Habari za Punde

Serikali Imewataka wanaouza Bidhaa za Kujikinga dhidi ya Covid-19, Kuuza kwa Bei iliyoko Sokoni


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari(hawapo pichani), kuhusu bidhaa za kujinga na Covid-19, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei, Waziri amewataka waache hiyo tabia kabla ya kuchukuliwa hatua kali, kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TBS. Dkt. Ngenya, na kulia ni Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), John Mduma katika mkutano na Waanshi wa Habari Jijini Dar es Salaam.


Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO                                                                                               
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Taasisi mbalimbali za Serikali imejipanga vyema kukabiliana na changamoto zinazohusiana na mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Covid-19).
Katika kuhakikisha changamoto hizo zinatatuliwa mapema hii leo Waziri Innocent Bashungwa ametembelea viwanda vinavyozalisha sabuni na Vitakasa mikono vilivyoko Jijini Dar es Salaam kuangalia bei ya bidhaa hiyo na kuwaagiza wafanyabiashara kuuza kuendana na bei iliyoko sokoni.
Katika mazungumzo na Waandishi wa Habari yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri Bashungwa alisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Serikali yanalenga kuwasaidia wananchi kujua hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa ili kujinga na Covid-19.
“Watanzania wote tunawiwa kuwa na mchango katika kupambana dhidi ya kuenea Covid-19, watalaam kutoka tume ya Ushindani (FCC), katika maeneo ya kuuzia barakoa (face masks), vikinga mkono (gloves), vitakasa mikono na kemikali za usafi wa mazingira (Hand sanitizer and surface disinfectant) katika eneo la Dar es Salaam watalaam wamebaini kuwepo kwa uhaba na changamoto ya kupanda bei kwa bidhaa hizo”, Alisema Waziri Innocent Bashungwa.
Waziri Bashungwa Amewataka wafanyabiashara kuacha njama za makusudi za kuficha bidhaa hizo kwa kigezo cha kuadimika hali ambayo inasababisha kupungua kwa uwezo wa kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo wa Covid-19 kwa kuzuia maambukizi mapya.
Aidha Waziri Bashungwa alisema kuwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limebainisha kuwepo na umuhimu wa wazalishaji wa bidhaa za kujikinga na maambukizi mapya ya Covid-19, hususani kwa wazalishaji wa Vitakasa mikono (Hand Sanitizer)  kuzingatia viwango vilivyoweka na Shirika hilo.
“Kiwango kilichowekwa kwa uzalishaji wa vitakasa mikono ni Na. TZS 1650: 2014, kiwango hiki kinahusisha pia uwepo wa kileo (alcohol) ya walau asilimia 60 kuwezesha vitakasa mikono kuweza kufanya kazi iliyokusudiwa, kwa hiyo nawaelekeza TBS kushirikiana na wazalishaji waliopo na wapya ili kukidhi matumizi ya bidhaa hizo ili kuwawezesha wananchi kupata bidhaa yenye kiwango bora ili kudhibiti janga hili,” Alisema Waziri Bashungwa.
Alibainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na taasisi zake imeendelea kufanya ukaguzi na uchunguzi sokoni ili kubaini endapo kuna vitendo vyovyote vya udanganyifu au vinavyokiuka sheria zinazosimamiwa na taasisi hizo ikiwemo TBS  katika kuzalisha, kuingiza,  kusambaza na kuuza bidhaa hizo.
Aliongeza kuwa kumekuwepo na udanganyifu wa bei za bidhaa hizo za kujinga dhidi ya Maambukizi ya Covid-19, hususani vitakasa mikono, kwa mujibu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), mil.250 inauzwa Tsh. 5,500, lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiuza kwa Tsh. 20,000, huku mil. 60 ikiuzwa Tsh. 2,500 lakini kwenye baadhi ya maduka  wanauza  kwaTsh.8,000, na amewataka wafanyabiashara kuuza kulingana na bei iliyoko sokoni.
“Nawaelekeza TBS na FCC kuendeleo kuchunguza bei,  uzalishwaji, uingizwaji wa bidhaa unaozingatia viwango vya ubora na ushindani  wa soko ili bidhaa hizi zipatikane kwa urahisi , zikidhi matarajio ya matumizi na zipatikane kwa bei ya soko, kwahiyo kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa hizo kwa bei ya juu wakibainika wafutiwe leseni ili tuone wataenda kuuza wapi”, Alisema Bashungwa
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini TBS, Dkt. Yusuph Athuman Ngenya amewataka wananchi kuepuka habari za utengenezaji wa Vitakasa mikono, ikihusisha uwepo wa kiwango cha Alcohol kwa asilimia 60 ambacho ndiyo kiwango cha chini cha kutengeneza bidhaa hiyo ili iweze kupambana na Covid-19.
“Kuhusu ubora na kiwango cha chini cha Alcohol kwenye vitakasa mikono ni asilimia 60 ambacho kimebainishwa kwenye kiwango cha 1650: 2014 cha TBS, lakini pia tunahusika kwa kiasi kikubwa kudhibiti bidhaa zinazoingia nchini kwahiyo tumejipanga kulinda ubora wa vitakasa mikono hasa vinavyotoka nje ya nchi ili kupata bidhaa bora kwa matumizi ya wananchi kujikinga na Covid-19,” Alisema Dkt.Athuman.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.