huduma kama kawaida.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mustafa Aboud
Jumbe akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Kazi alieleza jinsi Wizara hiyo
inavyotekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ya barabara na hatua Unguja na Pemba.
Nao viongozi wa Wizara hiyo
waliupongeza na kuusifu uongozi wa Rais Dk. Shein ambao umesaidia kwa kiasi
kikubwa kuimarika kwa huduma za mawasiliano hapa Zanzibar.
Walieleza kuwa mawasiliano
yameweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta za maendeleo
ikiwemo utalii sambamba na hatua kubwa zilizofikiwa katika mradi wa “Mji
Salama” ambapo matumizi ya Kamera za CCTV zimekuwa zikifanya kazi vizuri katika
kuwatambua wahalifu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment