Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Nigeria Nchini Tanzania Mhe.Dk. Sahabi Isa Gada,(kulia kwa Rais) akiwa na Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka Nchini Nigeria, wakiwa katika mazungumzo hayo yaliofanyika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewakaribisha
wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Nigeria kuja kuekeza Zanzibar katika sekta
yoyote wanayoitaka.
Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Sahabi Isa Gada Ikulu Jijini Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe wa wafanyabiashara
na wawekezaji wa Kampuni ya IBRU kutoka
nchini Nigeria.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa
Zanzibar ina rasilimali nyingi za uwekezaji hivyo ni vyema wafanyabiashara na
wawekezaji hao wakaangalia sekta wanayoitaka na baadae kutumia fursa hiyo ya
kuekeza.
Rais Dk. Shein alisema kuwa licha ya Kampuni hiyo
kuwa na uzoefu katika uwekezaji wa sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya uvuvi
ambapo imeweza kuekeza ndani na nje ya Nigeria pia, ni vyema wakaangali
uwezekano wa kuja kuekeza Zanzibar katika sekta nyengine zilizopo.
Alieleza kuwa mbali ya juhudi kubwa
zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya
uvuvi ikiwa ni pamoja na kuifufua Kampuni yake ya uvuvi iliyoanzishwa miaka ya 70
na kuianzisha tena upya miaka mitatu iliyopita bado kunahitajika mashirikiano
ya pamoja na Kampuni zenye uzoefu katika sekta hiyo.
Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo na
ujumbe wake kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka milango wazi kwa
wawekezaji wanaotaka kuja kuekeza Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwawekea
mazingira mazuri kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA).
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar inahitaji
viwanda vya uvuvi hasa ikizingatiwa kuwa imezungukwa na bahari ambayo ina
rasilimali nyingi wakiwemo samaki wenye sifa duniani lakini bado uvuvi wa
bahari kuu haujafanyiwa kazi ipasavyo kutokana na ukosefu wa vifaa, viwanda vya
kuchakata samani na hata utaalamu wa uvuvi wa kisasa.
Alisema kuwa uvuvi ni sehemu ya uchumi wa buluu ambapo
Zanzibar haiko tayari kuachwa nyuma na ndio maana juhudi za makusudi zimekuwa
zikichukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuhakikisha inatekeleza vyema
mchakato huo.
Rais Dk. Shein alieleza imani yake kwa Kampuni hiyo
ya IBRU na kuutaka ujumbe huo kuzitumia fursa hizo zilizopo Zanzibar hasa
ikizingatiwa kuwa Zanzibar na Nigeria zina uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria.
Aliongeza kuwa imefika wakati kwa nchi za bara la
Afrika kuzidisha ushirikiano wa pamoja katika sekta za maendeleo na uchumi hasa
ikizingatiwa kuwa Afrika ina utajiri mkubwa wa rasilimali.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa nchi za
Bara la Afrika kufanya kazi kwa pamoja na mashirikiano ili zipate maendeleo
endelevu kwa manufaa ya Mataifa ya bara hilo pamoja na watu wake.
Aidha, Rais Dk. Shein aliipongeza Serikali ya Nigeria
kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu hapa
nchini ambapo nchi hiyo imeendelea na utamaduni wake wa kuwaleta waalimu wa Sekondari
wa masomo ya Sayansi kuja kusomesha Zanzibar.
Rais Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo ni ya
kihistoria kwani Nigeria pamoja na Ghana ni nchi za mwanzo katika Bara la
Afrika zilizoiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu mara tu
baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.
Nae Balozi wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dk. Sahabi Isa Gada alimueleza
Rais Dk. Shein kuwa ujio wa wafanyabiashara na waekezaji hao kutoka
Nigeria unatokana na mazungumzo aliyoyafanya kati yake na Dk. Shein wakati alipokuja kujitambulisha mnamo Februari 28,
mwaka 2018.
Balozi huyo akirejea mazungumzo aliyozungumza na
Rais Dk. Shein na kusema kuwa miongoni mwa mambo matatu makubwa waliyozungumza ni
pamoja nan chi yake kuleta wawekezaji kuja kuekeza hapa Zanzibar jambo ambalo
amelifanyia kazi.
Balozi Gada alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa
wafanyabiashara na wawekezaji aliokuja nao katika kutoka Kampuni ya IBRU ya
Nigeria wana uzoefu mkubwa katika uwekezaji wa sekta mbali mbali na tayari wameshaekeza
nchi kadhaa katika bara la Afrika.
Alisema kuwa wawekezaji hao wanauzoefu na wameweza
kuekeza ndani na nje ya Nigeria zikiwemo sekta za uvuvi, mawasiliano, hoteli na
utalii, kilimo, usafiri wa anga, mafuta na gesi asilia, usafiri na usafirishaji
wa baharini pamoja na sekta ya habari.
Aidha, Balozi Gada alimueleza Dk. Shein kuwa Kampuni
hiyo iliyoanzishwa mwaka 1956 imejikita sana katika sekta ya uvuvi kwa nchi ya
Nigeria na tayari ina mtandao mkubwa katika kufanya shughuli zake za uvuvi kwa
nchi za Magharibi mwa Afrika kama vile Togo, Cameroun, Benin, Mauritania,
Gambia, Angola, Namibia pamoja na bahari ya Irish.
Sambamba na hayo, Balozi Gada alimueleza Rais Dk.
Shein hatua zinazochukuliwa na Serikali yake kwa mashirikiano ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika
kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya Sayansi pamoja na mashirikiano kwa vyuo
vikuu kikiwepo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Nao wawekezaji na wafanyabiashara hao walimueleza
Rais Dk. Shein jinsi walivyovutiwa na mazingira ya Zanzibar sambamba na
rasilimali na ukaribu wa watu wake na kuahidi kuja kuekeza.
Walieleza kuwa kutokana na fursa zilizopo hapa
Zanzibar wako tayari kuja kuekeza na kuahidi kuendelea na mchakato kwa kukutana
na taasisi husika zikiwemo Wizara na Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi
Zanzibar (ZIPA) na Wizara ya Kilimo.
Sambamba na hayo, wafanyabiashara na wawekezaji
hao walieleza uwezo walionao wa kuekeza kutokana na Kampuni yao ya IBRU jinsi
ilivyojiimarisha huku wakisisitiza namna
ya sekta ya elimu ilivyoimarika nchini Nigeria na kueleza haja ya kushirikiana
na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment